WANAKIJIJI zaidi ya 75 wa Kata ya Nyalikungu katika Halmashauri
ya Wilaya ya Maswa, wameulalamikia uongozi wa Kanisa Katoliki Jimbo la
Shinyanga kwa kuwapokonya eneo lao la kilimo lenye ukubwa wa ekari 600.
Kwa mujibu wa nakala za mahakama, wanakijiji hao awali walifungua
shauri la madai namba 6 la mwaka 2012 kudai eneo hilo na kushinda kesi
hiyo lakini hadi sasa uongozi wa kanisa haujawakabidhi eneo hilo.
Hata hivyo baada ya wanakijiji kushinda kesi hiyo, kanisa nalo
lilikata rufaa ambapo hukumu ilitolewa kuwa hakuna mshindi bali
kinachohitajika ni maelewano baina ya pande hizo mbili.
Wanakijiji hao ambao waliwakilishwa na Charles Ndaha, ambaye katika
shauri hilo alidai kuwa eneo lenye mgogoro kati yao na jimbo liko katika
Kata ya Nyalikungu ambalo kanisa linadaiwa kuvamia kwa kujenga Shule
ya Seminari ya Shanwa.
Kutokana na sintofahamu katika kesi hiyo, wanakijiji waliamua kukaa
kikao cha pamoja kujadili hatima ya mashamba yao na kukubaliana
kulifuatilia suala hilo kwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya
Makazi.
Mjumbe aliyehudhuria mkutano huo,
Richard Masele, alisema tangu eneo hilo lichukuliwe na kanisa wanakijiji
hawaruhusiwi kulima wala kukatisha.
Ofisa Ardhi wa Wilaya ya Maswa, Elikana Duda, alisema
kwa njia ya simu kuwa wananchi wana haki ya kumiliki eneo hilo, kwamba tatizo ni
kudanganywa kwa aliyekuwa Mkuu wa mkoa wakati wa kutoa vibali.
Alisema kesi ilisikilizwa na wananchi walishinda lakini suala hilo
lilikuwa gumu, kwani baadaye waliliingiza kidini, licha ya wamiliki
halali kujulikana kuwa ni wananchi.
- Tanzania Daima -