|
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Mh. Leonidas Gama |
MKUU wa Mkoa (RC) wa Kilimanjaro, Leonidas Gama, anatarajiwa
kuwa mgeni rasmi katika ufunguzi wa tamasha la sherehe za miujiza
linalotarajiwa kuanza saa tisa hadi saa 12 jioni.
Tamasha hilo la siku tano linaloanza leo, limeandaliwa na Umoja wa
Makanisa ya Kipentekoste (PCT) Kilimanjaro kwa kushirikiana na Shirika
la Sos Mission kutoka Sweden.
Mhubiri wa kimataifa, Johannes Amritizer, atahubiri na kuendesha
kongamano la masuala ya uongozi kwa watumishi mbalimbali wa taasisi
binafsi na za serikali katika Uwanja wa Mashujaa ulioko mjini Moshi.
Akizungumza mjini Kilimanjaro, Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi,
Askofu Samweli Yohana, alisema maandalizi yote yamekamilika na waumini
kutoka madhehebu mbalimbali watahudhuria tamasha hilo.
Alisema lengo la tamasha hilo ni kuliombea taifa amani na mshikamano pamoja na kuwahimiza watu kutii sheria bila shuruti.
Askofu Yohana alisema tamasha hilo litakalomalizika Novemba 10, mwaka huu litahudhuriwa na wageni 120 kutoka Marekani.
Alisema waimbaji mbalimbali ikiwamo kwaya ya waumini kutoka madhehebu maarufu kama Mass wataimba katika tamasha hilo.
Pia alitoa wito kwa wakazi wa Moshi pamoja na mikoa ya jirani
kuhudhuria tamasha hilo la miujiza ambalo halina kiingilio chochote.
- Tanzania Daima -