James Kalekwa |
Shukrani
Bwana Yesu
asifiwe! Naomba nianze mafundisho kwenye safu hii kwanza kwa kumshukuru Mungu
kwa kunipatia mke mwema kwaajili ya kulitumikia kusudi lake. Kwangu imekuwa ni
furaha na shangwe kubwa sana… Nimekuwa nikisubiri kwa shauku kubwa sana.
Pili
niushukuru uongozi na watendaji wa Gospel News Media kwa maombi na maneno ya
kunitia moyo kwenye shughuli hii iliyoyabadili maisha yangu. Na zaidi ya hapo
ninawiwa kuwashukuru wasomaji wa safu hii wale walioniandikia ujumbe mfupi wa
maneno (SMS), email, kunipigia simu na namna zote za mawasiliano. Wamo ambao
waliniombea na kunitamkia mema bila kuwasiliana nami moja kwa moja- Nyote
mmefanyika baraka kwenye maisha yangu na hasa siku hiyo kubwa kwangu.
Mimi na mke wangu tunafurahi sana
kumtumikia Mungu pamoja na kila mmoja wenu! Sasa karibu tuambatane kwenye mafundisho haya…
Tunakupenda na Mungu anakupenda zaidi.
Maneno
Baada ya kujifunza kwa kiasi juu ya mawazo ndani ya
Mwamba wa kwanza unaozungumza juu ya milango ya fahamu na kazi zake. Tafadhali
niruhusu nikuchukue hatua moja mbele. Baada ya muda kiasi, mawazo yanapofanya
kazi ndani ya mtu au mtu anapoyatunza mawazo hayo na kuanza kuyakubali (kwa
kujua ama kwa kutokujua), hatua mpya huzaliwa nayo huwa ni hatua ya maneno.
Kwahiyo maneno ni mawazo yaliyotamkwa!
Mithali 6:2
"Basi
umetegwa kwa maneno ya kinywa chako, umekamatwa kwa maneno ya kinywa
chako."
Mithali 12:13
"Mtu atashiba mema kwa matunda ya kinywa
chake; Na atarudishiwa matendo ya mikono yake."
Kitu ninachotamani ujifunze hapa ni kwamba “Ukiri
wako ndiyo umiliki wako, ukiri wako ndiyo ukomo wako.” – Your confesion is your
possesion, your confesion is yout limitation! Kwahiyo kile unachokikiri ndiyo
huamua ni kwa kiasi gani uende.
Kimantiki ni sawa kabisa kwasababu kila
unapotamka maneno unajua nani huwa wa kwanza kuyasikia maneno/matamshi hayo?
Jibu ni rahisi sana…. Wewe mwenyewe! Kila unapofungua Kinywa kutamka neno, wewe
huwa wa kwanza kusikia kile ulichotamka kuliko mtu mwingine yeyote na huenda
wewe ukawa muathirika au mfaidikaji wa kwanza juu ya maneno hayo kabla ya mtu
yeyote.
Hebu nikuonyeshe mifano kadhaa kabla hatujavuka
hatua nyingine: Unafahamu kwenye maisha ya elimu hasa kwenye ngazi za
sekondari, kuna wanafunzi ambao walijiona ni wadhaifu kwenye masomo fulani
mathalani hesabu/hisabati na kwa kujiona hivyo nimeshuhudia wengi wakijisemea
“Mimi nasoma ili nipate D tu ya somo hili.” Au “Mimi si mjuzi sana wa hesabu
hivyo ninasoma ili nisipate F”.
Umeshawahi kusikia wanafunzi ambao wamekuwa na
maandalizi dhaifu au kwa sababu nyingine yoyote hujisemea “Mimi hata nikipata
Division III (Daraja la tatu la ufaulu) inatosha kabisa…”….Je, ndugu hao hupata
tofauti sana na ukiri wao? Je, watu wanaweka juhudi zao kusoma ili wapate alama
D hujikuta wamepata alama A? Je, ndugu watafutao Division III hujikuta wamepata
Division I?
HAPANA!!! Kanuni za kiroho zinaniambia “umetegwa kwa maneno ya
kinywa chako”. Ukitamka ya kwamba wewe si mshindi, tafadhali kumbuka kuwa mtu
wa kwanza anayesikia na kuelewa vyema sana maana ya taarifa hiyo ni wewe
mwenyewe.
Naomba kuweka mkazo sana juu ya jambo muhimu sana:
kuwa na ukiri/maneno/matamshi yale yale pasipo kujali mazingira, nyakati, watu
– consistence in confesions. Ili uyaone matunda halisi ya kinywa chako unapaswa
kutunza ukiri au maneno ya kinywa chako… Unatakiwa kuwa ni mtu mwenye msimamo
ule ule wa kimaneno juu ya hali fulani japo utumizi wa lugha unaweza kubadilika
lakini maana ya maneno iwe ni ilele.
Kuna kitu kwenye lugha ya kiingereza wanaita
“doublé standards” yaani kigeugeu au hali ya kubadilikabadilika kama kinyonga
hivi. Kuna ndugu ambao wao hukiri au huwa na maneno yaliyo na utofauti mkubwa
sana kama mbingu na nchi juu ya hali zile zile… Yaani maneno yao hukinzana sana
juu ya jambo moja ambalo walipaswa kuwa na usemi uleule.
Kwa mfano, kuna ndugu
ambao juu ya hali ya uchumi na maendeleo ya maisha yao hukiri kwamba
wamefanikiwa na Baadaye hujikuta wanakiri juu ya kutokufanikiwa- huukiri
utajiri na Baadaye huukiri umaskini.
Yaani mtu wa namna hii akikaa na ndugu
wanaowaza na kukiri utajiri hujikuta anakiri vivyo hivyo au anafanania na
wanaokiri utajiri na kisha mtu huyo huyo akijikuta mingoni mwa ndugu wanaopenda
kuukiri umaskini juu ya maisha yao naye hujikuta anakiri umaskini!
Kwahiyo ni
dhahri ya kwamba mtu huyo hana ukiri mmoja (consistence in confesion) juu ya
hali ya kiuchumi… Ni mtu mwenye kigeugeu! Mungu akusaidie sana usiwe na namna
hiyo ya maisha! Tunza sana ukiri wako, tunza sana maneno ya kinywa chako.
1 Timotheo
6: 13
“Nakuagiza
mbele za Mungu anayevihifadhi hai vitu vyote, na mbele za Kristo Yesu,
aliyeyaungama maungamo mazuri yale mbele ya Pontio Pilato.”
Biblia ya
kiswahili inatumia neno “maungamo” ambalo miongoni mwa watu wengi hujenga dhana
ya toba au kujutia dhambi na kuomba msamaha! Lakini kwenye mstari huu
haimaanishi hivyo… Si unajua Yesu hakutenda dhambi na hakuwahi kuwa mwenye
dhambi? Kwahiyo mbele ya Pilato hakuwa anatoa maungamo uyajuayo…
Kwa kutumia
mwanga/ufahamu wa vitabu vya Injili (Yohana sura ya 18&19; Luka sura ya 23;
Marko sura ya 15 na Mathayo sura ya 27). Nakushauri ukipata muda usome kwenye
injili hizo. Yesu hakukinzana katika ukiri wake- ndiyo yake ilikuwa ni ndiyo na
hapana yake ilikuwa ni hapana.
Haijalishi nani alisimama mbele yake, haijalishi
nani alimuhoji maswali, haijalishi vitisho au mazingira aliyokuwamo hakubadili
ukiri wake… Aliungama maungamo yaliyo mema! Na matokeo yake, Yesu ni sawa sawa
na maungamo yake… Alikiri juu ya ufalme, aliungama juu ya mamlaka aliyonayo,
alitamka juu uungu wake na “akashiba matunda ya kinywa chake”! Hatimaye akawa
sawasawa na ukiri wake – He eventually became as His confesión!
Kitu
ninachotamani sana ndani ya moyo wangu kiumbike na kufanyika halisi kwako ni
kwamba asikudanganye mtu – huwezi kuwa tofauti na ukiri wako! Kuna watu wanomba
na kumwamini Mungu juu ya kupata wenzi wa kuwafaa kwenye maisha yao kisha baada
ya Maombi wanaungana na wanadamu wa
kawaida kulalamika na kukiri “Siku hizi hakuna mapenzi, hakuna upendo… sidhani
kama nitapata mwenzi.”.
Kwa ukiri huo wanayafuta Maombi waliyowekeza muda wao
mwingi! Ndugu, usiwe kigeugeu, usiwe na “double
standards” ndiyo yako na iwe ndiyo, na siyo yako na iwe siyo!
Kumbuka
sana maneno hukuwekea wewe ukomo/mipaka ya utendaji wako…
Huwezi kuyavuka!
Kwahiyo ningependa kukushauri ya kwamba ni heri ukatumia muda wako kujibidiisha
kulijua neno la Mungu na baada ya hapo uanze kulikiri neno la Mungu juu ya hali
mbali mbali za maisha na hilo ndilo lifanyike ukiri wako.
Somo litaendelea Jumatatu Ijayo.....
Mafundisho haya yameandaliwa na James Kalekwa
Mwanataaluma, Mwandishi wa vitabu na Mwalimu wa Neno la Mungu
+255 714 762 669
+255 754 917 764