Rebecca Malope |
MASHABIKI wengi wa muziki wa injili nchini wameomba malkia wa
muziki huo nchini Afrika Kusini, Rebecca Malope, asikose katika Tamasha
la Krismasi mwaka huu.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya tamasha hilo,
Alex Msama, hadi sasa katika maombi wanayoyapokea, wadau wengi wamekuwa
wakimpigia chapuo Malope, ambaye amewahi kuja nchini kutumbuiza kwenye
Tamasha la Pasaka.
“Homa ya Tamasha la Krismasi imeanza kupanda, mashabiki wamekuwa
wakiomba safari hii tusiache kumualika Malope, yapo maombi mengi,
lakini hilo la Malope linaongoza, kwamba lazima awepo tamasha la
Krismasi Dar es Salaam,” alisema Msama.
Malope amewahi kutamba na albamu za ‘Saturday Nite’ (aliyoitoa
Januari 1, 2009), ‘Hlala Nami’ (Novemba 11, 2003), ‘Siyabonga’ (Desemba
21, 2000), ‘Free at Last’ (Novemba 18, 1997), ‘African Classics’ (Mei
5, 2009), na ‘Greatest Hits’ (Januari 10, 2006).
Tamasha la Krismasi linaloandaliwa na Kampuni ya Msama Promotion ya
jijini Dar es Salaam, ambayo pia huandaa Tamasha la Pasaka kila mwaka,
linatarajiwa kufanyika Desemba 25 jijini Dar es Salaam.
Aidha, Msama alibainisha kuwa Kamati ya Maandalizi ya Tamasha la
Krismasi, imeamua lifanyike Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Desemba 25
na siku inayofuata wataangalia mkoa gani waupe heshima.
Alisema hilo litakuwa tamasha kubwa la nyimbo za kumsifu Mungu na
litakuwa na tofauti kubwa ukilinganisha na mengine yaliyowahi
kuandaliwa na kampuni yake.
- Tanzania Daima -