Rose Muhando |
Mwimbaji wa Nyimbo za Injili toka Tanzania, Rose Muhando ameshindwa kutokea kwenye Tamasha la Uzinduzi wa Album ya Mwimbaji wa Nyimbo za injili toka Tabora, Mch. Egon Israel, Album ijulikanayo kama "Nakuombea Jirani".
Rose Muhando alialikwa kuimba kwenye Tamasha hilo kwa Gharama ya Sh. Milioni 2, pesa iliyolipwa kupitia Akaunti ya Rose Muhando ya Benki ya NMB.
Kwa Mujibu wa Maelezo ya Mchungaji Egon Israel, kutokufika kwa Rose Muhando kwenye Tamasha hilo, kumeingiza hasara ya Sh. Milioni 15, huku watu waliofika kwenye Uzinduzi huo wakirudishiwa pesa zao.
Tamasha hilo lilifanyika Jana katika Uwanja wa Ally Hassan Mwinyi huku Mkuu wa Mkoa wa Tabora Bi. Fatma Mwasa akiwa ndiye Mgeni rasmi.
Katika kutuliza vurugu zilizotokana na kutokufika kwa Rose Muhando, Kikosi cha Kutuliza Ghasia(FFU) Mkoani Tabora, walifika Uwanjani hapo ili kutuliza Ghasia hizo.
Mpaka sasa, waandaji wa Tamasha hilo wanafanya jitihada za kumtafuta Rose Muhando kujua sababu ya yeye kutokufika katika Tamasha hilo, huku waandaji hao wakidai kuwa Rose hapatikani kwenye simu yake toka jana, na mara chache anapopatikana hataki kupokea simu zao.
Hii si mara ya kwanza kwa Rose Muhando kutokufika kwenye Matamasha anayoalikwa, huku sababu za Msingi zikiwa hazijulikani.