|
Na Mwl. Christopher Mwakasege |
“Basi Yesu akawaambia, Amini, amin, nawaambieni, Msipoula mwili
wake Mwana wa Adamu na kunywa damu yake, hamna Uzima ndani yenu. Aulaye
mwili wangu na kuinywa damu yangu anao UZIMA WA MILELE; nami nitamfufua
siku ya mwisho. Kwa maana mwili wangu ni chakula cha kweli; na damu
yangu ni kinywaji cha kweli. Aulaye mwili wangu na kuinywa damu yangu
hukaa ndani yangu, nami hukaa ndani yake. Kama vile Baba aliye hai
alivyonituma mimi, nami ni hai kwa Baba; kadhalika naye mwenye kunila
atakuwa hai kwa mimi” (Yohana 6:53-57).
Mtu ambaye ameula mwili wa Kristo na kuinywa damu yake ile
iliyomwagika msalabani, ni yule ambaye anakaa ndani ya Yesu Kristo, na
Yesu Kristo anakaa ndani yake. Kwa maneno mengine amepokea uzima wa
Mungu, ambao ni uzima wa milele. Unapompokea Yesu Kristo moyoni mwako unapokea uzima wa milele; kwa kuwa, “Ndani yake ndimo ulimokuwa uzima, nao ule uzima ulikuwa nuru ya watu” (Yohana 1:4).
Inatupasa tukumbuke ya kuwa, kwa mtu mmoja Adamu, dhambi iliingia
ulimwenguni, na kwa dhambi hiyo mauti; na hivyo mauti ikawafikia watu
wote kwa sababu wote wamefanya dhambi.
Pia, inatupasa tukumbuke ya kuwa, “ikiwa kwa kukosa mtu mmoja
mauti ilitawala kwa sababu ya yule mmoja, zaidi sana wao wapokeao wingi
wa neema, na kile kipawa cha haki, watatawala katika UZIMA kwa yule
mmoja, Yesu Kristo” (Warumi 5:17).
Dhambi inapoingia mahali inaleta mauti, magonjwa, uasi, ubishi,
umaskini na kutokufanikiwa. Uzima wa milele unapoingia ndani ya mtu
unaleta, – Uzima, uponyaji, amani, upendo, utajiri na kufanikiwa na
baraka zingine za Mungu.
UZIMA WA MILELE NA UPONYAJI
Kabla sijampokea Yesu Kristo moyoni mwangu awe Bwana na Mwokozi wangu, nilisumbuliwa sana na magonjwa.
Nakumbuka nilikuwa nasumbuliwa na maumivu ya kichwa mara kwa mara.
Nilipokwenda kupimwa hospitali kwa daktari, niliambiwa nina ugonjwa wa
vidonda vya tumbo ‘Ulcers’ na pia ‘High blood pressure’. Nilipewa dawa za kutumia, na pia niliambiwa nisile vyakula vya aina fulani maana vitaniongezea ugonjwa.
Niliyafuata masharti ya daktari, na nilipata nafuu kidogo. Lakini
kitu cha kushangaza ni kwamba mara kwa mara magonjwa yalinirudia na
kunisumbua sana – sikujua kitu cha kufanya. Baada ya miaka kadha neema
ya Bwana ilifuniliwa moyoni mwangu, nikaokoka baada ya kutubu na
kumpokea Yesu Kristo kuwa Bwana na Mwokozi wangu. Mabadiliko yaliyotokea
katika maisha yangu ni makubwa mno. Wakati huo nilikuwa sijajua ni kitu
gani kimetokea – lakini nilijua kuwa ninaishi maisha mapya.
Nilishangaa kuona kuwa miezi kadhaa imepita bila kusumbuliwa na
magonjwa. Kichwa hakikiniuma tena, moyo uliacha kwenda mbio tena vyakula
vingine nilivyokatazwa nisile na daktari havikunidhuru nilipovila tena
kama mwanzo. Nilijua hakika kuwa nimepona!
Wakati huo sikuweza kufahamu kitu kilichotokea hata nikapona mara
moja namna hiyo. Lakini kwa kadri ambavyo Roho Mtakatifu alivyoendelea
kunikuza katika wokovu nilikuja kufahamu ya kuwa MSAMAHA WA DHAMBI
UNAONGOZANA NA UPONYAJI WA MWILI.
Kabla ya mwanadamu kutenda dhambi, hakukuwa na magonjwa. Dhambi
ilipoingia ilileta na magonjwa pia. Sadaka ya uhai wa Yesu Kristo
msalabani ilileta msamaha na ondoleo la dhambi na madhara yake yote
ikiwa ni pamoja na MAGONJWA.
Unapompokea Yesu Kristo moyoni mwako kuwa Bwana na Mwokozi wako,
unampokea MPONYAJI. Roho wa Uzima wa milele anayeingia kutawala maisha
yako, ni Roho wa Uponyaji anayefukuza magonjwa yote ndani yako na kukupa
afya.
Ndiyo maana imeandikwa hivi; “Hata kulipokuwa jioni,
wakamletea (Yesu Kristo) wengi wenye pepo; akawatoa pepo kwa neno lake,
akawaponya wote waliokuwa hawawezi, ili litimie lile neno lililonenwa na
nabii Isaya, akisema, Mwenyewe aliutwaa udhaifu wetu, na KUYACHUKUA
MAGONJWA YETU” (Mathayo 8:16,17). Soma pia (Isaya 53:4,5)
Kwa kuwa alichukua dhambi zetu, dhambi hizo zimeondolewa kwetu, na
tumepokea utakatifu wake. Kwa kuwa alichukua magonjwa yetu, hakuna
sababu ya sisi kuendelea kuumwa kwa kuwa tumepokea uponyaji wake. Ndiyo
maana imeandikwa hivi;
“Yeye mwenyewe (Yesu Kristo) alizichukua dhambi zetu katika
mwili wake juu ya mti; ili tukiwa wafu kwa mambo ya dhambi, tuwe hai
kwa mambo ya haki; na KWA KUPIGWA KWAKE MLIPONYWA” (1Petro 2:24).
Angalieni anasema, “ Kwa kupigwa kwake MLIPONYWA” na siyo ‘MTAPONYWA’. Ikiwa TULIPONYWA kwa hiyo sasa TUMEPONA!
Ndiyo maana watu wengi sana nimewasikia wakishuhudia ya kuwa magonjwa
yaliyokuwa yanawasumbua kwa muda mrefu yamepona baada ya kumpokea Yesu
Kristo mioyoni mwao na kuokoka.
Kuna mama mmoja alinishuhudia ya kuwa alisumbuliwa sana na majini kwa
muda wa miaka kumi na mitatu. Alikwenda hospitali – hakupona. Alikwenda
kwa waganga wa kienyeji – hakupona. Mwili wake ulidhoofu sana.
Siku moja neema ya Mungu ilimzukia aliamua kuokoka. Mhubiri aliposema
watu wanaotaka kuokoka waje mbele, huyo mama naye alikwenda – akafanya
sala ya toba na kumkaribisha Yesu Kristo moyoni mwake.
Mama huyo alinambia tangu wakati huo maumivu aliyokuwa nayo mwilini
kwa miaka 13 yaliondoka. Mume wake na ndugu zake walishangaa sana. Tangu
wakati huo aliookoka na kupona hadi alipokuwa ananisimulia ilikuwa
imepita miaka minne, na bado alikuwa amepona na afya njema.
Kama wewe unayesoma haya unaumwa na hujaokoka, nakushauri utubu
dhambi zako na umpokee Yesu Kristo moyoni mwako, na DAMU YAKE
itakutakasa, na utapokea uponyaji unaouhitaji sasa. Kwa sababu
imeandikwa, “ Akusamehe maovu yako yote, akuponya magonjwa yako yote” (Zaburi 103:3).
UZIMA WA MILELE NA MABADILIKO YA TABIA
“Hata imekuwa, mtu akiwa ndani ya Kristo amekuwa kiumbe kipya; ya kale yamepita; tazama! Yamekuwa mapya” (2Wakorintho 5:17)
“Naye alituokoa katika nguvu za giza, akatuhamisha na
kutuingiza katika ufalme wa Mwana wa pendo lake; ambaye katika yeye
tuna ukombozi yaani, msamaha wa dhambi”.(Wakolosai 1:13,14).
Yesu Kristo alisema ukiula mwili wake na ukiinywa damu yake yeye
anakaa ndani yako na wewe unakaa ndani yake – unapokea uzima wake au
uzima wa milele.
Mtu akiwa ndani ya Kristo, anakuwa mtu mpya. Mtu anapokuwa ndani ya
Kristo anabadilika tabia yake kwa kuwa amehamishwa toka katika nguvu za
giza na tabia yake na kuingia katika ufalme wa Kristo na tabia ya
Kikristo.
Mtu akiwa ndani ya Kristo anavua utu wake wa kale na kuvaa utu mpya – anavaa tabia mpya. Wakati fulani nilikuwa mji fulani hapa nchini nikihubiri mkutano wa
siku nane, asubuhi moja alikuja mzee mmoja kuniona katika hotel
niliyokuwa ninakaa.
Yule mzee akasema; “ Unakumbuka jana ulipoita watu wanaotaka kuokoka waje mbele waombewe, kuna mtoto mmoja alikuwa wa kwanza kufika mbele”.
“Ndiyo, nakumbuka”; Nikamjibu.
Yule mzee akaendelea kusema; “Yule mtoto ni wa kwangu, na tangu jana kumetokea mabadiliko makubwa mno ya tabia, nikaona heri nije nikushirikishe”.
Nikamuuliza, “Kumetokea mabadiliko gani?”
“Huyu mtoto wangu”; yule mzee alieleza; “Kabla
ya jana alipoamua kuokoka, alikuwa si mtii, alikuwa hapendi usafi,
alikuwa hawezi hata kutandika kitanda chake akiamka asubuhi. Hata
tukimwambia afagie uwanja unaozunguka nyumba yetu alikuwa hasikii.
Kweli, tumempiga fimbo mpaka tuliogopa tutamuumiza. Lakini kuanzia jana
alipookoka (sisi tulifikiri anatania) tabia yake imebadilika kabisa.
Amekuwa mtii, kazi anajituma kufanya, amekuwa msafi, hata wakati wa
usiku, anachukua biblia na kusali yeye mwenyewe – maajabu haya”.
Usikose Muendelezo wa Somo hili Jumatano ya Wiki Ijayo.