Waziri Mkuu Mizengo Pinda akiweka Shada la Maua katika Kaburi la Marehemu Askofu Simalenga |
Waziri Mkuu akiaga Mwili wa Marehemu |
Katika ibada hiyo iliyofanyika jana,
Waziri Mkuu alisema Dayosisi imepoteza mhimili muhimu lakini akawataka
wawe na umoja na upendo huku wakiendelea kumtumainia Mungu.
“Mhashamu Baba Askofu Simalenga
alisimikwa Julai 6, 2008. Ni miaka mitano tu ya utumishi kwenu na
alikuja wakati ambapo Dayosisi hii ilikuwa imekaa kwa miaka 10 bila ya
kuwa na kiongozi. Siku anawekwa wakfu nilikuwepo na ninakumbuka mlimuomba asaidie kuleta mshikamano,” alisema Waziri Mkuu.
Ibada ikiendelea |
Aliendelea kusema, “Nawaomba
wanadayosisi muwe na upendo na mshikamano mkubwa miongoni mwenu hadi
hapo Mungu atakapotupatia kiongozi mwingine. Tumuombe Mungu ili kiongozi
huyu ajaye apatikane kwa njia ya amani.
Alimuomba mke wa marehemu, Martha pamoja
na watoto wa marehemu kupokea msiba huo kwa mikono miwili na kuahidi
kuwaombea faraja kwa Mwenyezi Mungu.
Mwili wa Marehemu ukiwekwa Kaburini |
Waziri Mkuu ambaye alishiriki maziko kwa
niaba ya Serikali, alitumia fursa hiyo kuwapa pole maaskofu, mapadri,
watawa na familia zikiwa ni salamu maalumu kutoka kwa Rais Jakaya
Kikwete ambaye alisema yuko ziarani kwenye Mkoa mpya wa Simiyu.
Spika wa Bunge, Anne Makinda ambaye pia
ni Mbunge wa Njombe Kusini ilipo Dayosisi hiyo, akitoa salamu za
rambirambi alisema wana Njombe wamepungukiwa na nguvu kwa kuondokewa na
kiongozi huyo wa dini.
“Alisaidia kuleta umoja hapa kwetu,
tumempoteza mtu muhimu sana katika harakati za maendeleo ya wilaya yetu
na mkoa kwa ujumla. Alisaidia kuleta umoja na upendo na sisi tuwe na
upendo na amani, tuendelee kumuomba Mungu hadi tutakapoletewa msimamizi
mwingine,” alisema Makinda.
Waziri Mkuu akiweka udongo katika Kaburi la Marehemu |
Katika mahubiri yake, Askofu Mkuu wa
Kanisa la Anglikana Tanzania, Jacob Chimeledya alitaka waumini wote
kumtazama Mungu na wamtegemee kwa sababu licha ya kwamba wanampenda
askofu wao, ameona ni vema ampunzishe mtumishi wake.
“Sote tunajua kuwa katika kipindi chake,
Dayosisi hii ilitulia kabisa je tutaruhusu kuondoka kwake kuzue tena
chokochoko? Msiba huu usifike mahali ukaanza kututenganisha na kutoa
mwanya wa kuanza kunyoosheana vidole. Tumuombe Mungu atusaidie afute
machozi yetu,” alisema.
Askofu John Andrea Simalenga alizaliwa
Novemba 30, 1953 na kufariki Novemba 24, 2013 baada ya kuugua kwa siku
mbili. Novemba 22, mwaka huu alijisikia vibaya na alipopimwa alikutwa na
malaria, kisukari na shinikizo la damu.
Alilazwa Hospitali ya Kibena, Njombe na
kuruhusiwa siku iliyofuata lakini Novemba 24 alizidiwa tena na kuaga
dunia. Ameacha mjane na watoto wanne.
- Habari Leo, Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu -