Dr. Mohammed Gharib Bilal |
MAKAMU wa Rais, Dk. Mohammed Gharib Bilal, amezindua Benki ya
Maendeleo ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi
ya Mashariki na Pwani huku akiitaka kukabiliana na changamoto
zinazoikabili sekta ya fedha nchini.
Akizungumza wakati wa hotuba ya uzinduzi wa benki hiyo jijini Dar es
Salaam jana, Dk. Bilal alisema changamoto tatu zinazoikabili sekta ya
fedha ni uhaba wa matawi ya benki vijijini, kiwango kikubwa cha riba na
mikopo ya masharti magumu inayowakwamisha watumiaji.
Dk. Bilal alisema ujio wa Mendeleo Bank uwe chachu ya kushinda vita
katika kukabiliana na changamoto hizo ili kutanua wigo wa ongezeko la
watumiaji wa huduma za kibenki na kuharakisha maendeleo ya Mtanzania na
taifa kwa jumla.
Uzinduzi huo ulihudhuriwa na viongozi mbalimbali, akiwamo Meya wa
Ilala, Jerry Silaa, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mecky Sadick na
Naibu Waziri wa Fedha, Janeth Mbene aliyeupongeza uongozi kwa wazo la
kuuza hisa ili kupata mtaji wa kuanzishia benki.
Akimkaribisha Dk. Bilal, Askofu Mkuu wa KKKT, Dk. Alex Malasusa,
alisema Maendeleo Bank inaamini kuwa fedha ni damu ya uchumi duniani,
hivyo imejizatiti kuongeza idadi ya watu ndani ya mtandao wa fedha ili
kuharakisha ukuaji wa maendeleo.
“Sisi tupo tayari kwa jukumu hilo na tutakabiliana na changamoto
hiyo, lakini tunaiomba serikali kupigania uimara wa taasisi za kifedha
ili kuzipa nguvu katika kuharakisha maendeleo ya Watanzania na taifa,”
alisema Dk. Malasusa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Maendeleo Bank, Ibrahim
Mwangalaba, alimshukuru Dk. Bilal kuzindua benki hiyo kwa niaba ya Rais
Jakaya Kikwete, na kwamba Watanzania watakaojiunga watafanya uamuzi
sahihi.
- Salum Mkandemba -