Solly Mahlangu |
MWIMBAJI Solly Mahlangu wa Afrika Kusini amekubali kutumbuiza kwenye
Tamasha la Krismasi linaloandaliwa na Kampuni ya Msama Promotion ya Dar
es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mkurungenzi wa Msama
Promotion, Alex Msama alisema mwimbaji huyo atakuja pamoja na waimbaji
wake kwani anamiliki kikundi chake cha muziki wa Injili.
“Nashukuru maandalizi ya tamasha yanaendelea vizuri na naamini
tamasha la mwaka huu litavutia kuliko yaliyotangulia kwani mwimbaji toka
Afrika Kusini, Solly Mahlangu ambaye anaimba baadhi ya nyimbo zake kwa
lugha ya Kiswahili amekubali kuja,” alisema Msama.
Baadhi ya nyimbo ambazo Solly Mahlangu ameimba kwa ludha ya Kiswahili
ni Mwamba mwamba na Ee baba na zimewavutia waumini wengi hasa kwenye
kuabudu.
Alisema ujumbe wa mwaka huu ni “Tanzania ni ya Watanzania, tutailinda na kuidumisha amani yetu.”
Msama alisema mwimbaji huyo anatarajia kushiriki katika tamasha hilo
jijini Dar es Salaam, tamasha ambalo litafanyika pia katika mikoa ya
Morogoro (Desemba 26), Tanga (Desemba 28), Arusha (Desemba 29) na Dodoma
(Januari mosi).
Aidha, Msama alisema bado wanaendelea kufanya mazungumzo na waimbaji
wengine yameshakamilika kwa waimbaji wa ndani na nje ya Tanzania ikiwa
ni pamoja na Solomon Mukubwa (Kenya), Ephraim Sekeleti (Zambia), Liliane
Kabaganza (Rwanda).
Waimbaji wa Tanzania ni pamoja na Rose Muhando, Upendo Nkone, Upendo Kilahiro, Edson Mwasabwite, New Life Band na John Lissu.
- Habari Leo -