Solomon Mukubwa |
MWIMBAJI mahiri wa muziki wa Injili, Solomon Mukubwa atashiriki
Tamasha la Krismasi lililopangwa kufanyika Desemba 25, mwaka huu kwenye
Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya tamasha hilo, Alex Msama
alisema jana kuwa tayari wamemalizana na Mukubwa ambaye ni raia wa
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) anayeishi Kenya.
“Pia tumemalizana na mwimbaji wa hapa nchini anaitwa John Lissu
ambaye ni mmoja kati ya waimbaji mahiri na wenye mashabiki wengi.
“Dhamira yetu ni kuwa na wasanii wote wanaokubalika na mashabiki,”
alisema Msama na kuongeza kuwa Desemba 26, mwaka huu tamasha hilo
litafanyika Uwanja wa Jamhuri Morogoro.
Mukubwa ametamba na albamu mbalimbali ikiwemo Usikate Tamaa, ambayo
ina nyimbo kama Mungu Wangu Nitetee, Niko na Yesu, Mke Si Nguo, Moyo
Tukuza Bwana, Chunga Ahadi Yako na Yesu Jina Zuri na Usikate Tamaa.
Pia Mukubwa amewahi kutoa albamu mbili ambazo ni Sijaona Rafiki na
Mungu Mwenye Nguvu. Sijaona Rafiki Kama Yesu ambayo ni albamu yake ya
kwanza ina nyimbo za Uwe Nami Bwana, Sijaona Rafiki Kama Yesu,
Nitayainua Macho, Matendo ya Mungu, Bwana Wastahili na Yesu Kimbilio.
Wasanii wengine wameshathibitisha kushiriki tamasha hilo la nyimbo za
kusifu na kuabudu ni Watanzania, Rose Muhando, Upendo Nkone na Upendo
Kilahiro wakati wa nje ni Ephraim Sekeleti wa Zambia.
- Habari Leo -