Advertise Here

Thursday, April 25, 2013

Ufaransa yahalalisha ndoa za Jinsia Moja.

Bi. Christiane Taubira, Waziri wa sheria wa Ufaransa
Watunga sheria wa Ufaransa wamehalalisha ndoa za jinsia moja baada ya miezi ya mjadala mkali na maandamano ya mitaani yaliyopelekea mamia kwa maelfu kwenda Paris.

Kura 331 dhidi ya 225 za siku ya jumanne zimeangukia kwa walio wengi ndani ya bunge ambao ni Socialist. Waziri wa sheria wa Ufaransa Christiane Taubira, amesema ndoa ya kwanza kufungwa itafanyika mapema mwezi june.

Wanaopinga sheria hiyo wanasema Ufaransa haiko tayari kuhalalisha ndoa za jinsia moja, na kura zinaonyesha kuwa wafaransa wamejitenga juuu ya swala hilo.

Mamia ya askari walimwagwa nje ya viwanja vya bunge kabla ya kura hizo kupigwa, kwa maandalizi ya kama kungekuwa na maandamano kuzunguka jengo la bunge na kando kando ya Mto Seine.

Ufaransa ni nchi ya 14 ya kuhalalisha ndoa za jinsia moja, na kura ya Jumanne imekuja wiki moja baada ya New Zealand kuruhu wanandoa wa jinsi moja kuoana.

Mambo ya kuzingatia katika kipindi cha Uchumba.

Mpenzi msomaji tunakusalimu kwa jina la Yesu!
Baada ya kuwa tumepata maombi ya vijana wengi kutaka kujifunza habari za Uchumba, mke wangu pamoja nami tumeona ni vema tukaandaa somo hili ambalo tunaamini litafanyika msaada kwa vijana wengi ambao wapo kwenye uchumba au wanajiaandaa kuingia katika eneo hili. Hata hivyo somo hili ni pana sana, kwa sasa tumeandika vitu vichache vya msingi, tunaamini kwamba huko mbele tutaandika kitabu chake rasmi.

Katika kitabu cha Muhubiri 3:1 Biblia inasema “Kwa kila jambo kuna majira yake, na wakati kwa kila kusudi chini ya mbingu”. Hivyo mwanadamu katika maisha yake hapa chini ya jua  kuna vipindi mbalimbali anavyovipitia hii ni pamoja na kipindi cha uchumba kwa sehemu kubwa ya watu.  

Katika kipindi hiki yapo mambo mengi ambayo wachumba hufanya, mengine ni mazuri na mengine hayafai kabisa. Na hii yote inatokana hasa na mitazamo au tafsiri ya uchumba kwa watu husika. Fahamu kwamba tafsiri unayokuwa nayo juu ya mchumba wako ndiyo inayokuongoza kujenga mahusiano ya aina fulani pamoja naye.

Lengo la somo hili ni;
Kuongeza ufahamu wa wachumba kuhusu kipindi hiki na Kuwapa vijana maarifa ya kuwasaidia kuishi kwa nidhamu ya Ki-Mungu katika uchumba wao. Pia ni kuwafikirisha vijana wanaotarajia kupita katika kipindi hiki mambo ya kuzingatia. Si wachumba wengi wanajua, Mungu anawataka wafanye nini katika uchumba wao au kwa lugha nyingine si wachumba wote wanaojua kwa nini kipindi cha uchumba kipo. Naam katika somo hili tumeandika mambo hayo kinaga ubaga.

Kwa kuwa suala la uchumba ni pana na lina mitazamo mingi, yafuatayo ni mambo tuliyozingatia katika uandishi wa somo hili;
  • Kuna makundi mbalimbali ambayo yana taratibu zao kuhusu mchakato wa mtu kumpata mke au mume kikiwepo kipindi cha uchumba. Makundi hayo ni pamoja na makanisa, makabila, familia nk.
  • Wachumba wanaweza kutofautiana kwa kiwango cha elimu, uchumi, ufahamu juu ya mambo mbalimbali, kikabila, umri na hata kwa rangi pia.
  • Kuna baadhi ya wachumba hadi kufikia muda wanakubaliana kwamba watakuja kuishi pamoja walishafahamiana tangu zamani na wengine hawakufahamiana.
  • Wachumba wanaweza wakatoka katika madhehebu/makanisa tofauti na hili ni kwa kuzingatia madhehebu/makanisa mengi yaliyopo.
Lengo letu ni kuandika juu ya mwongozo wa Neno la Mungu katika kipindi cha uchumba. kwa lugha nyingine, je Mungu anataka wachumba wafanye nini katika kipindi chao cha uchumba?. Kumbuka uchumba ni kipindi/wakati. Basi kama ni wakati jua kabisa kuna baadhi ya mambo ambayo ni lazima yafanyike, kwani Biblia inasema katika Mhubiri 8:5b “ Na moyo wa mwenye hekima hujua wakati na hukumu”, neno hukumu linamaanisha maamuzi, mambo ya kufanya.   

Yafuatayo ni mambo ya msingi kufanya katika kipindi cha uchumba;

Jambo la kwanza –  Mruhusu Roho Mtakatifu afanyike Bwana wa uchumba wenu
2Wakorinto 3:17 ‘Basi Bwana’ ndiye Roho; na alipo Roho wa Bwana, hapo ndipo penye uhuru’.
Kumbuka Roho Mtakatifu ni msaidizi. Hivyo basi ni vema kumtumia vema hasa katika nyanja hii ya mahusiano katika kipindi hiki cha uchumba. Ni Roho Mtakatifu pekee mwenye uwezo wa kukujulisha mambo na siri nyingi kuhusu mchumba wako hata kama yeye hataki kukueleza. Ukimruhusu Roho Mtakatifu afanyike Bwana, yeye atakuongoza katIka kufanya maombi yanayolenga maeneo ya msingi juu ya huyo mwenzako. Kila mtu ameumbwa pamoja na mapungufu fulani au kwa lugha nyingine mapungufu/ udhaifu (weakness) ni sehemu ya maisha ya mwanadamu. Roho Mtakatifu anapokuwa Bwana wa mahusiano yako yeye atakusaidia kuona madhaifu au mapungufu ya mwenzako kama kitu cha wewe kujivunia(Strength) kwa maana ya kuona udhaifu wa mwenzako kama kitu chema na si kibaya.

Kumbuka Paulo katika 2Wakorinto 12:9-10. —‘Basi nitajisifia udhaifu wangu kwa furaha nyingi, ….kwa hiyo napendezwa na udhaifu——- maana niwapo dhaifu ndipo nilipo na nguvu. Hivyo Roho Mtakatifu atabadilisha tafsiri ndani yako za vyote unavyoona kwa mwenzako huenda juu ya umbile lake, umri wake, macho yake, kabila lake viwe vitu vya wewe kujivunia. Zaidi Roho Mtakatifu pia atakuongoza katika maombi yatakayosidia kuuondoa ule udhaifu ambao umekuja si katika mapenzi ya Mungu, yaani wa kishetani.

Jambo la pilini wakati wa kuweka msingi imara wa uchumba wenu na kufahamiana zaidi.
Hili jambo ni la muhimu  kuzingatia. Ni vema wachumba wakatafsiri na kuelewa vizuri maana ya uchumba. Wachumba wanapaswa kuwa na mipaka fulani katika uchumba wao na  kuwa makini kwa kujilinda na mazingira ya kila namna ambayo yanaweza yakapelekea wao kuanguka dhambini. Ni vema mkajua kwamba ninyi ni wachumba na si wanandoa. Na kama ni wachumba basi uchumba una mipaka yake na hamruhusiwi kufanya mambo ya wanandoa. Mipaka hii iwe kwa habari ya kutembeleana,kupeana zawadi, mawasiliano (ingawa mnapaswa kuwa makini na lugha mnazotumia pia) nk.  Lengo la kutafsiri misingi ya mahusiano yenu ni kujiwekea mipaka na mazingira yatakayowasaidia kuishi maisha ya nidhamu, ushuhuda na kumletea Mungu utukufu.

Sambamba na hili sehemu kubwa ya wachumba huwa wanakuwa hawafamiani vizuri. Japo wapo baadhi ambao walianza tangu shule za msingi/sekondari/chuo na sasa wamechumbiana hivyo kwa sehemu wanafahamiana vema. Kwa wale wasiofahamiana vema huu  ni wakati wa kumjua mwenzako vizuri kwa maana ya kabila lake, familia yake, umri wake, interest zake, matatizo aliyo nayo yeye binafsi au ya kifamilia, mitazamo yake juu ya mambo mbalimbali kama uchumba, ndoa, maisha, wokovu, neno la Mungu nk. Huu ni wakati wa kumjua mwenzako kwa njia ya maswali mbalimbali ya msingi yanayohusu vitu nilivyovitaja hapo juu. Lengo hapa ni kujua mapungufu/madhaifu(weakness) na mazuri(Strength) za mwenzako ili mjue namna ya kukabilana na mapungufu na namna ya kuendeleza yaliyo mazuri.

Ni vema pia kuulizana historia zenu za maisha ya nyuma. Kabla ya kuokoka umepitia katika mifumo gani ya maisha ambayo imechangia kukufanya uwe ulivyo. Kabla ya kumpata uliye mpata ulikuwa umefuatwa na wangapi na uliwakubalia au la, na kama uliwakubali kwa nini mliachana, na sasa wako wapi, je bado wanakufuatilia. Hii itawasaidia sana kujipanga vizuri kimaombi na katika mahusiano yenu na zaidi itawasaidia kuweza kuchukuliana na kuhifadhiana katika madhaifu ya kila mmoja.

Mungu anapowaunganisha anakuwa na kusudi maalum. Hivyo jua kwamba huyo mwenzi uliyepewa umepewa kwa ajili ya kusudi fulani la Mungu. Ni wachumba wachache sana ambao pindi wanapokutana kila mmoja anakuwa anajua walau kwa sehemu kwa nini aliumbwa. Sasa ni vema mkae chini mfikiri, nini Mungu anataka kukifanya duniani kupitia ninyi? Na zaidi angalieni kazi zenu au yale mnayoyasomea, Je mtawezaje kuliimarisha agano la Bwana kwa pamoja kama mke na mume?.

Hapa maana yetu mnatakiwa kujibu maswali yafuatayo? Je ni kwa nini mlizaliwa? Je kwa nini Mungu amekuunganisha na huyo uliye naye sasa? Na je kupitia elimu, bisahara zenu au kazi mlizonazo mtawezaje kuimarisha agano la Bwana?, Kwa kuzingatia vipawa na uwezo Mungu aliowapa, je ni wapi Mungu anataka kuwapeleka na kuwafikisha? Kama ndani yenu mna huduma fulani, je ni watu gani ambao Mungu atataka mshirikiane nao katika huduma hiyo?, je ipi ni nafasi yenu katika mwili wa Kristo na taifa kwa ujumla? Ni vema zaidi mwanaume akajua wito/ kusudi aliloitiwa ili pia amshirikishe na mwenzake.

Kufanikiwa kwa hili kunahitaji uwepo muda wa kutosha wa wachumba kukutana ili kupanga na kuweka mambo yao mbalimbali, na kama ni watu walioko mbali basi suala la mawasiliano kwa njia mbalimbali kama simu, barua pepe, na barua na hata zawadi ni la muhimu.

Jambo la tatu- ni wakati wa kulinda wazo la Mungu hadi litimie.
Siku zote uamuzi wowote unaoufanya una gharama. Naam uchumba pia una gharama nyingi Sana za kuzikabili kuliko unavyofikiri. Gharama hizo ni pamoja na muda, pesa, mawasiliano, maombi, uhuru nk. Kumpata mchumba au mwenzi ambaye ni wa kusudi la Mungu, usidhanie ndio umemaliza. Kama huo uchumba wenu ni wa mapenzi ya Mungu muwe na hakika mtakutana na vita kubwa sana katika kipindi hicho cha uchumba na lengo ni kuwatenganisha. Ni lazima mjifunze siku zote kuombeana kwa kumaanisha maana Shetani naye yupo kazini ili kuvuruga hayo mahusiano.

Kumbuka huyo mwenzi ni agano toka kwa Bwana hivyo unawajibika kumlinda, kumlinda ni pamoja na kuhakikisha wewe hausabibishi au haufanyiki chanzo cha ninyi wawili kuanguka dhambini, au ukamwacha na kumsababishia majeraha ya nafsini na hivyo kuharibu mahusiano yake na Mungu. Wapo watu waliofikia kuharibu mahusiano yao na Mungu kisa mchumba, saa ya ibada imefika mchumba anasema twende zetu out bwana, unataka kufanya maombi ya kufunga mchumba anasema kesho nitakutoa out, inagharimu sana muda wa kuwaza pia kwa ajili yake na familia yake au mahitaji mbalimbali aliyo nayo.

Zaidi pia uchumba unaweza kukunyima uhuru hata wa kuwa na maongezi na rafiki zako, maana kuna baadhi ya watu huwa hawataki kuona mchumba wake anaongea au kucheka na watu wengine, na pia kuna wengine ni wachumba lakini wamewekeana taratibu ngumu utafikiri wanandoa kabisa na ukweli zinawatesa ila kwa sababu hataki kumpoteza huyo mchumba wake inabidi avumilie.  Jambo tunalosisitiza hapa ni kwamba, uchumba una gharama nyingi angalia mahusiano yako na Mungu yasiharibikie hapa.

Jambo la nne- ni wakati wa kupanga malengo na mikakati yenu ya baadae.
Mithali 29:18a “Pasipo maono, watu huacha kujizuia’
Hili si jambo ambalo vijana wengi hulipa kipaumbele linavyostahili. Katika hili ni vema wachumba wafikirie mapema ni aina gani ya maisha ambayo wangependa kuwa nayo, na pia je ni aina gani ya ndoa wanataka kufunga, tatu je ni wapi wangependa kuja kuishi kwa maishayaoyote. Haya yatawasaidia wahusika kujipanga ndani na nje kukabiliana na yaliyo mbeleyao.Kamawanataka kufunga harusi kanisani basi maana yake wanahitaji kuwa na maandalizi mazuri kifedha, waweke katika muda kila wanalotaka kuelekea katika harusiyaoili iwasaidie kujiaadaa mapema. Malengo yoyote yale ambayo mtaweka basi hakikisheni yanatekelezeka, yanafikika, yanapimika na mnayapangia muda wa utekelezaji.

Mambo zaidi ya kuzingatia katika malengo yenu;
Katika hili ni vizuri wachumba waangalie nafasi yao kifedha imekaaje, na changamoto zinazowakabili wote kwa pamoja. Je hali yao kifedha inawaruhusu kuzikabili gharama za maandalizi ya ndoa kwa ujumla. Je hali ya kimaisha ya kijana wa kiume inamruhusu wakati wowote baada ya kuchumbia aweze kufunga harusi kama anataka. Je nafasi zao kielimu zikoje, je kama zinatofautiana ni kwa kiwango gani? Na je tofauti zao kiuchumi na kitaaluma zinaweza kuwa kikwazo kwao kuoana, au kwa wazazi wao nk. Na je baada ya kuwa wamegundua na kupima uwezo wao katika hayo mambo mawili, je wanaweza wakasaidianaje ili wafike mahali pazuri wote wawili.

Vijana wengi wa kiume huwa wanakosea sana hapa, wengi huwa wanasema sitaki kuchumbia/kuoa mpaka niwe nimesha jikamilisha kiuchumi, niwe angalau na maisha mazuri. Sisi hatushauri sana dhana hii, ukweli ni muhimu kwa kijana wa kiume akjikamilisha kwa yale mambo ya msingi. Lakini fahamu kwamba kuna wakati mwingine kuendelea kwako kiuchumi, au kuvuka kwako kimaisha ni rahisi zaidi pale unapokuwa na mchumba au ndoa yako. Tunasisitiza tena ni vema wachumba wakae chini na kufikiri ni kwa namna gani wataendelezana kiuchumi na kitaaluma. Angalizo, ni vema uwe na uhakika kweli huyo mtu ni wa mapenzi ya Mungu kwa maana ya kuwa ni wa kwako kweli, maana wapo wachumba ambao wamekuwa wakisaidiana mpaka kulipiana ada, kupeana mitaji, kununuliana nyumba, magari nk, halafu mwishowe mmoja anavunja maagano, maumivu yake ni makubwa sana.

Jambo la tano – ni wakati wa matengenezo na kuzijenga nafsi zenu
Wachumba wengi huwa wanafichana mambo mengi sana wanapokuwa wachumba na matokeo yake hawayashughulikii mapema na hivyo yanakuja kuwaletea shida kwenye ndoa. Huenda kabla hujakubaliwa wewe tayari mwenzako alikuwa amesha wakubali vijana au mabinti wengine kwamba ataolewa nao au kuwaoa. Pia  kama ni msichana huenda ameshawahi kubakwa, au kutokana na masumbufu ya kupata mtu sahihi na wakati mwingine kuachika mara kwa mara imefika mahali huyo msichana akasema sitaki kuja tena kuolewa. Zaidi  huenda  mmoja wenu huko nyuma ameshawahi kufanya uasherati au zinaa kabla hamjachumbiana. Au kuna mwingine amekuwa akisumbuliwa na tatizo la harufu, kufanya tendo la ndoa na mapepo nk.

Haya yote na mengine mengi yanayofanana na haya yana athari kubwa sana kiroho na kimwili kwenu kama wachumba na wanandoa watarajiwa kama hayatashughulikiwa vema katika kipindi hiki cha uchumba. Licha ya kuwa na athari mambo hayo yamepelekea nafsi za watu au wachumba wengi kujeruhika. Nafsi inapojeruhiwa inaharibu ndani ya mtu mfumo wa kufanya maamuzi, mfumo wa utiifu kwa Mungu wake, mfumo wa kunia na kuhisi pia. Sasa mifumo hii inapoharibika inapelekea watu kufanya maamuzi ambayo yapo nje ya mapenzi ya Mungu kabisa. Nawajua baadhi yao ambao wameacha na wokovu, na, wengine wamekata tamaa ya kuolewa, wapo walioamua kuolewa na mataifa ilimradi ameolewa nk.

Hivyo basi tumieni wakati huu kufanya matengenezo na kujengana nafsi zenu kwa maana ya kuombeana sana, pili kwa kuongeza ufahamu wenu katika neno  la Kristo hasa maandiko yanayolenga uponyaji katika nafsi zenu, tatu kufuta na kufisha mapatano/maagano yote ambayo mmoja wenu aliyafanya huko nyuma na watu wengine na pia kufuta picha za kubakwa na kujenga ufahamu wa mtu aliyeathirika kisaikolojia kutokana na mambo kama hayo kwa njia ya Damu ya Yesu. Hatua hizi zitawasaidia kurejesha mifumo iliyoharibika na kuziruhusu nafsi zenu zifanye kazi kama inavyotakiwa.

Jambo la sita – ni wakati wa kujua taratibu mbalimbali kuelekea kwenye ndoa
Tumeshasema, kila dhehebu au kabila wana taratibu zao kuhusu uchumba hadi ndoa. Hivyo ni vema wachumba, wakafuata taratibu ambazo zimewekwa na makanisa yao hasa zile ambazo zipo katika mapenzi ya Mungu. Lakini pia lazima tukubali kwamba kuna baadhi ya taratibu za makanisa, makabila na hata madhehebu ambazo nyingine zipo tu lakini hazitekelezeki na nyingine hazimpendezi Mungu.

Sasa ni vema wachumba wazijue hizo taratibu na wajue je wanaweza kuzitekeleza au la, na kama hawawezi wafikirie kabisa wanafanyeje. Mfano kuna baadhi ya makanisa ambayo hayaruhusu mtu wa kwao aoe au kuolewa na mtu wa nje ya dhehebu hilo. Sasa hii ina maana kama una mchumba wa aina hiyo jipange kujibu maswali ya wazee wa kanisa na Mchungaji vizuri. Na zaidi kuna baadhi ya makabila na familia hazitaki uoe au kuolewa na watu nje ya kabila lako, au aliyekuzidi umri kama wewe ni kijana wa kiume nk. Hivyo ni vema kuzijua hizo taratibu ili mjue mnajipangaje kukabiliana nazo. Ushauri wetu ni huu kama una uhakika huyo mtu ni wa kutoka kwa Mungu basi simamia la Bwana maana lipi jema, kumpendeza Mungu au wanadamu?. Kumbuka Mungu ndiye mwenye ratiba ya kila mmoja wetu.

Swala la  kukagua/kupima afya zenu kwa pamoja.
Kwa mazingira ya ulimwengu wa sasa suala la ukimwi limechukua sura mpya na kuleta mtafaruku ndani ya kanisa hasa kwa vijana wanochumbia kabla ya kupima afya zao. Siku hizi jambo hili limewafanya wachungaji kuomba sana kwa habari ya vijana ndani ya kanisa. Sasa kama mlikuwa hamjapima afya zenu mpaka mmechumbiana basi chukueni hatua mwende kupima. Ni vema wachumba wakapima mapema afya zao ili jambo hili lisije likawaletea shida baadaye, maana kwa sheria ya nchi yetu wachungaji hawaruhusiwi kufungisha ndoa kama mmoja wa wahusika ameathirika.

Upimaji wa afya zenu ni wa muhimu kwani, ndani ya makanisa kuna rekodi ya vijana wengi tu ambao wameshaathirika na huenda si kwa sababu ya zinaa, maana kwa mujibu wa watu wa afya njia za maambukizi ni nyingi. Kuna wengine wamezaliwa nao, kwa nia ya kuongezewa damu,kutumia vifaa kama nyembe, sindano nk. Hata hivyo swali la msingi inabaki kwamba je, liko tumaini kwa mtu aliyeathirika kuoa au kuolewa
 
Tukueleze hivi, hakuna jambo gumu lolote la kumshinda Bwana, hii ni pamoja na ukimwi, kama Mungu alimfufua Lazaro, alitenganisha bahari ya Shamu na watu wakapita, kama Yesu alitembea juu ya maji, basi naomba ujue kwamba Ukimwi hauwezi kuzuia kusudi la Mungu hapa duniani kwa wale awapendao na kwa sababu hiyo tunasema hata kama mtu ana ukimwi na Mungu bado ana kazi naye hapa duniani, hakika atamponya huo ukimwi na atampa mke au mme.

Faida na lengo la kupima ni hili, hata kama majibu yatatoka mmoja ameathirika isiwe mwanzo wa ninyi kuachana. Kama mna uhakika Mungu aliwaanganisha huu ndio wakati wa kurudi mbele za Mungu kwa maombi ya uponyaji na kujipanga zaidi juu ya hilo.

Jambo la saba – ni wakati wa kuongeza ufahamu wenu kuhusu nafasi yako kwenye ndoa.
Je umeshawahi kujiuliza ni kwa nini Mungu anakupa mke au mme? Yamkini zipo sababu nyingi lakini baadhi yake ni; Mungu anakupa mke kama msaidizi, mlinzi, na pia unapopata mke au mme unakuwa umejipatia kibali kwa Bwana na pia ni kwa sababu ya zinaa ndio maana unahitaji mwenzi. Hizi ni baadhi ya sababu zilizoko ndani ya Biblia. Hivyo basi tafuteni wanandoa mnaowaamini na zaidi waliokoka  muwaulize   kuhusu wajibu  wa kila mmoja kwa nafasi yake kwenye ndoa. Katika hili baadhi ya makanisa  huwa yana utaratibu wake wa nani atahusika na maelekezo ya aina hii kwa wachumba. Hivyo kama kanisa lako lina utaratibu huo, fuata huo utaratibu.

Katika ndoa kuna mambo mengi sana ambayo mtatakiwa kufanya, ni vema kufuata mwongozo na ushauri wa viongozi wenu au wachungaji wenu kuhusu nini mnatakiwa kufanya katika ndoa yenu. Angalizo hapa ni hili, uwe makini na vyanzo vya ushauri au mafunzo katika eneo hili ili lisije kuleta madhara baadae. Usitafute wala kufuata kila ushauri, bali sikiliza pia uongozi wa Mungu ndani yako.

Jambo la nane– Msifanye tendo la ndoa, maana jambo hili litaharibu mpango wa Mungu na kusudi lake kupitia ninyi.
Wakati wa uchumba, si wa kufanya mapenzi au kufanya michezo ya mapenzi. Tunarudia tena ili kuonyesha msisitizo kwamba chonde chonde jamani, uchumba sio ndoa, maana uchumba unaweza kuvunjika. Hairusiwi kabisa kwa wachumba kufanya mapenzi kwa maana ya tendo la ndoa kabla ya ndoa. Kitendo cha Mungu kukujulisha/kukupa huyo mwenzako kama mke/mume mtarajiwa haina maana mna haki ya kufanya mambo ya wanandoa. Mungu kukupa huyo mwenzako sasa ni taarifa kwamba  huyu ndugu ndiyo atakuwa mkeo au mmeo na anakupa taarifa sasa ili ujipange kufanya mambo ya msingi mnayotakiwa kuyafanya katika kipindi cha uchumba. Kipindi cha uchumba ndicho kipindi ambacho wachumba wengi sana wanavuruga kusudi la Mungu, na kuharibu maisha yao ya baadae na ndoa yao kwa ujumla.

Ndoa nyingi sasa hivi zina migogoro kwa sababu wakati wa uchumba walidiriki kufanya tendo la ndoa. Vijana wengi hawajajua kufanya tendo la ndoa kipindi cha uchumba lina madhara gani kwao na ndio maana wengine wanafanya. Biblia inasema katika Mithali 6:32 “Aziniye na mwanamke hana akili kabisa, afanya jambo litakalomwangamiza nafsi yake mwenyewe”. Hata kama ukifanya tendo la ndoa na mchumba wako ambaye mlibakiza siku moja kufunga harusi, bado umezini.

Ndani ya nafsi ya mtu kuna akili, hisia, nia na maamuzi. Biblia inaposema afanya jambo litakalomwangamiza nafsi yake ana maana hii, dhambi hii inapofanywa, ina haribu mfumo wa utiifu na uamnifu kwa Mungu wako, inapelekea kukosa usikivu wa rohoni kabisa, ina haribu mfumo wa kufikiri, kunia na kufanya maamuzi. Na kwa sababu hiyo si rahisi tena kusikia na kutii uongozi wa Roho Mtakatifu. Kwa watu ambao wamezoea kuwa na mahusiano mazuri  na Mungu watanielewa ninachosema hapa.

Zaidi kuna baadhi ya wachumba kweli hawafanyi tendo la ndoa bali wanafanya michezo ya mapenzi. Michezo ya mapenzi (Fore play) ni maalum kwa ajili ya wanandoa, na ni sehemu ya tendo la ndoa. Hivyo kufanya michezo ya mapenzi ni kufanya mapenzi kwa sababu ile ni sehemu ya mapenzi. Kuna vitu unavichochea,  unaamusha hamu ya mapenzi au unayachochea mapenzi. Biblia inasema katika Mhubiri 2:7 “Nawasihi, enyi binti za Yerusalemu, kwa paa na kwa ayala  wa porini, msiyachochee mapenzi, wala kuyaamsha, hata yatakapoona vema yenyewe.

Mungu pia anachukia michezo ya mapenzi soma Isaya 57:4-5 “Mnafanya dhihaka yenu juu ya nani, juu ya nani mmepanua vinywa vyenu, Na kutoa ndimi zenu? Je, ninyi si wana wa uasi, uzao wa uongo; ninyi mnaowasha tamaa zenu kati ya mialoni, chini ya kila mti wenye majani mabichi….. Wachumba wengi hawajui haya kwa sababu si makanisa yote yanayofundisha maswala ya mahusiano ya wachumba kimpana.

Mpaka hapa tunaamini umeshajua hasara za jambo hili  na utazijizuia kabisa kulifanya. Michezo ya mapenzi ni pamoja na kunyonyana ndimi, kushikana sehemu ambazo zinaamsha ashiki ya mapenzi kama sehemu za siri, matiti, kiuno nk, pamoja na kuangalia picha za ngono. Katika kipindi ambacho tumemtumikia Mungu kupitia vijana tumejifunza na kukutana na kesi mbalimbali za aina hii na kuona namna Shetani anavyovuruga mpango wa Mungu kwa vijana. Mwenye sikio na asikie neno ambalo Roho wa Bwana awaambia vijana ili kulida kusudi la ndoa.

Ni imani yetu kwamba mambo haya nane yameongeza ufahamu na hivyo kuwa maarifa ya kutosha kukusaidia kuenenda kwa mapenzi ya Mungu katika kipindi cha uchumba.

Bwana awabariki!

Somo limeandaliwa na:
Mwl. Patrick & Frola sanga
 0755 816800

Christina Shusho, Upendo Nkone kushiriki International Gospel Music Festival 2013.

Mwimbaji wa Nyimbo za Injili Tanzania Christina Shusho anatarajia kushiriki Tamasha la The International Gospel Music festival kwa Mwaka 2013, lililoandaliwa na Kanisa la All Nation Break Through lililoko lililoko Columbus, Ohio, USA chini ya Watumishi wa Mungu Pastor Donnis & Nnunu Nkone.

Waimbaji wengine watakaoshiriki ni pamoja na Upendo Nkone, Pastor Daniel Kiza na Wengine wengi watakaoendelea kutangazwa siku chache zijazo. Taarifa zaidi kuhusu Muda na Sehemu zitatolewa hivi karibuni.

Wednesday, April 24, 2013

Kanisa Katoliki latoa Waraka kuhusu Mchakato wa Katiba Mpya.

Kardinali Pengo
Kwa njia ileile iliyotumika Mwaka 2009 yaani Kanisa Katoliki kupendekeza waumini wake jinsi ya kushiriki uchaguzi wa mwaka uliokua unafuatia yaani 2010, sasa wakati tukiwa katikati ya mchakato wa Katiba mpya, Kanisa limetoa tena waraka unaoelekeza Wakatoliki njia inayofaa wafuate katika mchakato huo.

Waraka huo umetoka kwa njia ya kitabu kama mwaka ule 2009, na sasa hivi Waraka huu una jumla ya kurasa 65. Bei ya Kitabu hicho chenye Waraka ni shs. 3000/= kwa kitabu kimoja na kinapatikana kwenye maduka ya Kanisa Katoliki.

Chanzo: Jamii Forum

Rais Kikwete akutana na Maaskofu Ikulu.

Rais akiwa kwenye mazungumzo na viongozi wa dini ya kikristo ikulu jijini Dsm.
RAIS Dkt Jakaya Mrisho Kikwete katika picha ya pamoja na viongozi wa madhehebu mbalimbali ya dini ya Kikristo Ikulu jijini Dar es salaam leo (Jumanne 24 Aprili). Kulia ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Mahusiano) Mhe Steven Wassira.

Viongozi wa dini wamewataka waumini kote nchini kulinda amani na umoja uliopo ili nchi isije ikaingia kwenye mgawanyiko wa kidini na kuleta machafuko hapa Tanzania.

Wito huo umetolewa na viongozi wa dini leo (Jumanne 24 Aprili) Ikulu ya Dar-Es-Salaam mara baada ya kikao cha pamoja baina ya viongozi wa dini na Rais Jakaya Kikwete. Viongozi hao wa dini wamefika leo (Jumanne 24 Aprili)wakiongozwa na Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa, ambaye ni Mwenyekiti wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC).
Pichani Rais Kikwete akisalimiana na viongozi wa madhehebu ya Kikristo Ikulu jijini Dar es salaam jana.
Viongozi wengine wametokea Baraza la Kikristo Tanzania (CCT) Seventh Day Advertist (SDA) na Baraza la Pentekoste Tanzania (PCT). Mkutano huo umeanza kwa Askofu Ngalalekumtwa kusoma tamko lao la pamoja kwa Rais Kikwete ambalo ndilo limetoa muongozo wa mazungumzo hayo ya leo ambayo yamehusu Amani na Usalama wa Taifa na migogoro ya kidini ndani ya jamii.
Mkutano wa viongozi wa dini ya Kikristo Tanzania ni mojawapo ya jitihada za Rais Kikwete kutafuta muafaka na kutafuta utatuzi wa hali ya sintofahamu ambayo inanyemelea nchi yetu katika kipindi hiki.

“Nataka tuzungumze ni namna gani tunaweza kutoka kwenye hali hii na tunakwendaje mbele zaidi na kuhakikisha nchi yetu bado inakua ya amani na umoja kama ilivyozoeleka”
Rais amesema na kutoa nafasi kwa viongozi wa dini kutoa maoni yao.

Viongozi hao wa dini wamemueleza Rais Kikwete kuwa wanaunga mkono jitihada zake za kutafuta amani na kwa pamoja wamekubaliana uandaliwe mkutano wa pamoja baina ya viongozi wa dini zote ambapo masuala ya amani na umoja wa nchi utajadiliwa kwa kirefu.

Katika kikao cha leo pande zote zimekubaliana kuwa kuna changamoto zilizoko sasa zinahitaji kutatuliwa haraka iwezekanavyo ili kuepusha nchi kutumbukia katika mgogoro mkubwa zaidi, na pia kukubaliana kuwa pande zote, kwa maana ya serikali na taasisi za dini, zinawajibu mkubwa wa kuhakikisha amani inadumu.

Kabla ya kikao cha leo, Rais amewahi kukutana na viongozi wa dini ya kiislamu na kikristo mmoja mmoja ambapo alikua akitafuta maoni na ushauri wa pande zote kabla ya pande zote hazijakaa pamoja na kuwa na msimamo wa pamoja.

Kikao cha leo kimehitimisha jitihada hizo na kinachofuata ni mkutano mmoja ambapo Rais Kikwete atakutana na viongozi wa dini zote kwa pamoja hivi karibuni.

…”MWISHO”…
Imetolewa na:
Premi Kibanga,
Mwandishi wa Habari wa Rais, Msaidizi,
Ikulu-DSM
23 Aprili, 2013
 
CHANZO: Strictly Gospel & Gospel Kitaa

Tuesday, April 23, 2013

Historia ya Mwimbaji Sifa John.

Jina langu ni Sifa John. Nilizaliwa katika familia ya kiislamu na ni mtoto wa tano kuzaliwa ila kwa upande wa mama mimi ni mtoto wa pili, na wa kwanza alifariki ambaye alikua anaitwa Mwamvita. Nikiwa muislam nilikua naitwa Tiba Hamadi na baada ya kuokoka siku ambayo nilibatizwa ndipo nikapewa jina la Sifa, na baada ya kuolewa nikawa naitwa Sifa John(John ni Jina la Mume wangu). Baba yangu alitengana na mama yangu baada ya mama kurudi kwenye dini yake awali ya kikristo alikotokea kabla ya kuslim na kuolewa na baba. Baada ya mama kuondoka, baba yangu alioa mke mwengine na ambaye ndiye aliendelea kunilea baada ya kuachwa na mama.

Nilikaa kwa baba yangu mda mrefu bila kumjua mamaangu kwa sababu aliniacha nikiwa mdogo sana mana nilikua na miaka miwili tu, na baada ya kufikisha miaka kumi na nne nilikutana na mkutano wa injili hivyo nikaokoka kupitia mkutano huo. Ugomvi wangu na babaangu mzazi ulianzia hapo. Baba alikasirika sana na akanitenga kabisa na akakataa kuniendeleza kimasomo, na aliniambia hata akifa nisifike na mimi nikifa hatofika kwenye Mazishi. Lakini pamoja na yote baba yangu ananipenda sanaaaaana. na niliwahi kupata ajali ya mguu, mfupa ukakatika mara mbili na kupishana ikawa kwamba nikatwe mguu. Baba yangu alikua analia sanaaa kila akija hospitali.

Madaktari walikua wakimtoa nje mara kwa mara kwajili ya kulia, lakini alipambana kiume na kukwangua acount yake yote ili mimi nisikatwe mguu, mana aliambiwa kwamba ili nipone dawa inatakiwa iagizwe Ufaransa. Baba hakusita juu ya hilo kwani dawa iliagizwa hivyo nikatibiwa mpaka sasa nina miguu yote miwili. Hii yote ni kwaajili ya upendo wa baba yangu, hata mimi nampenda sanaaa baba yangu, lakini ninachomshukuru Mungu baba yangu amerejeza Moyo na sasa tunaishi nae kwa upendo sanaaa.

HISTORIA YAKE KIUIMBAJI
Nilianza huduma ya uimbaji Mwaka 1983 katika kwaya moja ya kanisa la Mchungaji Lukindo Kawe, na wakati huo nilikua nasoma Shule ya Msingi Kawe darasa la 4. Badae niliimba kwaya ya Yerusalem ya kanisa la Pentecoste Kawe-Mbezi kwa Mchungaji Kibingu Marandura ambae kwa sasa ni marehemu.Nipoolewa nilianza kuimba kwaya ya kanisa la EAGT Imani Choir ambayo ilikua chini ya kanisa la Mch. Ernesti Nyanda aliyekuwa Waziri wa Mawasiliano na Uchukuzi, na hapo nilikua Sololist niliyevuma sana na wimbo wa Kigeugeu. Hiyo ilikuwa ni katika mkoa wa Mwanza.

Badae nilichukuliwa na Kwaya ya Calvary EAGT Nyamanoro kwa Mch Kapera nikiwa Sololist na nilivuma sana kwa wimbo wa Malaika katika Kanisa la Efeso. Hapo sasa nilipata mtu mmoja anaitwa Gahutu akanidhamini nikatoa Album yangu ya kwanza ya Wateule Tutakwenda. Kwa sasa nimetoa album yangu ya pili ujulikanayo kama Usililie Moyoni Yupo Mungu.
Namshukuru sana Mungu ananipigania sana katika huduma hii mana nimekuwa nikisafiri huku na huko kwa ajili ya huduma na ananilinda sana. Pia kupitia huduma ya uimbaji nimefanikiwa kuanzisha huduma ya kusaidia watoto yatima na watoto waishio katika mazingira magumu. Pia ninao vijana ambao walikua wamekata tamaa tunaowapa mafunzo mbali mbali kama kushona, uigizaji, na computer.

Watoto hao nilionao wanapata misaada mbali mbali kama vile elimu mana kuna walimu wanawafundisha hapo kituoni mana walikua hawajawahi kusoma kwajili ya matatizo na shida walizonazo na kukosa msaada.
Pia namshukuru sana Mungu kwa sasa amenifanikisha nimefungua studio ya kushoot video pamoja na kupiga picha aina zote. Ofisi yetu iko Bunju B, hapahapa jirani na ofisi yangu ya Sifa Group Foundation, yote hii ili kupata pesa za kunisaidia katika uendeshaji wa kituo hiki. Soma Zaidi kuhusu Sifa Group Foundation Hapa.

Kwasasa vijana wangu wa upende wa maigizo wako location wanashoot movie iitwayo NO LOVE. Pia watoto hao wamepata mwalimu wa kuendeleza vipaji vyao. Kwa upande wa huduma yangu ya uimbaji tayari nimeanza kuandaa nyimbo mpya mbazo nitazitoa mwaka huu. Sitoacha kumtumikia Mungu kwa huduma hii mana alikonitoa ni mbali sanaaa.
Pia naomba mtu yeyote ambae ataguswa kuniwezesha katika huduma zangu hizi aniwezeshe mana nahitaji msaada sanaaa, hasa katika kituo cha watoto hao yatima na wale wa mazingira magumu.

Mungu akubariki sana wewe utakayewaza Kunisidia!

Mwalimu na Mwimbaji John Shabani atunukiwa Shahada.

Mwl. John Shabani akipokea Cheti chake
Mchungaji mtarajiwa John Shabani (kushoto) amekabidhiwa shahada yake na Askofu Kitonga (Kiongozi wa Makanisa ya Redeemed duniani), baada ya kuhitimu Mafunzo katika chuo cha kimataifa cha huduma (International School of Ministry - ISOM) chenye makao makuu New York Marekani.

Ilikuwa ni siku ya furaha kwa Mwalimu huyo wa muziki wa injili Afrika mashariki bwana John Shabani, baada ya kuhitimu mafunzo yake hayo kwenye chuo hicho cha kimataifa. John ambaye amekuwa na ndoto za kujiendeleza sana katika elimu mbalimbali, amekuwa miongoni mwa wanafunzi waliofanya vizuri katika chuo hicho.
Mchungaji huyo mtarajiwa anategemea kujiunga na chuo kimoja huko marekani ili kuendelea zaidi na masomo yake, pia amewahasa waimbaji wenzake wa injili kuwa na mpango wa kujiendeleza ki-elimu.

Mahafali hayo yamefanyika jijini Dar es salaam na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa ki-dini na serikali. Makao makuu ya chuo yaliwakilishwa na Dr. Lee kutoka Marekani.

CHANZO: Tanzania Daily Eye

Sunday, April 21, 2013

Edward Lowasa akabidhiwa Tuzo na Kanisa la Overcomers Power Centre.

WAZIRI  Mkuu  mstaafu  Edward  Lowassa amesema kuwa mbali ya  kuwa  yeye  si tajiri ila bado ataendelea  kufanya kazi  yake kwa  ukaribu  zaidi na jamii ikiwa ni pamoja na kushirikiana na  marafiki  zake  kusaidia na kuwataka  wale  wote  wenye kusema dhidi yake  kuendelea  kusema ila hatarudi  nyuma katika kutoa misaada kama njia ya  kutafuta baraka za Mungu.

Lowasa ambae  pia alikabidhiwa  tuzo ya  heshima kwa ajili ya  kuendeleza  kulipigania  Taifa  la Tanzania, huku  mwenyewe akichangia kiasi cha Tsh milioni 15  na mbunge  wa jimbo la Ludewa  Deo Filikunjombe akichangia  milioni 9  kati  ya  fedha  zote  zaidi ya Tsh milioni 75 zilizochangwa kwa ajili ya   kuendeleza ujenzi  wa kanisa la OPC mkoani Iringa kama njia ya  kuhamasisha amani katika Taifa ametaka  watanzania  kuwapuuza  wale  wote wanaoeneza siasa  za uchochezi .

“Nataka  kuwaomba  leo wachukieni  wachochezi na pia niwaelezeni  kuwa mimi  si tajiri ila nina utajiri  wa  watu na ushawishi na ninafanya  mambo haya ili kumbukumbu yangu  iweze  kuandikwa  Mbinguni  na nimekuwa  nikialika watu  wengi  na nimekuwa nikifika   wacha  wenye  kusema waseme  watasema ila usiku  watalala wenyewe ....sitaacha  kusaidia kwa kuogopa kusemwa”

Akizungumza katika hafla  hiyo  iliyoandaliwa na kituo  cha maombezi na uponyaji mkoani Iringa Overcomers Power  Center (OPC) na kufanyika katika  ukumbi  wa St Dominic mjini Iringa leo  Lowassa  alisema kuwa yeye  si tajiri kama ambavyo  watu  wanavyofikiri ila amekuwa akipewa  nguvu na rafiki  zake ambao  wamekuwa  wakimuunga mkono pindi anapoalikwa katika hafla  mbali mbali.

“Nataka  kwanza  kuwashukuru  ndugu zangu  wa mkoa  wa Iringa na napenda  kumshukuru  zaidi Askofu Dkt  Boaz Sollo kwa kunialika  mkoani Iringa …..ila napenda  kuwaeleza  kuwa  si kwamba nachangia michango mbali mbali katika jamii kama mimi ni tajiri  ila mimi ni mtumishi nisiye na faida na nayaweza yote  katika  yeye anitiaye nguvu Pia  nawashukuru  sana  wabunge  wenzangu ambao  wamepata  kushiriki name  leo katika  ziara  hiyo  akiwemo  mbunge machachari  bungeni Deo  Filikunjombe, Kagi Lugola  na dada yangu  Ritta Kabati  bila kumsahau mbunge Mendradi Kigola kwa kuungana nami leo naamini nao  wamepanda  mbegu  bora”.

Lowassa  alisema kuwa anatambua  bado ana mialiko migi  sana na lazima ataifanyia kazi mialiko yote kama ambavyo jamii imepata  kumwalika na kuwa hata  hatua ya  mkoa  wa Iringa kumpa  tuzo hainamanishi  kuwa ni mwisho wa  yeye  kualikwa.

Hata  hivyo  Lowassa  alisema  kuwa  kwa upande  wake anapongeza  jitihada za Askofu Dkt  Sollo kwa  kuwa na mipango na mitazamo ya  kulisaidia  Taifa  kwa kuanzisha  ujenzi  wa kanisa kwa ajili ya  kudumisha amani na  kwenda mbali  zaidi kwa  kuanzisha  kituo cha  radio  Overcomers  Fm   chombo ambacho  kitatumika  kudumisha amani ya mkoa wa Iringa na Taifa  pia

Kuhusu amani ya Taifa  la Tanzania  Lowassa alisema  kuwa alikuwa ni miongoni mwa watu  walioalikwa Kenya  katika sherehe ya  kuapishwa Rais mpya wa Kenya  Uhuru Kenyatta ila  sehemu kubwa ya  wote  waliotoa  salam zao  walitumia muda mwingi kupongeza  vyombo vya habari kwa kulinda amani na hivyo  kuvitaka  vyombo  vya habari za Tanzania na wanahabari  kuendelea  kuandika habari bila kuhatarisha amani ya Taifa 

“Tusiruhusi amani ya nchi  yetu  iyumbishwe na mtu  awaye  yeyote  na kila mtanzania anapaswa  kulinda amani  hii  kwa nguvu  zote ….Nawaombeni  wanahabari  tunzeni amani  yetu…wapuuzeni  wale  wote  wanaoch0chea machafuko katika Taifa  hili ….tuachane na  udini  wala ukabila katika  taifa  letu"
 
Katika  hatua  nyingine  Lowassa  aliwapongeza  wabunge wa CCM ambao  wameendelea  kupigania wanyonge  bungeni akiwemo  Deo Filikunjombe mbunge wa Ludewa na mbunge wa jimbo la Mwibara Kagi Lugola  kuwa ni miongoni mwa wabunge ambao  amekuwa akiwapenda kutokana na kusema ukweli  bungeni.

Kwa upande  wake mbunge  Filikunjombe alisema kuwa mbali ya kutoa ahadi ya  kuchangia  kiasi cha Tsh milioni 9 ila bado atamwalika  Lowassa  jimboni kwake  Ludewa na kuwa kanisa  hilo la OPC halijakosea  kumpa tuzo ambayo ni ramani  ya  Tanzania kutokana na Lowassa kuwa ni mtu  wa  watu mpendwa na  watu na kuwa tuzo  hiyo  ina maana kubwa na hawajakupa ramani ya jimboni kwako Monduli.

Filikunjombe  alimtaka  Lowassa  kuendelea  kuchapa kazi na  kuwa hajakosea  kuwaalika  wao kwani bungeni  kuna  wabunge  zaidi ya  300 ila amewachagua wao  pekee, hivyo ni jambo la kumshukuru  na  kumfananisha Lowassa  na mti  unaopigwa mawe  kuwa ni mti wenye matunda.

“Nakuomba  Lowassa simama Imara  sisi  wana Iringa  tupo nyuma yako na niseme  tuna kazi kubwa ya kuifanya katika Taifa  hili kubwa ni  kumwomba Mungu na makanisa na dini  zote  kuungana katika maombi  zaidi kwani  vita  ni kubwa mbele “

Kwa  upande  Askofu  Dkt  Sollo  mbali ya  kumpongeza Lowassa bado  alisema kuwa  wao kama kanisa wataendelea  kumwombea  afya njema na kuona kuwa mambo yake yanafanikiwa na ndio maana ya kumpa  tuzo  hiyo  ya heshima.

Sollo alisema kuwa mchango  wa TSh milioni 15  ulioahidiwa na Lowassa na ule  wa milioni 9  ulioahidiwa na mbunge wa jimbo la Ludewa Deo  Filikunjombe ni mchango ambao  wao wanaupongeza na kuwapongeza  wabunge  wengine akiwemo Ritta Kabati aliyeahidi Tsh milioni 2 ,Benki ya  wananchi Mufindi milioni 2 , mwenyekiti  wa CCM mkoa  wa Iringa Jesca Msambatavangu milioni 2  mfanyabiashara Salim Abri milioni  1 na wengine  wengi ambao  wamepelekea  kupata  zaidi ya Tsh milioni zaidi ya 75  pesa taslim na ahadi.
 
Chanzo: Francis Godwin

Thursday, April 18, 2013

Historia ya Mwimbaji Ephraim Sekeleti.

Ephraim Sekeleti Mutalange ni muimbaji maarufu wa nyimbo za Injili nchini Zambia, alizaliwa Mwaka 1983 katika mji wa Kalulushi nchini Zambia. Alimaliza elimu yake ya sekondari katika shule ya Kalulushi mwaka 2001.Ephraim ni mtoto wa pili toka mwisho kati ya watoto sita, aliingia kwenye muziki wa injili tangu akiwa kinda huku alifundishwa kupiga kinanda na mmishonari alipokuwa bado mdogo. Mama yake anasema  “ Ephraim alikuwa ni mtoto aliyekuwa wa kelele nyingi”.

Yeye pamoja na dada zake waliimba kanisani wakitumia kinanda na huko alipata uzoefu katika uimbaji na upigaji wa kinanda. Baadaye alijiendeleza katika uimbaji kwenye kikundi kilichojulikana kwa jina la  “Virtue for Christ” na aliimba katika kikundi hicho kwa muda wa miaka miwili.
 
Mwaka 2002 akiwa na kiu ya kurekodi album yake, Aliamua kujitoa muhanga kwenda Afrika ya Kusini kwa kutumia kiasi kidogo tu cha pesa alichokuwa nacho, nia ilikua ni kurekodi album yake ya kwanza. Pamoja na jitihada hizo, baada ya kufika nchini Afrika ya Kusini alijikuta anaweza kurekodi nyimbo mbili tu kati ya album nzima. 

Hivyo akaamua kujiingiza katika Theater ya Pretoria na ndipo akapata fursa ya kuimba mbele ya Rais wa Afrika ya Kusini. Nafasi nyingi ziliendelea kujitokeza zilizomsababishia kutaka kuacha kuendelea na muziki wa injili ili aimbe miziki ya kidunia, lakini akawa muaminifu kuendelea na uimbaji wa injili. Mlango ulifunguka kumruhusu kurekodi album ya kwanza iitwayo Temba Baby“(Mtoto wa Miujiza)”.

Baada ya kurekodi, na kuuza nakala za kutosha za album hiyo ya Temba boy, kwa mafanikio ya hiyo kazi Ephraim aliamua kurudi nyumbani kuwekeza ile fedha. aliona awekeze zaidi kwenye ya album yake ya pili iliyopata mafanikio makubwa iliyoitwa Limo Ndanaka. Hi album imefanya vizuri kwenye chati mbalibali za muziki wa injili. Ephraim akiwa nje ya Zambia ameimba katika nchi mbali mbali zikiwemo Namibia, Afrika ya Kusini, Tanzania, Zimbawe na Australia.

Alisema anafurahi akiona watu wasiokuwa na tumaina la Kristo wakianza kuwa na matumain, Licha ya kufanya muziki wake nchini Zambia amewahi kuja nchini Tanzania na kurekodi album yake nzima kwa Lugha ya Kiswahili. Moja kati ya Nyimbo zake zinazotamba hapa nchini ni pamoja na;
                                             1. Uniongoze                                 
                                             2. Baraka Zako
                                             3. Huu Mwaka 
 
Ephraim hajui Kiswahili fasaha na nyimbo zake hizo alifundishwa kuziimba kwa lugha ya Kiswahili na Mchungaji ambaye pia ni muimbaji wa nyimbo za Injili kutoka Tanzania Ency Mwalukasa. Ephraim amesema ataendelea kuhubiri kwa njia ya uimbaji kwa sababu imempa changamoto zilizomuinua. Licha ya uimbaji Ephraim amefunga ndoa na Faith Chelishe na wamejaliwa kupata mtoto mmoja wa kike.Imeandaliwa Na; Victor Nivox

Baraza la Makanisa Zimbabwe launda Tume ya Wasimamizi wa Uchaguzi Mkuu.

Wananchi wa Zimbabwe wameanza maandalizi kwa ajili ya uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwaka huu, baada ya kupitisha Katiba kwa kura ya maoni na hivyo kufanya mabadiliko makubwa yanayopania pamoja na mambo mengine, kupunguza madaraka makubwa aliyokuwa nayo Rais, kusimamia haki msingi za binadamu pamoja na kudumisha misingi ya haki na amani.

Kwa kuzingatia historia ya Zimbabwe kwa miaka ya hivi karibuni, iliyopelekea machafuko ya kisiasa na hatimaye kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa, Baraza la Makanisa Zimbabwe limeunda Tume ya Kiekumene ya Wasimamizi wa Uchaguzi mkuu, yenye dhamana ya kukoleza moyo wa majadiliano, ili kulinda na kudumisha misingi ya haki, amani na upatanisho wa kitaifa.

Tume hii inatekeleza wajibu wake kabla, wakati na baada ya uchaguzi mkuu na inasimamiwa na Tenda Maregere. Haya ni malengo ambayo Baraza la Makanisa Zimbabwe lilijiwekea kwa kitambo kidogo, kwa sasa yanafanyiwa utekelezaji wake, kadiri ya taarifa iliyotolewa na Shirika la Habari la Misna.

Makanisa nchini Zimbabwe yamekuwa yakichangia kwa kiasi kikubwa katika kulinda na kudumisha misingi ya haki, amani, upendo na umoja wa kitaifa, bila kusahau upatanisho pale ambapo kinzani na migogoro ya kisiasa ilipojitokeza; mambo ambayo yamekuwa ni sehemu ya historia ya wananchi wa Zimbabwe tangu wakati wa harakati za kupigania uhuru kutoka katika utawala wa Mwingereza.

Tume ya Mabaraza ya Makanisa pamoja na mambo mengine inapania kukuza moyo wa majadiliano miongoni mwa wananchi wa Zimbabwe, kudhibiti mchakato mzima wa upigaji kura ili haki, uhuru na ukweli viweze kutawala na hatimaye, Zimbabwe iweze kuwapata viongozi watakaochaguliwa kwa kura halali wakitambua dhamana na wajibu wao katika kuiendeleza nchi yao. Tume itakuwa na wajibu wa kusema haraka iwezekanavyo pale ambapo kutakuwepo na ukiukwaji wa haki msingi za binadamu.

Vyama vikuu vya upinzani vinavyotoana jasho kwa sasa ni ZANU-PF kinachoongozwa na Rais Robert Mugabe pamoja na Chama cha Democratic Movement for Change kinachoongozwa na Waziri mkuu wa Zimbabwe Bwana Morgan Tsvangirai; wapinzani wakuu waliopelekea machafuko ya kisiasa nchini Zimbabwe kunako mwaka 2008.

Saturday, April 13, 2013

Namna ya Kuongeza Imani unapokuwa kwenye Jaribu.

2 
Mpenzi msomaji Shalom,

Biblia katika kitabu cha Mathayo 17:18 inasema‘..Ni kwa sababu ya upungufu wa imani yenu. Kwa maana amini nawaambia, Mkiwa na imani kiasi cha punje ya haradali mtauambia mlima huu, Ondoka hapa uende kule; nao utaondoka; wala halitakuwako neno lisilowezekana kwenu. Hii ni habari ya yule kijana aliyekuwa na pepo bubu na kiziwi, mzazi wake akamleta kwa wanafunzi wa Yesu wamwombee. Biblia inatueleza kwamba wanafunzi walijaribu kumtoa yule pepo wasiweze, wakati huo Yesu alikuwa amepanda Mlimani kwenda kuomba.
 
Yesu aliporudi alielezwa kilichotokea, akawakemea wanafunzi wake na kisha akamuombea yule kijana akapona. Baadaye wanafunzi wa Yesu wakamuuliza, kwa nini sisi hatukuweza kumtoa yule pepo. Ndipo Yesu akawajibu akasema ‘Ni kwa sababu ya upungufu wa imani yenu… Neno upungufu lina ya isiyo – tosheleza, yaani imani yao ilikuwa ina upungufu na kwa hiyo wasingeweza kumtoa yule pepo. Jambo ninalotaka tuliangalie ni kwamba kwa kuwa tatizo lilikuwa ni upungufu wa imani yao, ina maana walitakiwa kuongeza imani yao wakati wanaendelea kukemea. Sasa swali muhimu ni je wangeongezaje imani yao wakati wako kwenye jaribu/vitani?

Naam licha ya swali hili kuna maswali mengine ambayo ni muhimu kuyatafakari ili tuweze kuwa na ufahamu mzuri wa imani. Je upungufu huu wa imani kwa wanafunzi walikuwa nao kabla hawajaanza kukemea yule pepo au ulikuja wakati wanaendelea kuomba. Naam Yesu anatuonyesha kwamba kosa la hawa wandugu wenzetu lilikuwa upungufu wa imani yao?

Ni kwa namna gani walikuwa na upungufu wa imani?
Biblia katika Waebrania 11:1 inaeleza kwamba ‘imani ni kuwa na uhakika wa mambo yatarajiwayo ni bayana ya mambo yasiyoonekana’. Kwa hiyo endapo Yesu alisema ni kwa sababu ya upungufu wa imani yao ina maana ndani yao walipungukiwa uhakika wa kile walichokitarajia, ambacho ni kufunguliwa/kuponywa kwa kijana mwenye pepo. Naam upungufu wao wa imani ulitokana na  mashaka juu ya uhakika wa yule kijana kufunguliwa.

Nini kilipelekea wao kuingiza hofu/mashaka?
  • Kukosekana kwa dalili za kijana kufunguliwa – Ni imani yangu kwamba wanafunzi walipoanza kukemea walikuwa na uhakika kwamba Yule kijana atafunguliwa. Naam kadri walivyoendelea kuomba na kuona kwamba hakuna mabadiliko ya aina yoyote kwa mgonjwa yule ndipo hofu/mashaka yakawaingia mioyoni mwao. 
  • Maneno ya kusikia – Ikumbukwe kwamba chanzo cha imani yoyote ni kusikia (Warumi 10:17)?  Kumbuka wakati wanendelea kuomba kulikuwa kuna kundi kubwa la watu ambao walikuwa wanamsubiri Yesu pamoja nao. Hivyo huenda wakati wanafunzi wanaaendelea kuomba walisikia watu wakisema, wanafunzi wa Yohana wenyewe walishindwa kumuombea, wao wataweza, wamejaribu watumishi wa kila aina wameshindwa, huyu hawezekani anasubiri kifo, naam haya yote yakapunguza uhakika ndani yao kwamba kwa jina la Yesu yule kijana anaweza kupona.
  • Maneno yao wenyewe – Biblia haituelezi namna/approach waliyoitumia kuomba/kukemea. Huenda walianza kuomba mmoja mmoja/ au waliomba wachache na mwishowe ndipo wakaomba kama kundi. Kwenye kundi lolote kuna mengi, huenda walipokemea kwa muda kadhaa na bila kijana kuonyesha dalili za kupona baadhi ya wanafunzi wakaingiwa na hofu na wakawaambukiza na wengine na hivyo kushindwa kumtoa pepo. Hebu jaribu kufikiri mtu kama Yuda Iskariote alikuwa anafanya nini wakati wenzake wanakemea?

Nini cha kufanya?
Hofu/mashaka ni silaha kubwa sana ambayo Shetani huitumia kuwafanya watu washindwe kupata majibu ya maombi/miujiza yao kutoka kwa Mungu. Shetani anafahamu kwamba imeandikwa ‘Mwenye haki wangu ataishi kwa imani, naye akisstasita roho yangu haina furaha naye’ (Wabrania 10:38). Hivyo ili kuharibu/kuondoa imani ya mtu kwa Mungu, silaha anayotumia ni kuingiza mashaka moyoni mwake dhidi ya ahadi za Mungu/neno la Mungu kwenye maisha yake. Yesu aliwaambia hivi wanafunzi wake ‘… amini nawaambia yeyote atakayeuambia mlima huu ng’oka ukatupwe baharini, wala asione shaka moyoni mwake, ila aamini kwamba hayo asemayo yametukia, yatakuwa yake’ (Marko 11:22).  

Mpenzi msomaji kamwe usimruhusu Shetani kwa kutumia silaha hii ya mashaka azuie baraka zako na wale wanaokuhusu maishani mwako. Haijalishi jaribu limesimama mbele yako kwa kiwango gani usiondoe imani yako juu ya kile ambacho Yesu amekisema kwenye neno lake juu yako. Naam Mungu wetu si mtu hata aseme uongo, ahadi zake ni amina na kweli.   Naam katikati ya jaribu/changamoto wewe ongeza imani yako kwa kupambana na roho ya mashaka/hofu, naam tumia Biblia ili ikuongoze kukupa mistari ambayo itakuongezea uhakika wa kufanikiwa katika lile ulifanyalo.

Zaidi kuwa makini na maneno ya kusikia kwa habari ya imani yako. Wanafunzi wa Yesu walipaswa kutokujali maneno ya kusikia kutoka kwa watu, au kwa wenzao walioingia mashaka, naam walipswa kudumu kuamini kwamba kijana atapona naam ingekuwa hivyo. Je si unakumbuka habari za Petro alivyoambiwa na Yesu atembee juu ya maji. Awali alianza vema na akatembea hatua kadhaa juu ya maji.    Biblia inasema dhoruba ilipompiga akaona shaka na kuanza kuzama. Kwa nini alizama? si kwa sababu Yesu hakuwepo, bali ni kwa sababu aliona shaka.

Naam kitu kilichopungua kwenye imani ya wanafunzi, ni uhakika kwamba yule kijana atapona. Na kilichopelekea upungufu wao wa imani, si   kutokumwamini/kumjua Yesu, bali ni kuruhusu hofu ichukue nafasi ya imani/uhakika waliokuwa nao kwamba yule mgonjwa atapona. Naam kwa mara nyingine tena ‘usirihusu hofu iharibu muujiza/future yako’.

Neema ya Bwana wetu Yesu Kristo iwe nawe daima.

Mwl. Patrick Samson Sanga
+255 755 816 800

Friday, April 12, 2013

Mwimbaji wa Bongo Flavour Kenya Aokoka.

http://themonsterradio.com/wp-content/uploads/2012/10/size-81-440x248.jpgMwimbaji wa Muziki wa kizazi kipya Nchini Kenya Linet Munyali a.k.a Size 8, ametangaza rasmi ya kuwa Ameokoka na hivyo kuachana na Muziki wa Kizazi kipya.
 
Akiongea na Mtangazaji wa Clouds Fm Millard Ayo kupitia kipindi cha Amplifier cha leo April 12, Size 8 amesema, "Nimeamua kuokoka kwasababu Maisha yangu yalikuwa hayana Amani. Mara nyingi nilikuwa Mtu wa Huzuni na kuna kipindi nilikuwa nikitoka kufanya Show Usiku najikuta nalia mwenyewe".

"Pamoja na kwamba pesa ninayo lakini maisha yangu yalitawaliwa na Huzuni" aliongeza Size 8. Akitoa sababu ya yeye kutokuwa na Amani, Size 8 amesema kuwa, hali hiyo ilikuwa ikimtokea tu, na yeye pia hajui sababu ilikuwa ni nini.

Huyu atakuwa si Mwimbaji wa kwanza wa Muziki wa kizazi kipya Nchini Kenya kutangaza kuokoka. Mwimbaji mwingine aliyewahi kuokoka ni DNA aliyetamba sana na Wimbo wa Banjuka. Kwa Tanzania Mwimbaji Stara Thomas pia aliwahi kutangaza kuokoka lakini akaamua kurudi nyuma tena na kuimba Bongo Flavour tena.

Swali la Msingi la kujiuliza, ni; Je! Nini kinafanya Waimbaji hawa kurudi nyuma na kuimba tena Bongo Flavour? Ni jukumu la Kanisa sasa kuhakikisha kuwa watu kama hawa wanalelewa vizuri Kiroho ili waweze kudumu katika Wokovu.

Papa Francis kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu, Kanisa la Mt. Paulo Jumapili hii.

Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili, tarehe 14 Aprili 2013 kuanzia saa 11:30 jioni, anatarajiwa kutembelea Kanisa kuu la Mtakatifu Paulo, nje ya Kuta za Roma na baadaye, kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu. Katika Maadhimisho ya Ibada hii, Baba Mtakatifu atasaidiana na Kardinali James Michael Harvey, Kardinali Codero Lanza di Montezemolo, Kardinali Francesco Monterisi pamoja na Abate Edmund Power, OSB.

Itakumbukwa kwamba, Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili iliyopita majira ya jioni aliadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Yohane wa Laterano, Makao Makuu ya Jimbo kuu la Roma na kuanza utume wake rasmi kama Askofu wa Jimbo la Roma. Ibada hii ilihudhuriwa na umati mkubwa wa watu waliokuwa wamefurika ndani na nje.

Kama inavyoonekana kuwa ni sehemu ya utaratibu wake, Baba Mtakatifu Francisko huanza kwa kusalimiana na waamini na watu wenye mapenzi mema, ambao wamekuwa wakifurika katika matukio kama hawa tangu alipochaguliwa kuliongoza Kanisa. Huu ni upepo mpya wa imani na matumaini ndani ya Kanisa.

Thursday, April 11, 2013

Spacio: Mwimbaji wa Nyimbo za Injili aliyeishi na Jini Mahaba kwa Miaka 17.

Kwa jina naitwa Spacio Abubakary Ngalla, nimezaliwa na kukulia Dar es salaam, Sinza. Na ni mtoto wa 3 katika familia ya kiislamu.

Kiukweli mimi nilikuwa mmoja wa watu ambao hawakutaka kusikia Jina la YESU na nilikuwa siamini miujiza yeyote na kuona ni mazingaombo tu wachungaji wanafanya kuwateka watu akili. Ila hadi siku ambayo mungu aliponionesha njia ya uzima na kuniponya tatizo lililonisumbua mda mrefu, ndipo nikaamini uwepo wa UKRISTO

NILIVYOKUTANA NA JINI MAHABA
Nakumbuka ilikuwa mwaka 1996, nikiwa na miaka 7, Mimi na marafiki zangu tulikuwa na tabia ya kwenda kuogelea coco beach siku za weekend, siku moja baada ya kumaliza kazi zangu za nyumbani majira ya saa 6 hivi nikaenda kuwapitia marafiki zangu (4) ili twende beach kuogelea ikifika jioni turudi nyumbani. Tulipofika beach watu walikuwa ni wengi sana kila mmoja alikuwa yupo busy na yake, sisi tulijigawa wengine walienda kuogelea sehemu nyingine, mimi na mwenzangu Ali tulibaki upande wa mwanzoni kwa kuwa hatukuwa tunajua kuogelea vizuri.

Majira ya saa 10, hivi nikiwa na Ali, nilisikia harufu nzuri kweli ikiwa inavuma kuja kwetu, ambayo siku wahi kuisikia kabla, ni nzuri kwa kweli, nikamuuliza Ali “unaisikia harufu hii?” yeye akajibu ndio ninaisikia ila sijui inatoka wapi!

Baada ya dakika kadhaa nilisikia sauti ya kike ikinisalimia “hujambo?” nikashtuka, kugeuka nyuma nikakutana na msichana sijui nimuelezeeje, ni mweupe kiasi, ana nywele ndefu, sura yake ipo serious na ukiiangalia tena ni kama anatabasamu, macho yake ni ang’avu, ni mzuri kiufupi akiwa amevaa nguo za kawaida tu ila kichwani amejitanda baibui. Aliniambia jina anaitwa MAIMUNA!

Mwili uninisisimka huku kidogo nikiwa na natetemeka japo sikutaka kumuonesha kwa kuwa hilo jina halikuwa geni kwangu, cha ajabu kadri alivyokuwa anaongea na mimi uoga ulizidi kunipungua hadi nikawa najiskia kawada na kucheka pamoja. Aliomba tuogelee wote nikamwambia, mimi siwezi kuogolea vizuri, akaniambia “Usiwe na wasi wasi nitakufundisha usijali” basi akaanza kunishika mikono na kuanza kunivuta ili niweze kujifunza kupiga mbizi taratibu. Siku hiyo ilikuwa ni tofauti sana kwani tulifurahi sana.

Saa 12 na nusu jioni ilipofika tukaanza kujiandaa kwa safari, siku hiyo tulichelewa kweli kuondoka! Ghafla Maimuna nikawa simuoni, nikaita sana “Maimunaaaaa uko wapi sisi tunataka kuondokaaaaa!” Kimyaa! Basi  sisi tukaanza kuondoka pale beach, kuna sehemu huwa ina miti mingi sana na ni shortcut kwenda kituoni, kwa mchana ni salama lakini kama ni giza giza si pazuri huwa kunakuwa na wahuni. Sisi tukiwa tunakaribia hiyo njia roho ilisita kupita pale, kumbe nyuma kulikua na wahuni wakitufatilia. Na sisi tupo watato tu, wao walikuwa watatu.

Heee mara tukashangaa kundi la watu zaidi ya 15 nao wakawa wanapita hiyo hiyo njia, basi sisi tukaongozana nao hadi kupita ile njia salama, kushtuka tunajiona tupo wa tano tu mbele tunakajiuliza “wale watu wameenda wapi?” Wahuni kumbe walikimbia katikati! sasa hatukujua ni kwa kwa sababu gani. Ila mimi nikahisi kundi la watu wale hawakuwa watu bali ni majini ndo waliotusindikiza, nikawaambia wenzangu “jamani tukimbie wale ni majini” kwa sauti kubwa ya uoga”.


URAFIKI NA JINI MAIMUNA
Tukafika nyumbani kila mmoja hoi, mimi bado nilikuwa na mawazo ya yule msichana niliyekutana nae baharini. Usiku nikiwa ndotoni nilimuota akija kunitembelea nyumbani na kufurahi pamoja.

Hali ile iliendelea hadi nafika form 1, ambapo nilikuwa nasoma Azania Sec School, haipiti siku moja lazima niote tuko pamoja tunafurahi pamoja hadi nikazoea,

Mwaka 2004, Maimuna alijitokeza tena kwa mara ya pili nikiwa niko chumbani, niliogopa sana nilipiga kelele mama akaja Maimuna akaondoka. Mama alishushwa sana na hali hiyo akaniuliza tatizo ni nini lakini nikamwambia nilikuwa naota tu, niliogopa kusema kwa kuwa Maimuna aliniambia nisiseme chochote kuhusu yeye la sisivyo nitakiona cha moto.

Baada ya muda nikazoea, akija tunaongea tu vizuri na kazi zingine alikuwa ananisaidia kama kutengeneza computer za baba, alikuwa ananisaidia kama tatizo ni kubwa sana namwita kimoyo moyo anakuja ktk mwili wangu kisha naanza kutengeneza computer, watu wengi walinishangaa sana uwezo niliokuwa nao lakini kumbe walikuwa hawajui JINI ndie alikuwa mara nyingi ananifundisha usiku.

Alinipa hela nyingi tu kiasi kwamba nilikuwa naenda shule nikiwa elfu 50, laki, ILA ole wangu nitumie na mwanamke au nimnunulie mtu sigara, pombe, basi hela zote zinapotea na nitahangaika hata shilingi 100 sipati zaidi ya kupewa hela ya shule, na nitahangaika hadi basi.

KAMA kawaida ukisha fikia umri fulani lazima uanze utundu wa kufatilia wasichana, kuwapa hela au kuwanunulia zawadi hasa katika siku kuu vile au valentine day, mimi iliponza sana hiyo tabia, kwani niliteseka sana.Kwani maimuna alikuwa hapendi

Kitu kilichonifanya nitafute wasichana wengine ni kwamba Maimuna hakuwa anakuja kila wakati, ni mara moja tu kwa siku tena hasa usiku. Na pia ukiangalia hata nikija kukua yeye anabaki jini na mimi binadamu kwa hiyo si rahisi kuja kuishi pamoja.

ILA chochote kilichokuwa kibaya kwangu kilichotegeshwa kichawi hakikuweza kunipata na hata usiku wachawi hawakuweza kunifata fata, japo mwanzoni nilihangaika sana na wachawi kwani walikuwa wanatusumbua sana nyumbani, waganga walidai nyumba haikuwa na zindiko!

Kiukweli alinifundisha vitu vingi pamoja na uchoraji, utayarishaji muziki, computer ambavyo hadi sasa vinanisaidia ktk maisha yangu, baada ya kutoka darasani yeye hunifuata usiku na kunielekeza zaidi. MIAKA YOTE HIYO TULIISHI KAMA WACHUMBA.Mengine siwezi kuyataja lakini mtakuwa mshaelewa nini ninamaanisha.


UGOMVI NA JINI KUANZA
Mwaka 2009, nina miaka 20 nikiwa nafanya kazi Cellulant Tanzania, kuna dada mmoja alikosea namba na kupiga kwangu, alijitambulisha kwa jina anaiwa UPENDO, mara ndio ukawa mwanzo wa urafiki wetu ambae hadi sasa tunaishi pamoja tukijipanga kwa ajili ya kufunga ndoa. Nilitokea kumpenda sana dada huyo japo hatukuwa tumeonana, na hata yeye pia alitokea kupenda kuongea na mimi mda wote. Maimuna alikuwa hapendi tabia ya mimi kuongea na huyo dada na mara nyingi alikuwa ananionya sana, ila mimi ilikuwa vigumu mno kukubali kwani nilikuwa nimshapenda tayari.

Siku moja nikasema hataa lazima nionane na huyu dada, hadi lini tutaishia kuongea kwa simu tu. Kwa mara ya kwanza kukutana na dada huyo, usiku wake sikulala! Nilipatwa na homa hadi asubuhi yake sikuweza kwenda kazini ikabidi nipumzike. Mara mwili unachoma, mara kifua kinanibana, mara kichwa kinaniuma, kikitulia nyama za mwili zinatikisika kama mtu anani vibrate vile.Niliteseka sana wiki nzima nilkuwa mgonjwa. Maimuna akaniambia hiyo ni bakora moja nimekupa, nataka uachane na UPENDO.

Baada ya kuseka sana kwa hali hiyo kwani mara kwa mara ilikuwa inanitokea, nikaanza kwenda kwa waganga kutafuta tiba ya kumuondoa jini huyo katika mwili wangu,kwani alikuwa kero kwangu, zaidi ya waganga 15 nilikwenda lakini bila mafanikio.


                                                    KUOKOKA KWANGU
Baada ya kuchoka kuvumilia nikamfuata rafiki yangu wa karibu Robert na kuanza kumueleza,  akaniambia kwanini usiende kuombewa, mbona wengi tu wanapona na hata mjomba wangu alikuwa anaumwa miguu alipoombea akapona. Nikamwambia sasa nikienda huko wazazi wangu waanifikiriaje? Akanijaza moyo na kunipa ujarisi kuwa “IMANI YAKO NA MUNGU SI YA WAZAZI WAKO BALI NI WEWE NA MUNGU WAKO NA HATA UKIFA UTAENDA NAO? SI WEWE NDIE UTAKAYE ENDA KUJIBU HUKO? FANYA MAAMUZI YALIYO SAHIHI”

Nikakubali! Basi nikasubiri jumapili ilipofika nikajiandaa na kwenda kanisani kuombewa, hakika nilipoombewa kila kitu kili badilika na kijisikia mwepesi kama vile nilikuwa nimebeba viroba vya michanga! Nilipoombewa nikadondoka chini na kupoteza fahamu. Baada ya dakika kadhaa nikaamka na kujikuta nikochini nimelala huku nikijishangaa nini kilichotokea.

Toka hapo nikaamini na nikaamua kuimba Nyimbo za Injili ili kueneza Neno la Mungu kwa wasiofahamu utamu wake.

Kwasasa nipo huru na ni kweli Yesu anatenda na Roho Mtakatifu yupo kwa ajili yako endapo utaamua kumpokea! Mungu ni mwema, Mungu anatenda. NAMSHUKURU KWA KUNIOKOA!