Upendo Nkone |
MSANII, Upendo Nkone, amekuwa wa kwanza kuthibitisha kushiriki
Tamasha la Krismasi litakalofanyika Uwanja wa Taifa jijini Dar es
Salaam, Desemba 25.
Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya tamasha hilo, Alex Msama,
alisema jana kwamba tayari wamefikia makubaliano na msanii huyo na bado
wanaendelea na mazungumzo na wasanii wengine wa nje na ndani ili
kuhakikisha tamasha hilo la nyimbo za kumsifu Mungu linafana.
“Nafurahi kuwajulisha wapenzi wa muziki wa kiroho kuwa, kamati yangu
tayari imefikia makubaliano na Nkone, hivyo mambo yatakuwa mazuri
kadiri siku zinavyokaribia,” alisema Msama.
Mwimbaji huyo anatamba na nyimbo kama ‘Upendo wa Yesu’, ‘Hapa
Nilipo’, ‘Mungu Baba’, ‘Yesu Aliniita’, ‘Sikiliza Nikuambie’,
‘Usiogope’, ‘Ijaposema’, ‘Uumbaji’, ‘Yesu Nakupenda’, ‘Kanisa’ na
‘Habari Njema’.
Nyimbo nyingine ni ‘Niacheni Niimbe’, ‘Nimebaki na Yesu’, ‘Uniongoze
Yesu’, ‘Nakuhitaji’, ‘Acha Uovu’, ‘Yesu Atakutunza’ na ‘Moyo Wangu’.
Msama aliongeza kuwa Tamasha la Krismasi litakuwa bora zaidi kuliko
la Pasaka, ambako wataalika wasanii maarufu kutoka nje na ndani ya
Tanzania na kwamba, litakuwa tamasha kubwa la nyimbo za kumsifu Mungu.
Tamasha la Krismasi linaandaliwa na Kampuni ya Msama Promotion ya
jijini Dar es Salaam, ambayo pia huandaa Tamasha la Pasaka kila mwaka.
- Tanzania Daima -