Papa Francis |
KIONGOZI wa Kanisa Katoliki, Papa Francis, ametuma waraka kwa
maaskofu duniani kote kuomba mawazo yao kuhusu changamoto mbalimbali
zinazolikabili kanisa la sasa, likiwemo suala la familia za kisasa na
ndoa ya jinsi moja kama sehemu ya mageuzi makubwa katika mafundisho ya
kanisa hilo yanayofanywa.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na makao makuu ya kanisa hilo,
dodoso hilo limetumwa kwa maaskofu kuwauliza kwa kina kuhusu hali
nyingi mpya zinazojitokeza sasa, zinazopaswa kuangaliwa kwa umakini na
kanisa kwa huduma ya kichungaji.
Mambo ambayo yalikuwa vigumu kujadiliwa na kusikilizwa hadi miaka
michache iliyopita, yamejitokeza sasa kama matokeo ya hali tofauti
kutoka.
Wachunguzi na masuala ya dini walisema dodoso hilo lina maswali 39
mengi yakiwa mambo ambayo kwa kawaida ni yale ambayo yalikuwa
hayajadiliwi na kanisa hilo hadi miaka kadhaa ya karibuni.
Kujadiliwa kwa vitendo hivyo kunaweza kutafsiriwa kuwa ni ishara ya
uwazi kuongezeka kwa huduma za kichungaji bila kujali historia ya
muhimu kama ilivyokuwa zamani.
Akizungumzia kuhusu ndoa za mashoga, Papa katika waraka huo
amenukuliwa akiuliza swali “ni uangalizi gani makini wa kichungaji
unaopaswa kutolewa na kanisa kwa watu waliochagua aina hiyo ya maisha?”
Pia kwa muungano wa ndoa za jinsi moja ambazo wamepata watoto kwa
njia ya kuwarithi, anauliza “nini kifanyike kwa familia za aina hii kwa
busara ya kichungaji ili kupeleka mwanga wa imani kwao.”
Aidha, kuhusu kuoa au kuolewa tena wanandoa waliopewa talaka ambao
chini ya sheria ya sasa hawaruhusiwi kupokea komunio takatifu, dodoso
linauliza kama wanahisi kuwa wametengwa au wanakabiliwa na tatizo gani
kutokana na kutokuwepo uwezekano wa wao kupokea sakramenti.
Kuhusu talaka, dodoso limehoji maaskofu waseme wanakabiliana vipi na
hali hiyo kwa busara za kichungaji kwa kazi za kila wanapokumbana na
tatizo hilo.
Hoja ya talaka inatarajiwa kuwa mojawapo ya mambo ya kujadiliwa na
kanisa katika Sinodi ya Maaskofu mwaka 2015, kwa hiyo kutajwa katika
dodoso hii kumetafsiriwa kama maandalizi ya sinodi ili ifikapo mwaka
2015 kanisa liweze kuunda miongozo ya kufanya kazi katika huduma za
kichungaji katika ngazi ya mtu mmoja mmoja na katika ngazi ya familia.
Mkuu wa Sinodi ya Maaskofu, Lorenzo Kardinali Baldisseri, aliwaambia
waandishi mada ya mkutano huo kuwa sinodi ni nzuri na inaonyesha vizuri
zaidi bidii ya kichungaji ambayo Baba Mtakatifu anataka mbinu mpya za
kutangaza injili kwa familia katika dunia ya leo.
- Tanzania Daima -