Askofu Simalenga afariki Dunia.
Askofu wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Kusini Magharibi mwa Tanganyika, Jimbo la Njombe, John Simalenga (60), amefariki
ghafla akiwa nyumbani kwake Njombe, Mkoa Mpya wa Njombe, baada ya kuugua kwa muda mfupi.
Akizungumza na waandishi wa habari jana,
Katibu Mkuu wa Kanisa hilo nchini, Dickson Chilongani alisema Askofu
huyo alifariki jana saa 11 alfajiri baada ya kuugua malaria na kupelekwa katika Hospitali ya Dayosisi hiyo.
"Marehenu Askofu Simalenga siku moja kabla
ya mauti, aliugua malaria na kupelekwa katika Hospitali ya Dayosisi, baada
ya kupimwa aligundulika kuwa na kisukari pamoja na presha kuwa juu," alisema Chilongani.
Aliongeza kuwa, baada ya kufanyiwa vipimo
aliruhusiwa kurudi nyumbani na kupewa dawa wakiamini zitamsaidia lakini
hali yake ilibadilika ghafla na kufikwa na umauti.
Chilongani aliwataka Wakristo wote nchini,
kuungana na familia ya marehemu katika kipindi hiki kigumu ambapo
taratibu za mazishi zinaendelea kufanyika.
Marehemu Askofu Simalenga alizaliwa Novemba
30,1953 katika Kijiji cha Milo, Wilaya Ludewa, mkoani Iringa. Alimaliza
elimu ya msingi mwaka 1997 na 1971 alihitimu kidato cha nne.
Mwaka 1973 alihitimu kidato cha sita ambapo
mwaka 1974-1977 alijiunga na Chuo Kikuu nchini Kenya na baadaye alienda
nchini Uingereza kupata Shahada ya pili katika chuo cha Hull.
Amewahi kuwa Askofu Mkuu katika Kanisa la
Mtakatifu Andrea Njombe, Mchungaji kiongozi Kanisa la Mtakatifu Albano,
Dar es Salaam na kufundisha katika Chuo cha Mtakatifu Mark's.
- Gazeti la Majira -