Upendo Kilahiro |
BAADA ya msanii Upendo Nkone kuthibitisha kushiriki Tamasha la
Krismasi litakalofanyika Desemba 25, mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es
Salaam, msanii Upendo Kilahiro naye amejitosa kushiriki.
Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya tamasha hilo, Alex Msama,
alisema jijini Dar es Salaam jana kuwa tayari wamefikia makubaliano na
msanii huyo na wanafurahi kwamba tamasha litaenda vile wanavyotaka.
“Kilahiro tutakuwa naye, naamini mwaka huu tamasha hili litakuwa bora
zaidi kutokana na kushirikisha waimbaji wengi wakali,” alisema na
kuongeza kuwa hadi sasa Watanzania wawili wameshakubaliana nao, yaani
Kilahiro na Upendo Nkone na bado wanaendelea na mazungumzo na wasanii
wengine wa nje na ndani ya nchi.
Baadhi ya nyimbo za msanii huyo ni ‘Zindonga’ aliyoimba Kizulu,
‘Unajibu Maombi’ na ‘Ni Salama Rohoni’. Pia anatamba na albamu
mbalimbali ikiwamo ‘Ficho Langu’.
Tamasha la Krismasi linaandaliwa na Kampuni ya Msama Promotions ya
jijini Dar es Salaam, ambayo pia huandaa Tamasha la Pasaka kila mwaka.
Waandaaji hao wamepanga tamasha hilo lifanyike Desemba 25 Uwanja wa
Taifa, Dar es Salaam na siku inayofuata Uwanja wa Jamhuri, Morogoro.
- Tanzania Daima -