Solomon Mukubwa |
Mwimbaji wa nyimbo za Injili wa Nchini Kenya na mwenye asili ya Kongo, Solomon Mukubwa ameelezea jambo lililopelekea kupoteza mkono wake wa kushoto.
Solomon anasema akiwa na Umri wa Miaka 12, Uvimbe ulianza katika mkono wake wa kushoto, na hivyo wazazi wake walimchukua na kumpeleka katika hospitali mbalimbali na hata kwa waganga wa kienyeji ili kufahamu chanzo cha uzimbe huo lakini kote huko hawakufanikiwa kujua chanzo cha uvimbe huo.
Solomon aliishi na uvimbe huo kwa Miaka 3. Baadaye ilifunguliwa hospitali flani ya wazungu iliyokuwa karibu na nyumbani kwao hivyo wazazi wake walimpeleka hapo pia, lakini majibu yakawa ni yale yale. Madaktari wa hospitali hiyo baada ya kuona uvimbe unazidi na hawaoni chanzo cha uvimbe huo, walishauri mkono wa Solomon Mukubwa ukatwe ili kunusuru maisha yake.
Solomoni aliendelea kusema kuwa hakuna
mtu aliyejua kuwa uvimbe huo umetokana na nini lakini hapo baadae
ilidhihirika wazi kuwa mama yake wa kambo ndie aliyemroga na
kumsababishia tatizo hilo kwani baadae alikuja kukiri na kueleza
ukweli.
Solomoni ambaye kwa sasa maskani yake yapo jiji la Nairobi nchini Kenya
anasema wimbo wake wa Mfalme wa Amani aliutunga ili kumtukuza Mungu
baada ya kumuepusha na kifo ambacho kingempata baada ya mama yake wa
kambo kumroga na kusababisha mkono wake kuvimba na kutibiwa na madaktari
bingwa bila mafanikio na hata alipoenda kwa waganga wa kienyeji pia
hakupona.
“Wimbo wangu wa Mfalme wa amani niliamua kuuimba baada kuvuka katika
shida hizo na albamu yangu kuipa jina la Mungu mwenye nguvu, na kuna
maneno niliweka kwenye kibao hicho kwamba, ukiwa na shida usiende kwa
waganga wa dunia, mwite mfalme wa amani, yeye anajibu maombi,” alisema
Solomoni Mukubwa.