Edward Lowassa |
WAZIRI Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, ameelezea kusikitishwa
kwake na kiwango duni cha elimu katika shule za sekondari za kata na
hata baadhi ya vyuo vya elimu ya juu.
Akizungumza katika harambee ya kuchangia Mfuko wa Elimu wa Kanisa la
Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa Kijitonyama jijini
Dar es Salaam jana, Lowassa alisema kiwango cha elimu katika shule hizo
kinamsikitisha kwani ni cha chini.
“Napenda niseme wazi kuwa kiwango cha elimu katika shule zile za kata
na baadhi ya vyuo vikuu kwa kweli ni cha chini, hili mimi
linanisikitisha sana kwa sababu elimu bora ni mkombozi kwa mtoto wa
Kitanzania,” alisema.
Lowassa ambaye pia ni mbunge wa Monduli na muasisi wa shule hizo za
kata, alipongeza kanisa kwa kusaidia juhudi za serikali katika
kuimarisha na kuboresha elimu ambapo shule nyingi za kanisa zimekuwa na
kiwango cha juu cha elimu.
“Sasa napenda Watanzania kupitia kwenu niwaonyeshe hawa marafiki
zangu ambao wamekuwa wananisindikiza katika harambee, maana kumekuwa na
maneno maneno,” alisema.
Lowassa alitoa kauli hiyo baada ya wakili maarufu, Sadock Magai
kuwasilisha michango ya marafiki wa mwanasiasa huyo katika harambee
hiyo.
Marafiki hao walichangia sh milioni 50. Mbali ya wakili Magai,
wengine ni Lawrance Masha, Innocent Macha, Bashir Awale, Hamis
Kindoroko na Lemmy Bathelemew.
Lowassa pia alisindikizwa na mbunge wa Segerea ambaye pia ni Naibu
Waziri wa Kazi na Ajira, Dk. Makongoro Mahanga aliyechangia sh milioni 3
na mbunge wa Kinondoni, Idd Azan aliyechangia sh milioni 2.
“Nampongeza na kumshukuru sana Mh. Idd Azan kwa kuja kwake
kunisindikiza na kuchangia, hii ndiyo Tanzania ninayoijua, isiyo na
dini, watu wa dini zote mnashirikiana,” alisema.
Katika harambee hiyo, jumla ya sh milioni 615 zikiwa ni fedha taslimu
pamoja na ahadi zilipatikana na kuvuka lengo ambalo lilikuwa sh
milioni 250.
- Tanzania Daima -