Advertise Here

Monday, December 31, 2012

Salamu za Mwaka Mpya 2013 kutoka "Gospel News Media".

 

Bwana Yesu Asifiwe!


Kipekee Nianze kwa Kumshukuru sana Mungu kwa kunipa pumzi ya Uhai ambayo bado inanipa nafasi ya kutuunganisha Mimi pamoja na Wewe. Nawashukuru pia wazazi wangu ambao wamekuwa Msaada mkubwa sana kwangu. Mwaka 2012 ulikuwa ni Mwaka wa Mafanikio sana kwangu ingawa si kwa asilimia mia, lakini kwa kiwango kikubwa nimefikia malengo niliyojiwekea kwa Mwaka wa 2012.
Blogger Sowane Emmanuel
 Nikiwa kama Mwanzilishi wa Blog hii ya kikristo ya Gospel News Media, napenda kutumia fursa hii kukushukuru wewe Msomaji wa Blog hii, lakini pia niwashukuru watu wote ambao kwa Namna moja au Nyingine wamefanikisha Malengo ya Blog hii kwa Mwaka 2012. Sina cha kuwalipa ila Mungu wa mbinguni naamini ni Mkuu sana na Kamwe hata wapungukia.
Historia ya Blog Hii
Blog hii ilianza Mwaka 2011, ikiwa na Jina la Halleluyah Gospel Outreach ikiwa na link ya www.esowane.blogspot.com (Haiko hewani kwa sasa). Mwaka 2012 mwezi wa 2, blog nyingine ya kikristo ilianzishwa ikiwa kama mbadala wa blog ya Halleluyah Gospel Outreach, na blog hii ilikuwa ni Hot Gospel News ikiwa na link ya www.hotgospelnews.wordpress.com (Bado ipo hewani mpaka sasa ingawa haitumiki tena). Miezi michache baadae, blog hiyo ilibadilishwa Jina kutoka Hot Gospel News na kuwa Gospel News Media ikiwa bado na link ile ile. Baada ya Miezi 6, yaani Agosti Mwaka huu, ndipo Blog hii ya Gospel News Media ikiwa na Link ya www.gospelnewsmedia.blogspot.com ilipoanzishwa rasmi. Mabadiliko yote hayo yalifanyika ili kuhakikisha kwamba ubora wa kutosha unapatikana.

Shukrani za Dhati
Napenda sana kumshukuru Brother Victor Nivox (Mmiliki wa Blog ya Kikristo ya Hosanna Inc) ambaye alinipa hamasa ya kutosha ya kuanzisha Blog ya Kikristo. Alitoa muda wake kwa kunifundisha, kunielekeza na kunikosoa pia pale alipoona sipo sawa. Mungu akubariki sana kwa Msaada wako Kaka Victor ambao umefanya leo nimefika hapa. Mimi ni Moja ya Matunda yako!
Victor Nivox
 Pia napenda sana kuwashukuru wamiliki wenzangu wote wa blog za kikristo kwa Ushirikiano na Msaada wao ambao wamenipa mpaka leo nimefika hapa. Napenda nitambue wa Mchango wa Patrick Samson Sanga(Patrick Sanga Ministry)  Mary Damian(Strictly Gospel), Samuel Sasali(Sam Papaa Blog), Ambwene Michael(Gospel Kitaa), James Temu(Uncle Jimmy Blog), Jacqueline Moshi(Real Life 4 Christian), Firmina Matee(Amenhalleluyah Blog), Baraka Samson(Mjap Inc), Faraja Naftal(Fmndeme Blog), Tunu Bashemela(Gospel Vision),  King Chavala(Chavala Blog), Rulea Sanga(Ruma Africa Blog), Erick Brighton(Pamoja kwa Umoja Blog) na wengine wengi.
Baadhi ya Wamiliki wa Blog za Kikristo Tanzania, baada ya kikao kilichofanyika Octoba Mwaka 2012 Jijini Dar es salaam
Mbali ya hawa, napenda pia kutambua Mchango wa watu wangu wa karibu ambao walikuwa Msaada mkubwa sana kwa kufanikisha malengo ya blog hii, baadhi ni kama Adolph Nzwalla, Barnabas Shija, Elia Migongo, Buberwa, Nyamiti Kayora, Maganga Gwensaga, Joel Kaema, Ruth Lyanga, Vick Bonge, Shija Chongolo, Mary Ramadhani, Members wote wa TAFES SAUT, Wafanyakazi wenzangu wote wa Alive Fm na Wengine wengi.

Malengo ya kuanzishwa kwa Blog Hii
Kutokana na Mabadiliko ya Sayansi na Teknolojia, Dunia sasa inakuwa si kijiji tena, bali ni Nyumba moja. Mabadiliko hayo yanaleta umuhimu kwa sisi tukiwa kama wakristo, kuweka sehemu maalum ambayo wakristo wengi watapata habari mbalimbali za kikristo na mafundisho ya Neno la Mungu kupitia Mtandao.

Tasmini ya Blog hii Kwa Mwaka 2012
Najua tumefanya mengi sana kwa Mwaka 2012, Mimi pamoja na Team yangu nzima. Pengine kuna ambayo tuliyafanya tukihisi ni mazuri, kumbe kwa namna moja ama nyingine ilikuwa ni kwazo kwako. Pale tulipokosea na kukukwaza tunaomba utusamehe sana, na tuanze Mwaka Mpya wa 2013 tukiwa na amani ndani ya Mioyo yetu.

Tunakuahidi uboreshaji wa utaratibu wetu wa utoaji wa habari, na mafundisho mbalimbali. Lakini pia tunakaribisha Maoni yako au Ushauri wako ili kuboresha Blog hii. Mchango wako wa Mawazo ni wa Muhimu sana katika kuboresha Blog hii.

Gospel News Media-Team inawatakia Heri ya Mwaka Mpya 2013. Tunawashukuru wote na Mungu awabariki sana!

Kwa Maoni/Ushauri, Wasiliana Nami;
Sowane Emmanuel
0712 113305
0754 030789
Email; sowane@ymail.com
 Facebook Page; Gospel News Media

Msama Promotions yakabidhi Msaada wa Vyakula na Ada.

Bw. Alex Msama akikabidhi Misaada hiyo
Mkurugenzi wa kampuni ya Msama Promotion, Bw. Alex Msama akimkabidhi sehemu ya msaada wa vyakula Mkurugenzi wa Kituo cha kulelea watoto wanaoishi katika mazingira magumu cha Mwandaliwa, Halima Ramadhani. Mbali ya kukabidhi msaada wa vyakula hivyo, Msama pia alikabidhi hundi ya sh milioni 1.5 kwa ajili ya kulipia ada za wanafunzi waliofukuzwa shule. Msaada huo  umetokana na mapato ya tamasha la Pasaka lililofanyika Mwaka 2012. Hafla hiyo ilifanyika Mbweni nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam, Mwishoni mwa wiki.

Sunday, December 30, 2012

Mambo ya kukusaidia unapoweka Malengo ya Mwaka 2013.

Mwl. Patrick Samson Sanga
 KATIKA kuumalizia mwaka huu wa 2012, nataka nikutafakarishe kwa kukuuliza swali hili, Je! malengo yako uliyojiwekea katika mwaka 2012 katika nyanja mbalimbali kama vile kiroho, kihuduma, kifamilia, kikazi, kibiashara, kiuchumi nk yamefanikiwa kwa kiwango gani? Na kama hujafanikiwa je umejiuliza kwa nini hujafanikiwa kwa kiwango ambacho unaamini ulitakiwa kufanikiwa? Je, umegundua nini ni vikwazo vya wewe kufikia malengo yako?

Kama ukiyatafakari maswali hayo hapo juu utagundua kwamba najaribu kutaka kujua kama kwanza huwa una tabia ya kuwa na malenngo, na kisha kuweka mikakati inayotekelezeka ili kufikia hayo malengo, na mwisho kufanya tathimini   mara kwa mara ili kupima malengo yako yanafanikiwa kwa kiwango gani kadri siku zinavyozidi kwenda.

Naam najua si watu wengi sana wenye tabia ya kujiwekea malengo na hasa wapendwa. Ukiwauliza kwa nini huna malengo? atakuambia naenda kwa imani. Ukimuuliza imani maana yake nini? Atakujibu, kuwa na uhakika wa mambo yatarajiwayo tena bayana ya yale yasiyoonekana (Waebrania 11:1).

Tatizo la wapendwa wengi ni kutokujua uhusiano uliopo kati ya imani na mtu mwenye malengo. Kulingana na tafsiri ya imani ni dhahiri kwamba, kuwa na malengo ni namna mojawapo ya kuwa na imani, kwani ili imani iwepo ni lazima kuwe na matarajio. Hivyo unapoweka malengo maana yake unaifanya imani yako kuwa na uelekeo, kwa kujua mahali unapotaka kufika.

Kuna tafsiri nyingi za malengo na hasa kwa kutegemeana na kile unachotaka kukipata au kukifikia, lakini tafsiri rahisi zaidi ni hii. Malengo ni hatua fulani katika maisha ya mtu ambayo hajaifikia na hivyo anataka kuifikia. Na jambo la msingi, unapaswa kufafanua vizuri lengo husika ambalo unataka kulifikia. Ufafanuzi mzuri wa lengo au malengo yako utakusaidia katika kujiwekea mikakati mizuri yenye kutekelezeka.

Katika ujumbe huu mfupi wa  funga mwaka ya 2012 nataka tu kukukumbusha mambo kadhaa ya msingi yatakayokusaidia unapoanza kuweka  malengo yako ya mwaka 2013.

1. Weka malengo yako mapema, kwa kuzingatia vipaumbele vyako.
Ni vema ukaweka malengo ya mwaka unaofuata kabla mwaka huo haujaingia. Mfano, kama mpaka sasa bado hujaweka malengo unayotaka kuyafikia katika mwaka 2013 basi tumia muda huu uliobaki kufanya kazi hiyo. Kwa nini nasema jambo hili, hii ni kwa sababu utekelezaji wa malengo yako unapaswa kuanza tarehe 01.01.2013 kama tukifika kwa neema yake Kristo.

Kwa hiyo kama tarehe hiyo ikifika hujapanga malengo yako jua kwamba tayari umeanza vibaya na kuna uwezekeano mkubwa wa kutokufikia malengo yako. Ikiwa ulishaweka malengo kwa kipindi cha mika mtatu, mtano au zaidi, bado pia unalazimika, kuyafafanua vizuri hayo malengo yako kwa kuzingatia mazingira yaliyopo na rasilimali utakazohitaji. Naam unapoweka malengo kumbuka kuyawekea  muda wa hilo lengo kufikiwa.

Mfano;
Moja ya malengo yangu kila mwaka kihuduma, ni kuandaa masomo yasiyopungua hamsini(50) na kuyaweka kwenye blog. Ukichukua 50 ukagawanya kwa miezi kumi na mbili unapata wastani wa masomo manne kila mwezi. Na hii ina maana kila wiki ni lazima niandae somo moja. Kwa hiyo ikipita wiki sijaandaa somo, ni dhahiri kwamba nitakwama katika kufikia malengo yangu. Nimekupa mfano huu rahisi ili uone umuhimu wa kuweka malengo mapema tena kwa kuyafunga kwenye muda.

Kwa uzoefu wangu katika kuweka malengo kikazi,kihuduma,kiuchumi, kifamilia, nk, nimejifunza na kugundua kwamba malengo ni muda, malengo ni mikakati na kisha malengo ni nidhamu uliyonayo katika kutekeleza mikakati na hasa ile inayohusu fedha. Muda ni ufunguo mkubwa wa kukusaidia kufikia malengo yako. Ukicheza na muda, huwezi kufikia malengo yako. Na kwa sababu hii ni lazima ujifunze kufikiri kimuda na kim-kakati kwa kila lengo unaloliweka.

Naam kufanikiwa kwa malengo ya Mtu binafsi, Shirika, Serikali nk kutategemea namna mtu/watendaji wa Serikali au Shirika husika wanavyotumia muda walionao, mikakati iliyopo na mwisho nidhamu yao katika utendaji wao. Naam, mambo haya matatu yakizingatiwa yatafanyika funguo za kufikia malengo yako au ya Shirika lako.
  
 2. Weka mikakati ya kutekeleza malengo yako.
Ili malengo yako yaweze kutekelezeka, sharti uwe na mikakati inayotekelezeka, vinginevyo huwezi kuyafikia malengo yako. Mikakati ni mbinu, njia utakazotumia katika kutekeleza malengo yako. Naam kwa kuwa malengo yako yanakuwa ndani ya muda fulani ni lazima na mikakati nayo iwe kimuda. Katika kuweka mikakati, kuna baadhi ya malengo yatakutaka ushirikiane na baadhi ya watu, sasa kuwa makini na nani unashirikana naye katika kuyafikia malengo yako.

3. Fanya tathmini ya utekelezaji wako wa malengo.
Watu wengi sana, huwa wanasahau sana hiki kipengele katika utekelezaji wa malengo yao, na ndio maana si wengi wanaofikia malengo yao. Tathmini unaweza ukafanya kwa vipindi viwili au vitatu kwa mwaka. Maana yangu ni kwamba unaweza uka-ugawa mwaka mara mbili na hivyo kuamua kwamba utakuwa ukifanya tathmini zako mwezi wa sita na kumi na mbili. Naam huu ndio mfumo ambao mimi binafsi huutumia. Hata hivyo kuna baadhi ya malengo huwa nayafanyia tathmini yake kila mwezi, ingawa tathmini kubwa huwa nafanya Juni na Desemba. Katika kufanya tahmini jambo kubwa ni kuangalia mikakati yako imekusaidia kwa kiwango gani kufikia malengo yako.

4. Boresha malengo kadri muda unavyokwenda, kwa kuzingatia tathmini unayoifanya.
Kama katika tathmini unayofanya mara kwa mara umegundua kwamba kuna lengo au malengo haya tekelezeki, basi kwanza litazame hilo lengo tena vizuri, kisha mikakati yake. Lazima kama siyo lengo, basi mikakati unayotumia haijakaa vizuri, na kwa hiyo unaweza kuliboresha lengo lako vizuri na hvyo mikakati yake pia. Mimi hutumia tathmini ya mwezi wa sita kurekebisha baadhi ya malengo na kisha kuboresha mikakati yake. Na kisha baada ya tathmini kubwa ya Desemba ndipo pamoja na mke wangu tunaweka malengo yetu ya mwaka unaofuta. Jambo la msingi hapa ni kuhakikisha kwamba malengo tunayoweka kila mwaka yanalenga kutufikisha kwenye malengo yetu ya miaka mitano mbele, tuliyokwisha kuyaweka tangu mwanzo.

5. Jenga mazoea ya kuyasoma na kutafakari malengo yako mara kwa mara.
Jambo hili litakuwekea msukumo wa kuhakikisha unatekeleza mikakati yako ili kuyafikia malengo yako. Mfano unaweza kuweka malengo yako kwenye Laptop/Computer yako,  unaweza ukaweka malengo yako kwenye meza yako ya kusomea au unaweza ukaweka ‘Remainder” kwenye simu yako iwe inakukumbusha kila wiki kupitia malengo yako nk. Hata hivyo ni vema ukaweka, malengo/mikakati yako, mahali ambapo ni salama kwa maana ambayo haitakuwa rahisi kwa mtu au watu wengine kuona, Shetani asije akawatumia hao katika kukwamisha malengo yako.

Kutokana somo hili, hebu angalia katika mwaka wa 2012 kama uliweka malengo, umeyafikia kwa kiwango gani? Naam kama haujafanikiwa vizuri, basi naamni somo hili litakusaidia katika kujipanga kwa mwaka 2013 ili kama kwa neema ya Mungu tukifika Desemba 2013 unapofanya tathmini ya mwisho wa mwaka uwe na sababu ya kumshukuru Mungu kwa namna alivyokusaidia kuyafikia malengo yako.

Mungu akubariki sana. Mimi na familia yangu, tunakutakia heri ya Mwaka mpya wa 2013 na Neema ya Kristo na iwe nawe daima.

Mwl. Patrick Samson Sanga
+255 755 816 800

Saturday, December 29, 2012

Kongamano la Kuingia Mwaka 2013 laanza rasmi leo Jijini Dar.

Mch. Florian Katunzi katika Moja ya Huduma zake
KONGAMANO la Siku 4 linalofanyika katika viwanja vya Maonesho vya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere zamani Sabasaba leo limeanza rasmi huku waimbaji mbalimbali pamoja na Watumishi mbalimbali wakihudumu.
Martha Mwaipaja akihudumu
 Kongamano hilo ambalo ni Maalum kwa ajili ya kuukaribisha Mwaka 2013 na Kumshukuru Mungu kwa kutupigania kwa Mwaka wote wa 2012, litafanyika kwa Siku 4 mfululizo kuanzia leo.
 
Upendo Nkone akihudumu katika Kongamano hilo siku ya leo
Kwa siku ya leo, waimbaji mbalimbali kama Upendo Nkone na Martha Mwaipaja walihudumu huku Watumishi wa Mungu kama Mch. Florian Katunzi wakitoa Mafundisho Maalumu kwa ajili ya kuuanza vizuri Mwaka 2013.
Watoto nao hawakuachwa nyuma
Mbali ya hilo, familia mbalimbali zitapata nafasi ya kuombewa ili Mungu afanye kitu katika Maisha ya familia hizo kwa Mwaka 2013. Matangazo haya pia yatakuwa yakirushwa hewani moja kwa moja kupitia Wapo Radio Fm(98.1Mhz).

Watu Wote Mnakaribishwa!!!

Padri aliyepigwa risasi Zanzibar, akana maelezo ya Polisi.

Padri Ambrose Mkenda alipokuwa katika hospitali ya Mnazi Mmoja akipatiwa matibabu baada ya kupigwa risasi na watu wasiojulikana
 PADRI Ambrose Mkenda ambaye alipigwa risasi Jumanne iliyopita, mjini Zanzibar na watu wasiojulikana amekana maelezo yaliyotolewa na polisi yakimtaja kuwa ni Mhasibu wa Kanisa Katoliki, Zanzibar.

Akizungumza na waandishi wa habari jana katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ambako amelazwa, Padri huyo alisema wadhifa wake ni Mkurugenzi wa Idara ya Uchungaji anayeshughulikia masuala yote ya Kanisa Katoliki visiwani humo.

Alisema hakuwa mhasibu wa kanisa hilo kama inavyoelezwa na kwamba taarifa hizo siyo za kweli.Hata hivyo, Padri Mkenda alisema alikuwa akimsaidia mhasibu kwa kipindi cha miezi mitatu.

“Mimi sikuwa mhasibu wa kanisa kama inavyoelezwa na watu. Napinga vikali taarifa hizo kwani mimi nilikuwa namsaidia mhasibu kwa muda tu kwani hakuwapo,” alisema.

Alipoulizwa jana kuhusu madai hayo mapya ya Padri Mkenda, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi, Aziz Juma Mohamed alisema asingeweza kuzungumza lolote kwa kuwa alikuwa nje ya kituo chake cha kazi licha ya kuwa na jibu la madai hayo.

“Sasa nipo Dar es Salaam kikazi. Naogopa kuandikwa kwamba nimetoa ufafanuzi juu ya suala uliloniuliza. Japokuwa majibu ninayo, lakini cha msingi ni kwamba jaribu kumtafuta kaimu wangu Haji Hana anaweza kuwapa majibu,” alisema Mohamed.

Alipoulizwa Kamanda Hana alisema inawezekana madai ya Padri Mkenda yakawa ya kweli kwa kuwa baada ya tukio hilo hakuweza kuzungumza lolote na badala yake maelezo yake yalitolewa na wasaidizi wake ambao ndiyo waliosema kwamba alikuwa mhasibu.

“Padri alikuwa akizungumza kwa ishara, hivyo hakuweza kusema chochote. Wasaidizi wake ndiyo wakatoa taarifa hizo kwamba ni mhasibu wa Kanisa.”

Akizungumzia hali yake Padri Mkenda alisema anaendelea vizuri lakini bado ana maumivu makali katika sehemu za mwili wake ikiwa ni pamoja na kichwani.

- Gazeti la Mwananchi -

Friday, December 28, 2012

Kanisa kufukua Makaburi 15 kupisha Ujenzi wa Hospitali Dar.

UONGOZI wa Kanisa la Katoliki, Parokia ya Kinyerezi  Dar es Salaam unalazimika kugharimia ufukuaji wa makaburi zaidi ya 15 ya Waislamu yaliyopo kwenye kiwanja namba 1370 kitalu B  kilichopo katika Kata ya Kinyerezi , baada ya kupewa kwa  shughuli za kijamii.
Akizungumza na mwandishi wa habari hii Mwenyekiti wa Parokia hiyo, Venance Kweka alisema wanalazimika kugharimia ufukuaji wa makaburi hayo ili yaweze kuhamishwa kutoka katika kiwanja kupisha shughuli nyingine za kijamii kama Ujenzi wa hospitali katika eneo hilo. 
Alisema tayari wamejiandaa kugharimia shughuli hiyo kwa kuwa makaburi hayo ndiyo pekee yanayokwamisha  kuanza kwa mikakati ya ujenzi wa hospitali hiyo, ambayo kanisa linaamini itakuwa ni msaada mkubwa kwa kinamama na watoto  wanaoishi katika eneo hilo la Kinyerezi.  
Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Manispaa Halmashauri ya Ilala Gabriel Fuime, ilifafanua kuwa itasimamia zoezi  hilo kwa  Sheria ya Serikali za Mitaa( Mamlaka na Miji) ya mwaka 1982, kanuni ya mwaka 2008 namba 4 c ambako itatumia wataalam wake. 
Fuime katika taarifa yake hiyo alisisitiza ndugu na jamaa wa waliozikwa katika eneo hilo kuwasiliana na Afisa Mtendaji wa Kata ya Kinyerezi wakiwa na barua ya utambulisho kutoka kwenye ofisi ya Serikali ya mtaa wanaoishi kabla ya Januari 20 mwaka 2013.
Alibainisha kuwa makaburi hayo yanatarajiwa kuhamishiwa kwenye makaburi ya Halmashauri ya Manispaa ya Ilala yaliyopo kata ya Kitunda eneo la Mwanagati  Februari 9 mwaka 2013 baada yataratibu zote kukamilika.
- Juma Mtanda -

Maswala ya Udini Tanzania, Maaskofu Wacharuka.

 JUKWAA la Wakristo Tanzania (TCF), limeitaka Serikali ya Rais Jakaya Kikwete kutoa ufafanuzi juu ya baadhi ya madai mbalimbali yanayotolewa na Waislamu dhidi ya Wakristo, vinginevyo Serikali ikiri kwamba inaunga mkono madai hayo ya Waislamu. 
TCF ni jukwaa linalojumuisha Taasisi kuu za Umoja wa Makanisa nchini, ambazo ni pamoja na Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT), Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Jumuiya ya Makanisa ya Kipentekoste Tanzania (PCT) na Kanisa la Waadventiste Wasabato (SDA).
Tamko hilo limetokana na maazimio ya kikao cha wawakilishi wa taasisi hizo kilichofanyika Dar es Salaam, Desemba 6 mwaka huu, chini ya Mwenyekiti wake Askofu Bruno Ngonyani na Katibu wake, Mchungaji Dk. Leonard Mtaita. Lilianza kutangazwa katika ibada ya Krismasi juzi usiku na kurudiwa jana katika Ibada ya Kataifa mjini Moshi na Askofu Dk. Martin Shao.
Katika tamko hilo ambalo limechapishwa kwa ukamilifu ndani ya gazeti hili , TCF inaitaka Serikali kutoa ufafanuzi juu ya madai kadhaa yanayotolewa na Waislamu mara kwa mara dhidi ya Wakristo, yakiwamo madai ya kwamba Serikali ya Tanzania imekuwa ikiongozwa na Mfumo Kristo.
Mengine ni madai ya kuwapo kwa ‘Memorandum of Understanding (M.o.U)’ ya mwaka 1992 baina ya Makanisa na Serikali kwa ajili ya huduma za Makanisa kuhusu sekta za afya na elimu, uchochezi unaofanywa na baadhi ya viongozi wa Kislamu dhidi ya Wakristo, tishio la kuuawa kwa maaskofu na wachungaji wa makanisa pamoja na tukio la uchomaji wa makanisa Mbagala na Zanzibar.
Kwa mujibu wa maaskofu na wachungaji hao, kuendelea kukaa kimya kwa Serikali kuhusu madai hayo ya Waislamu, kwanza kunachangia kuongezeka kwa uhusiano mbaya baina ya dini mbili hizo, na hivyo kuhatarisha umoja na mshikamano wa taifa lakini pia kunatoa taswira kwa viongozi hao wa Kanisa kujua kwamba Serikali inaunga mkono chokochoko zote hizo za Waislamu dhidi ya Wakristo.  
Kikao hicho cha TCF kimewaagiza viongozi wote wa makanisa nchini kusoma tamko hilo mbele ya waumini wao kabla ya mwisho wa mwaka huu, wakianzia na ibada za Sikukuu ya Krismsi na Mwaka Mpya kutokana na kile ambacho makanisa hayo yanasema juhudi zao za kutaka kukutana na Rais Kikwete ili wamweleze msimamo wao huo wa Kanisa nchini, kukwama.
Kuhusu madai ya kwamba Serikali ya Tanzania imekuwa ikiongozwa na Mfumo Kristo, tamko hilo la TCF linasema: “Maneno ya kashfa ya hoja kuwa nchi inaendeshwa kwa mfumo kristo, hayana msingi wowote. Jukwaa la Wakristo nchini linakanusha wazi kuwa nchi hii haiongozwi kwa mfumo kristo.
“Labda kwa kuwakumbusha tu, viongozi wote waandamizi wa ngazi ya juu Tanzania asilimia 90 ni Waislamu, itakuwaje nchi iendeshwe na mfumo kristo? Rais wa nchi na Amiri Jeshi Mkuu, Makamu wa Rais, Mkuu wa Usalama wa Taifa, Jaji Mkuu, Mkuu wa Jeshi la Polisi (wote hawa ni Waislamu).
“Upande wa Zanzibar (viongozi Waislamu) ni asilimia 100. Na si kweli kwamba Zanzibar hawapo Wakristo wenye sifa za kuongoza. Hata uwakilishi wa Tume ya Kuandikwa Katiba Mpya, theluthi mbili ya wajumbe wake ni Waislamu, na mifano mingine mingi tu hii ni baadhi tu.
“Nchi hii (inaendeshwa kwa) misingi ya kidemokrasia, na Serikali yake haina dini bali wananchi wake ndio wana dini. Jukwaa la Wakristo linaitaka Serikali ithibitishe ukweli huu badala ya kukaa kimya wakati maneno ya uchochezi kama haya yanaenezwa wazi na hadharani.”
Kuhusu M.o.U, tamko linasema: “Memorandum of Understanding (M.o.U) ya mwaka 1992, kwa ajili ya huduma za Makanisa (Afya na Elimu) kwa jamii ya Watanzania katika huduma za hospitali, vituo vya afya na zahanati pamoja na shule mbalimbali zinazoendeshwa na Makanisa. Kanisa limeendelea kujishughulisha na huduma hizi kwa jamii hata kabla ya uhuru na baada ya uhuru pasipo ubaguzi.
“Ili kuondoa hali ya Kanisa kuendelea kutukanwa, chuki na kukashifiwa juu ya M.o.U, ambayo ni jambo zuri la kuwahudumia Watanzania afya zao, Jukwaa la Wakristo linaitaka Serikali ama izirudishe hospitali na shule za Makanisa kwa wamiliki wake wa awali, yaani Makanisa, na zile za Waislamu warudishiwe. Kama hili haliwezekani, basi Serikali itoe tamko la ufafanuzi juu ya M.o.U hiyo, maana na makusudi yake na manufaa yake kwa Watanzania.”
Kuhusu uchochezi, matusi dhidi ya Kanisa na kuzorota kwa uhusiano baina ya Uislamu na Ukristo, Jukwaa hilo linasema: “Ni wakati wa kukubali kwamba misingi ya Haki, Amani na Upendo katika Taifa letu vimetikiswa kwa kiwango kikubwa. Uchochezi, kashfa, matusi na uchokozi wa maksudi unaofanywa na baadhi ya waumini wa dini ya Kiislamu ukiendeshwa na kuenezwa kupitia vyombo vya habari vya kidini, mihadhara, kanda za video, CD, DVD, vipeperushi, makongamano, machapisho mbalimbali na kauli za wazi za viongozi wa siasa na dini husika, pasipo Serikali kuchukua hatua yoyote ikibakia kimya tu, inatoa taswira kwa viongozi wa Kanisa kujua kuwa Serikali inaunga mkono chokochoko hizi. Jambo hili linavyoendelea kuachwa hivi hivi, linaashilia hatari kubwa ya kimahusiano siku zijazo.
Aidha, Jukwaa hilo la makanisa nchini limeitaka Serikali kuhakikisha kwamba hadhi ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere inahifadhiwa. “Huyu ni kiongozi aliyetoa maisha yake kwa ajili ya ustawi wa nchi yetu akitetea Watanzania wote bila kuwabagua, akiimarisha umoja, amani na upendo kwa watu wote. Kashfa, kejeli na habari za uongo dhidi yake ni kuondoa moja ya alama muhimu ambazo kiongozi huyo alisimamia kwa ajili ya umoja wa kitaifa, mambo yote hayo yanayoenezwa yanalenga kukipotosha kizazi hiki na vizazi vijavyo juu ya juhudi binafsi za kiongozi huyo kwa Watanzania aliowapenda sana.

Wednesday, December 26, 2012

Wachungaji wafukuzana KKKT Dayosisi ya Kaskazini kati.

Askofu Mkuu wa KKKT, Dr. Alex Malasusa
 HALI imezidi kuwa tete katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania(KKKT) Dayosisi ya Kaskazini Kati baada ya Mchungaji Philemon Mollel kufukuzwa kazi na kusimamishwa kutoa Huduma katika Kanisa hilo Nchini.

Wiki iliyopita bodi ya Dayosisi hiyo chini ya Uenyekiti wa Israel Ole Karyongi ambaye pia ni katibu mkuu wa KKKT, ilimtimua kazi Meneja wa Hotel ya Corridor Springs Bw. John Njoroge kwa Tuhuma za Ubadhilifu wa fedha.

Vyanzo vya Habari vinasema kuwa, Chanzo cha Mchungaji Philemon Mollel kufukuzwa kazi, ni kushindwa kutekeleza mambo matatu ambayo Tume maalum ilimtaka Mch. Mollel ayafanye, na alipewa Siku 3 za kuomba radhi na hakufanya hivyo.

Habari zaidi zinasema kuwa, mambo matatu ambayo Mch. Mollel alitakiwa kuyafanya ni; 1. Kumuandikia Barua Askofu wa Jimbo la Kaskazini Kati Dr. Thomas Lazer kueleza ni kwanini alimkashfu na kumdharau. 2. Kutoa tamko katika Mtaa wa Azimio Ibadani Desemba 23, kuomba radhi kwa yale aliyotamka.

3. Amwarifu Katibu Mkuu kwa Barua baada ya kuyatekeleza hayo na awe amefanya hivyo kabla ya Desemba 24 Mwaka huu.

Habari zinaeleza kuwa, walioteuliwa Desemba 14 Mwaka huu na kwenda kumuona Mch. Mollel ili kutekeleza hayo ni Pamoja na Msaidizi wa Askofu, Mch. Solomon Massangwa, Katibu Mkuu wa Jimbo la Arusha Magharibi Mch. Godwini Lekashu na Katibu Mkuu Israel Ole Karyongi.

Hata hivyo Mch. Mollel alipopigiwa simu, alikiri kupokea nakala ya barua hiyo ya kufukuzwa kazi na kuvuliwa Uchungaji lakini alisema hakuwa kwenye nafasi nzuri ya kulizungumzia hilo. Mch. Mollel aliongeza kwa kusema kuwa Uamuzi huo umechukuliwa kwa Chuki na Fitina, na haukuangalia madhara ya Deni la Sh. Billioni 11 endapo Kanisa litashindwa kulipa fedha hiyo.

- Habari Leo -

Matukio ya Ibada za Chrismas katika Makanisa Mbalimbali.

Baadhi ya Waumini katika Katika Ibada ya Chrismas(Jana) katika Kanisa la KKKT-Usharika wa Azania Front
Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu la Dar es salaam, Eusebius Nzigilwa akiongoza Ibada ya Mkesha wa Chrismas katika Kanisa la Mt. Petro, Osterbay Jijini Dar es salaam
Askofu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania, Dr. Alex Malasusa akihubiri katika Ibada ya Chrismas hapo Jana katika Kanisa la KKKT-Usharika wa Azania Front.    
Baadhi ya Waumini wa Kanisa Kuu la Mt. Joseph wakiwa katika Ibada ya Sikukuu ya Chrismas hapo Jana
Baadhi ya Akina Mama waliojifungua Siku ya Chrismas(Jana) wakiwa na watoto wao katika Hospitali ya Mwananyamala, Jijini Dar es salaam.
Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es salaam Muadhama Polycarp Kadinali Pengo akipokea Michango mbalimbali ya fedha kutoka kwa Viongozi wa Jumuiya za Kikristo katika Jimbo la segerea

Tuesday, December 25, 2012

Ujumbe wa Krismasi toka kwa Mwl. Christopher Mwakasege.

Mwl. Christopher Mwakasege
 Mimi na mke wangu na familia yetu yote, yaani watoto na wajukuu, tunakutakia sikukuu njema ya krismasi.
Ujumbe nilionao kwako ni kutoka katika kitabu cha Mathayo 2:1-23. Ndani ya ujumbe huu napenda kukuambia mambo mawili makubwa.

Jambo la Kwanza
Yesu Kristo alipozaliwa Bethelehemu, si kila mtu alifurahi. Biblia inasema ya kuwa kuzaliwa kwa Yesu kuliposikika: " Mfalme Herode....alifadhaika, na Yerusalemu pia pamoja naye"(Mathayo 2:3). Kwa hiyo, hata wewe usishangae unapoona si kila mtu anafurahi juu ya kuokoka kwako. Si kila mtu atafurahi atakapoona Yesu anazaa kitu moyoni mwako. Na pia usitegemee kuona kila mtu anayekuona unadumu katika Kristo atakufurahia

Jambo la Pili
Kama vile Mungu alivyomsaidia na kumlinda Yesu alipozaliwa asiuwawe na wale waliochukia kuzaliwa kwake,uwe na uhakika Mungu huyu atakilinda kilicho cha Yesu katika maisha yako, kisiuwawe na wanaokichukia.

Naamini ujumbe huu utakutia moyo katika siku hii muhimu.

Thursday, November 22, 2012

Noel Didas ndani ya Ujio Mpya wa "Nuru ya rohoni".

Noel Didas Shirima
 Noel Didas Shirima anayejulikana sana kama Noel Didas, ni mwimbaji wa Nyimbo za Injili toka mkoani Arusha, Tanzania mwenye albam 2 mpaka hivi sasa.

Akizungumza nami kwa Njia ya Simu katika Kipindi cha Gospel Sound kupitia Hhc Alive Fm ya Jijini Mwanza kinachoruka kila Siku za Jumamosi kuanzia Saa 8 Mchana – Saa 10 Jioni, Noel amesema ameshakamilisha albam yake Mpya ya 3 aliyoipa jina la Nuru ya Rohoni itakayotoka hivi karibuni.
Sowane Emmanuel akiwa katika Studio za Hhc Alive Fm
 Kwa mujibu wa Maelezo ya Noel, albam hiyo ina nyimbo 10 ambazo zote amerekodia katika Studio ya Christ Studios ya Jijini Arusha chini ya Producer Mtangoo. Baadhi ya Nyimbo zilizomo kwenye albam hiyo ni kama Furika Roho Mtakatifu, Uzuri wa Yesu, Kuna Kuinuka Tena, Nimechagua maneno yako na Ninataka Kuingia Mjini kwa Mungu.

Mbali ya hilo, Noel amesema pia yuko mbioni kufanya Video ya Albam yake ya Pili yenye Jina la Uniinue Viwango Vingine atakayoifanya na Kampuni ya Gospel Media ya Jijini Arusha. Albam hiyo ya Pili ina Nyimbo kama Jina lako Mtakatifu, Kuna Wakati Nashindwa, Nimekutana na Mwanamume, na Yesu ni Rafiki. Audio Albam hii ya Uniinue Viwango Vingine aliirekodia Jijini Mbeya katika Studio za High Pitch Records chini ya Producer Fredy Kameta.
Cover la Album ya Uniinue Viwango Vingine
 Mwezi wa 5 mwakani (2013) Noel anatarajia kufanya Live Recording Video ya Nyimbo za Kusifu na Kuabudu Jijini Mwanza akishirikiana na Waimbaji mbalimbali akiwemo Solomon Mukubwa. Video hiyo itajumuisha Nyimbo za Kusifu na Kuabudu zilizomo kwenye Albam zake zote 3, na Nyimbo Mpya za Kusifu na Kuabudu atakazoziongezea.

Audio Albam yake ya Pili anaisambaza yeye mwenyewe. Kwa Ushauri, Maoni, au kama utahitaji Albam hiyo tafadhali Wasiliana na Noel Didas mwenyewe ili akupe maelekezo ya Jinsi gani utapata Albam hiyo.

Noel Didas Shirima
0655 115990
0765 115990

Muswada wa kuwaapisha wanawake kuwa makasisi wapingwa Uingereza.

Mkuu wa kanisa la Anglikana duniani Rowan Williams
Mkuu wa kanisa la Anglikana duniani, Rowan Williams

KANISA la Anglikana nchini Uingereza limetupilia mbali uwezekano wa kuwaapisha wanawake kuwa makasisi huku kiongozi wa kanisa hilo akionesha wazi kusikitishwa na hatua hiyo.

Uamuzi huo umechukuliwa baada ya kupiga kura katika uchaguzi uliofanyika juzi nchini Uingereza na kushuhudia makasisi waliopiga kura wakiupinga muswada huo kwa asilimia 76.7 ya kura.

Uamuzi huo huenda ukaleta madhara makubwa katika kanisa hilo ambapo kulikuwa na matumaini makubwa ya kuboresha na kufanya marekebisho katika taasisi za kanisa hilo la Anglikana.

Kiongozi wa kanisa hilo duniani, Rowan Williams ambaye anamaliza muhula wake Desemba ijayo, amebainisha masikitiko yake kuona muswada huo unashindwa kupasishwa baada ya kupambana kwa muda wa miaka 10.

Wednesday, November 21, 2012

Sanamu ya Papa John Paul yazinduliwa Upya baada ya kuzua tafrani hapo awali.

Sanamu Mpya ya Papa Yohane
 Katika kile kinachooonekana kuwa ni marekebesisho ya makosa yao, Roma wamezindua upya sanamu ya Papa Yohane (John) Paul tarehe 19 Novemba, baada ya ile ya awali kushambuliwa na kuharibiwa na watu kwa madai ya kuwa haifanani katu na baba huyo mtakatifu, bali kama dikteta Benitto Mussolini.

Msanii ambaye amefanya kazi ya kuirekebisha, Oliviero Rainaldi amesema kwamba ameridhishwa na matokeo ya alichokifanya, kwani ndicho alichokuwa nacho kwenye mawazo yake.

Hapo awali baada ya kuzinduliwa mnamo 2011 mwezi Mei, mkosoaji kutoka Vatican alisema kwamba sanamu hiyo inaonekana kama vile bomu ndo limetua, na si Papa wetu mpendwa kama inavyotakiwa.

Sanamu kushoto ikiwa imeharibiwa, na kulia ikiwa baada ya marekebisho
Sandro Barbagallo anaendelea kusema kuwa baada sanamu hiyo kukosewa, na kwamba ni watu wachache walioweza kumtambua kama Papa, basi ilibidi haraka iwezekanavyo meya wa jiji la Rome akutane na wasanii wataalamu wa uchongaji, maofisa utamaduni na wanazuoni ili kuweza kuokoa jahazi. Na hapo ndipo michoro ya Rainaldi ilipopitiwa upya na kufanyiwa kazi ipasavyo, jambo ambalo sasa limefanikiwa, kwani Papa amewekewa tabasamu, na pia anaonekana kuwa na shingo tofauti na hapo awali ambapo kichwa chake kilifananishwa na tufe (mpira wa bowling).

Hata hivyo katika uzinduzi huo wa mara ya pili, wananchi siku zote hawakosi ya kusema, na mjenzi wa barabara mwenye umri wa miaka 54 akafunguka.

"Sasa hivi inapendeza, naona wamefanya kazi nzuri, sio kama ilivyokuwa mwanzoni, naona wamerekebisha uso, sasa nona tabasamu na pia shingo ipo. Kazi ni nzuri".

Lakini msafiri mmoja akasema aliyefahamika kama Alberto Donella amekuwa tofauti na wenzake, yeye akisema.

"Sio yeye, sio yeye kabisa, alikuwa mwenye furaha - sio kitu kama hiki" Alberto alisema alipokuwa akipita kando ya hilo sanamu na kuongeza, "Kwangu mimi hiki naona kama ni jokofu tu".

- Gospel Kitaa -

Tuesday, November 20, 2012

Dk. Malasusa: Viongozi wa dini kuweni mfano.

Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Dk. Alex Malasusa
VIONGOZI wa dini wametakiwa kuwa mfano katika maeneo wanayoyaongoza ili kuendelea kudumisha amani  kwa ajili ya ustawi wa nchi.

Rai hiyo ilitolewa juzi na Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Dk. Alex Malasusa, alipokuwa akihubiri katika  ibada ya kumweka wakfu, Askofu wa Dayosisi ya Dodoma, Amon Kinyunyu.

Dk. Malasusa alisema Serikali imetoa uhuru wa kuabudu hivyo viongozi wasiposimamia amani iliyopo watahatarisha uhuru uliopo wa kuabudu.

 “Kwa sasa hivi tunaona vurugu zinazosababisha kufyatuliwa kwa mabomu ya machozi, hatupendi kuona risasi za moto zinatumika kwa kuwa wakati huo itakuwa ni vigumu kupata muda wa kuabudu,” alisema.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk. Rehema Nchimbi, ambaye aliiwakilisha serikali, alisema  viongozi wa dini wasibadilike, wahubiri amani na sio vurugu.

Dk. Rehema Nchimbi alisema serikali haina dini ila imetoa uhuru wa kila mwananchi kuabudu dini anayoitaka bila kuingiliwa uhuru wa mtu mwingine.

Aliwataka viongozi wa dini kumwogopa  Mungu aliyewaweka katika nafasi hizo na kuwasaidia katika kufanya mema.

Kwa upande wake, Askofu Kinyunyu aliwaomba waumuni wa Kanisa hilo kujikita katika kuendeleza mema yaliyoanzishwa na Askofu aliyemaliza muda wake, Festo Ngowo.

Alisema Askofu Ngowo alianzisha ujenzi wa ofisi za Dayosisi hiyo, ujenzi wa shule ya sekondari na miradi mingine mbalimbali ya Kanisa hilo.

Askofu Kinyunyu alichaguliwa kushika nafasi hiyo baada ya Askofu Ngowo kuugua kwa zaidi ya miaka miwili.

 Kwa mujibu wa taratibu za KKKT, inapotokea askofu akaugua zaidi ya muda huo, askofu mwingine huchaguliwa kuchukua nafasi hiyo.

- Nipashe -

Monday, November 19, 2012

R.I.O.T Presents Men's Conference from 19-25/Nov/2012 in Dar es Salaam.


Righteous Invasion of Truth (R.I.O.T) gladly brings ‘Men of Valor’, its first men’s conference in Dar es Salaam. M.O.V. is an interactive platform, reaching out to men across different ethnic groups, socioeconomic and religious backgrounds to restore, transform, equip and edify the man holistically.

Men have a natural tendency of internalizing issues. When you ask a man what he is thinking when things are up to his neck, without a glance, he’ll instinctively say, “Nothing”. Men do cry, but their tears are only visible from the inside. That’s why God had to say, “It is not good for a man to be alone”. As much as studies show that women are twice as much susceptible to depression, surprisingly the male-to-female ratio for completed suicides is greater than 4:1

When in this state where the internalization of things has reached its limit, men tend to shift the blame for how they feel on the inside to outside things. We exhibit anger or irritability over everything. Men are more prone to using alcohol or drugs as an outlet. As if this isn’t enough, the male infant has a higher mortality rate than the female. Let alone the fact that the woman has a higher life expectancy rate.

To those that have overcome these obstacles, there is still no rest for them. The enemy has strategically planned to emasculate the ‘man’ figure from marriage, family and even the society at large. The ‘man’ as an authority figure is being undermined from his God-given position bestowed upon him from Genesis by God Himself.

How can men prevail this ongoing fierce battle?  If only we could learn the greatest ‘Art of War’ – PRAISE!  You might be the least in your father’s house or perhaps you are coming from the poorest family in your clan, but I clearly hear the Commander-in-Chief of the Army of The Lord saying this to you: “Jehovah is with you, Mighty Man of Valor”!

The Event will be conducted at Makumbusho Hall near Institute of Finance(IFM)
From 19th-25/Nov/2012
Time:5;30Pm - 8:30Pm

We welcome you all Men and Women!

Saturday, November 17, 2012

Video ya "U Mwema" ya Felix Mshama, Noel Mlabwa na Barnabas Shija.


Kuanzia kushoto ni Felix Mshama, Noel Mlabwa, na Barnabas Shija

KWA wahudhuriaji wa Event nyingi sana za Injili za Jijini Mwanza, hizi sura pamoja na majina yatakuwa sio mageni kwao. Hawa ni Vijana toka Jijini Mwanza ikiwa ni Mazao ya Tanzania Fellowship of Evangelical Students(TAFES) katika Chuo Kikuu cha Mt. Agustino cha Jijini Mwanza.

Safari yao ya Uimbaji ilianzia mbali kidogo, kila mmoja akiwa na historia yake, lakini kukutana kwao TAFES Saut, kuna tengeneza historia nyingine ya vijana hawa katika kumtumikia Mungu, na safari hii ni katika wimbo wao mpya wa "U Mwema".

Wakiwa katika studio za Makaya records za Jijini Mwanza, vijana hawa wanapata Idea ya kufanya wimbo kwa kutumia Acoustic Guitar, chombo kilichopigwa na Felix Mshama toka Mwanzo wa wimbo mpaka mwisho.

Tofauti na Utengenezaji wa Video tuliouzoea kwamba inaanza audio halafu ndo inafuata video, utengenezaji wa video hii ilianza Video kisha Audio ndo ikafuata kwa kutengenezwa katika Studio za Makaya Records.

Video Producer wa Wimbo huu akiwa ni Wynjones Kinye toka Kinye Media ndo aliyehakikisha Video hii ina ubora wa kutosha huku rangi ya video hii ikiwa ni ya tofauti na rangi za kawaida tulizozizoea kuziona kwenye video nyingine.

WASIFU WAO
Barnabas Shija
  • Aliwahi kuwa Praise leader wa Tafes mkoa wa Mwanza(2010/2011).
  • Ni mmoja wa waimbaji waliofanya Back up katika Event ya Jehovah Yu Hai tour katika Mkoa wa Mwanza.
  • Alishawahi kurekodi audio albam ambayo hakuitoa kutokana na Sababu za Ubora wa Kazi.
  • Kwasasa anahudumu katika Praise Team ya Kanisa la FPCT la kurasini Jijini Dar es salaam.
  • Graphic Designer (Banners na Posters)
  • Kitaaluma ni mhitimu wa BA. Mass Communication (2012), SAUT-Mwanza.
 
Felix Mshama
  • Mpiga Gitaa aina ya Acoustic na Bass.
  • Aliwahi kuwa Mwalimu wa kwaya ya Caanan Anglican ya mkoani Dodoma akiwa na umri wa Miaka 18.
  •  Kitaaluma ni Mwanasheria (LLB, Saut-Mwanza, 2012)

Noel Mlabwa
  •  Mwimbaji wa Gospel Band ya Kingdom worshipers ya jijini Mwanza.
  • Mpiga Drums mwenye mapenzi sana na mahadhi ya kikongo.
  • Mwanasheria mwanafunzi Mwaka wa 4, Saut-Mwanza.
Wasiliana Nao, Kwa Namba zifuatazo;
0717 642263
0716 093245
0719 995061

Sasa itazame Video hiyo iliyopewa jina la "U Mwema"