Na Mwl. Christopher Mwakasege |
- Inaendelea -
Yesu Kristo alisema ukiula mwili wake na kuinywa damu yake, yeye
atakaa ndani yako na wewe utakaa ndani yake unapokea uzima wake wa
milele unaokuvika tabia ya Uungu.
Haya ndiyo yaliyotokea kwa huyu mtoto mdogo wa umri wa miaka kumi na
miwili. Huyu mtoto alipompokea Yesu Kristo na kuokoka – Kiroho aliula
mwili wa Yesu na kuinywa damu yake – akapokea uzima wa milele, Yesu
Kristo aliingia ndani ya mtoto, na mtoto akaingia ndani ya Yesu Kristo –
yote yalifanyika kwa Uwezo wa Roho Mtakatifu.
Unadhani mtoto huyu alipata wapi ujasiri wa kufanya sala yeye mwenyewe, kitu ambacho alikuwa anaogopa kufanya kabla hajaokoka?
Jibu lake ni – Damu ya Yesu Kristo! Imeandikwa hivi; “Basi ndugu, kwa kuwa tuna ujasiri wa kupaingia patakatifu kwa damu ya Yesu…….” (Waebrania 10:19).
Niliwahi kukaribishwa katika mkoa mwingine kuhubiri katika Kanisa
fulani, nakumbuka kuwa nilihubiri juu ya Bartimayo yule kipofu
aliyeponywa na Yesu Kristo kule Yeriko. Nilipomaliza mahubiri
nilikaribisha watu waje mbele wale wanaotaka kuokoka na kuombewa
magonjwa. Watu wengi waliokoka na pia kuponywa maradhi yaliyokuwa yanawasumbua.
Baada ya wiki moja kupita, alikuja mtu mmoja nyumbani kwangu
tukasalimiana na nikamkaribisha aingie ndani. Alipokwisha kukaa kwenye
kiti, akaniuliza akasema; “ Mlimpa kitu gani ndugu (alitaja jina lake) siku mlipokuja kuhubiri kanisani kwetu – maana mimi sikuwepo.”
Nikamuuliza, “Kwani kumetokea nini?”
Yule mgeni akasema; “Huyo ndugu alikuwa hawezi kunywa chai ya
maziwa wala maziwa – akinywa maziwa alikuwa anaugua. Nilishangaa siku
moja alifika nyumbani, nilipomkaribisha chai ya rangi alikataa, akasema
sasa anakunywa chai ya maziwa bila shida yoyote.“
“Nilipomuuliza ameanza lini kunywa chai ya maziwa, akasema
tangu baada ya maombi ya Jumapili pale Kanisani. Lakini pia, niliona
tabia yake imebadilika. Alikuwa hachani nywele- sasa anachana. Alikuwa
mlevi sana – sasa haonji tena pombe. Alikuwa mchafu, hajijali –
nilishangaa kumwona amevaa nguo safi. Ni kitu gani mlimpa?”
Nikamjibu nikasema; “ Sisi tulichokifanya ni kuhubiri habari
za Yesu Kristo na uwezo wake. Ndugu yako alifungua moyo wake siku ile,
akampokea Yesu Kristo moyoni mwake ili awe Bwana na Mwokozi wake
akaokoka. Pia tukamuombea tatizo la ugonjwa alilokuwa nalo na Bwana
akamponya”.
Ni jambo la kumsifu Mungu sana katika Kristo, kwa sababu baada ya
huyo ndugu kuokoka, na maisha yake kubadilika – sasa hivi ana kazi nzuri
ya kuajiriwa na pia, ni mhubiri wa injili. Jina la Bwana libarikiwe!
Huwezi ukampokea Yesu Kristo moyoni mwako na bado ukawa na tabia
uliyokuwa nayo zamani. Unapompokea Yesu Kristo moyoni mwako – unapokea
Uzima wa milele unaokupa tabia ya Uungu.
Yesu Kristo alisema hivi; “ Amini, amini, nawaambieni,
msipoula mwili wake Mwana wa Adamu na kuinywa damu yake hamna Uzima
ndani yenu…..Aulaye mwili wangu na kuinywa DAMU YANGU hukaa ndani yangu,
nami hukaa ndani yake. Kaeni ndani yangu, nami ndani yenu. Kama vile
tawi lisivyoweza kuzaa pekee yake, lisipokaa ndani ya mzabibu; kadhalika
nanyi, msipokaa ndani yangu. Mimi ni mzabibu; ninyi ni matawi akaaye
ndani yangu nami ndani yake, huyo huzaa sana; maana pasipo mimi ninyi
hamwezi kufanya neno lolote…….Ninyi mkikaa ndani yangu, na maneno yangu
yakikaa ndani yenu, ombeni mtakalo lote nanyi mtatendewa” (Yohana 6:53,56; Yohana 15:4,5,7)
Mtume Paulo alisema; “ Hata imekuwa, mtu akiwa NDANI YA KRISTO amekuwa kiumbe kipya; ya kale yamepita; tazama! Yamekuwa mapya” (2 Wakorintho 5:17).
Mtume Paulo alisema hivi katika waraka wake wa pili kwa watu wote,
sura ya kwanza mstari wa tatu na wa nne; “Kwa kuwa uweza wake wa Uungu
umetukirimia vitu vyote vipasavyo uzima wa utauwa, kwa kumjua yeye
aliyetuita kwa utukufu wake na wema wake mwenyewe. Tena kwa hayo
atumetukirimia ahadi kubwa mno, za THAMANI, ili kwamba kwa hizo mpate kuwa WASHIRIKA WA TABIA YA UUNGU, mkiokolewa na uharibifu uliomo duniani kwa sababu ya tamaa”.
- Mwisho -
- Mwisho -