Kardinali Mstaafu Domenico |
MWADHAMA Kardinali mstaafu wa Kanisa Katoliki nchini Italia, Domenico
Bartolucci (Pichani) aliyefariki dunia akiwa na umri wa miaka 96,
anatarajiwa kuzikwa leo.
Kwa mujibu wa taarifa, Kardinali Bartolucci ambaye aliwahi kuwa
kiongozi wa kwaya ya kanisa dogo la Sistine jijini Vatican City,
amefariki Novemba 11.
Katika salamu zake za rambirambi, Kiongozi wa Kanisa hilo, Papa
Francis alisema alikuwa mtu wa upendo na padri aliyeheshimika na
waamini.
Baba Mtakatifu alisema marehemu atakumbukwa kwa safari yake ndefu ya
kutangaza Neno la Mungu kupitia utunzi wake wa nyimbo za dini.
“Marehemu Kardinali Bartolucci alikuwa ni mtu aliyejitoa kwa moyo
wake wote kwa ajili ya kumtukuza na kumsifu Mungu,” alisema Papa
Francis.
Taarifa iliyopatikana makao makuu ya kanisa hilo inasema, Mkuu wa
makardinali, Angelo Sodano leo anatarajiwa kuongoza ibada ya maziko
katika Kanisa Kuu la St. Peter’s Basilica.
Baada ya ibada hiyo, Baba Mtakatifu anatarajiwa kujiunga na maelfu ya
waomboezaji wanaotarajiwa kufika kumsindikiza mpendwa wao katika safari
ya mwisho.
Kihistoria, akiwa tayari mwanafunzi wa muziki alipata daraja la
upadri mwaka 1939 sanjari na Diploma ya muziki kutoka Chuo cha Muziki
Florence.
Mwaka 1942 alikwenda jijini Roma nchini Italia kuongeza ujuzi wake
katika muziki na kwa muda mfupi alianza kuongoza kwaya katika Kanisa la
St. John Lateran.
- Jambo Leo -