KANISA la Tanzania Assemblies of God lililopo Chanika, Dar es
Salaam, limenusulika kuungua moto baada ya watu wasiofahamika kutaka
kulichoma moto kwa kutumia mafuta ya petroli.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Ilala, Marietha Minangi, alisema tukio hilo
lilitokea juzi, saa 8:30 usiku.
Alisema watu wasiofahamika walifika kanisani hapo na kidumu cha
mafuta ya petroli pamoja na mpira uliotumika kuingizia mafuta ndani ya
kanisa hilo ambapo katika tukio hilo viti 20 vya plastiki vimeteketea
kwa moto.
Kamanda Minangi alisema mpaka sasa wamekamata watu wanaowatilia shaka kuhusika na tukio hilo.
Mchungaji wa kanisa hilo, Fidelisi Kalinga, alisema hawana uhasama na
majirani zao na wanashirikiana vizuri, ila alikiri kuwapo kwa uhasama
wa kiimani na kupokea vitisho vinavyoashiria uvunjifu wa amani.
- Zawadi Chogogwe -