Advertise Here

Monday, November 18, 2013

Rose Muhando aingiza hasara ya Milioni 15 kwa kutokufika kwenye Tamasha huko Tabora.

Rose Muhando
Mwimbaji wa Nyimbo za Injili toka Tanzania, Rose Muhando ameshindwa kutokea kwenye Tamasha la Uzinduzi wa Album ya Mwimbaji wa Nyimbo za injili toka Tabora, Mch. Egon Israel, Album ijulikanayo kama "Nakuombea Jirani".

Rose Muhando alialikwa kuimba kwenye Tamasha hilo kwa Gharama ya Sh. Milioni 2, pesa iliyolipwa kupitia Akaunti ya Rose Muhando ya Benki ya NMB.

Kwa Mujibu wa Maelezo ya Mchungaji Egon Israel, kutokufika kwa Rose Muhando kwenye Tamasha hilo, kumeingiza hasara ya Sh. Milioni 15, huku watu waliofika kwenye Uzinduzi huo wakirudishiwa pesa zao.

Tamasha hilo lilifanyika Jana katika Uwanja wa Ally Hassan Mwinyi huku Mkuu wa Mkoa wa Tabora Bi. Fatma Mwasa akiwa ndiye Mgeni rasmi.

Katika kutuliza vurugu zilizotokana na kutokufika kwa Rose Muhando, Kikosi cha Kutuliza Ghasia(FFU) Mkoani Tabora, walifika Uwanjani hapo ili kutuliza Ghasia hizo.

Mpaka sasa, waandaji wa Tamasha hilo wanafanya jitihada za kumtafuta Rose Muhando kujua sababu ya yeye kutokufika katika Tamasha hilo, huku waandaji hao wakidai kuwa Rose hapatikani kwenye simu yake toka jana, na mara chache anapopatikana hataki kupokea simu zao.

Hii si mara ya kwanza kwa Rose Muhando kutokufika kwenye Matamasha anayoalikwa, huku sababu za Msingi zikiwa hazijulikani.

Saturday, November 16, 2013

Makanisa Nchini Zimbabwe yakataa kulipa Kodi.

Wakati serikali ya Zimbabwe ikifikiria kuyatoza kodi Makanisa Nchini Zimbabwe, Viongozi mbalimbali wa Makanisa Nchini humo, wamepinga hatua hiyo huku wakisema Makanisa hayapaswi kulipa kodi mana yanafanya kazi ambayo Serikali imeshindwa kuifanya hivyo kwao ni kama Unyanyasaji kwa Makanisa.

Wakati hayo yakiendelea, Mkuu wa Mawasiliano wa Mamlaka ya Mapato Zimbabwe, Taungana Ndoro amesema hana kauli rasmi kuhusiana na Ukandamizaji huo kwa Makanisa kwani kuna timu maalumu iliyoundwa kuchunguza swala hilo hasa vyanzo vya Mapato ya Makanisa.

Askofu Noah Pashapa wa Kanisa la "Life and Liberty" amesema Makanisa hayapaswi kuliko Kodi, isipokuwa kwa yale Makanisa yanayoendeshwa kama Biashara, hayo ndo yalipe Kodi.

Hapa Askofu Pashapa anasema, "Kuna Makanisa yanaendeshwa kama Biashara kwa kua yanamilikiwa na watu na wananufaika na Sadaka pamoja na Mafungu ya Kumi moja kwa moja. Na pia kuna Makanisa yanayoendeshwa Kiimani zaidi na hayategemei faida, huku kipato kikielekezwa katika Maendeleo ya Kijamii".

Aliongeza kuwa, Makanisa hayo yanayojiendesha kibiashara, ndiyo yanayopaswa kulipa Kodi.

Kasisi atekwa huko Cameroon.

Kasisi mmoja mfaransa ametekwa nyara Kaskazini mwa Cameroon karibu na mpaka wa Nigeria. Taarifa hii ni kwa mujibu wa Wizara ya mambo ya nje ya Ufaransa.

Kasisi huyo, Georges Vandenbeusch alitekwa nyara mapema asubuhi mnamo siku ya Alhamisi, umbali wa kilomita 30 kutoka mpakani.

Takriban watu 15 waliokuwa wamejihami, walivamia makao ya Nguetchewe ambako kasisi huyo alikuwa akifanya kazi , kulingana na Askofu mkuu.

Kundi la wapiganaji wa Boko Haram, wanajulikana kuendeshea harakati zao katika eneo hilo.

Askofu mkuu ambaye kasisi huyo alikuwa chini yake, alisema kua kijisanduku cha kasisi huyo kilipatikana barabarani.

Baadhi ya waliofanya kazi na kasisi huyo walisema kuwa watekaji nyara walifika kwa miguu kumteka nyara kasisi na kuwa walikuwa wanaongea kiingereza.

Msemaji wa serikali ya Cameroon, Issa Tchiroma Bakary, alisema kuwa maafisa wanahofia kwamba kasisi huyo tayari ameondolewa nchini.

Kwa mujibu wa maafisa wakuu, huenda wapiganaji wa Boko Haram ndio waliomteka kasisi huyo.

Rais Francois Hollande, amesema kuwa wanafanya kila hali kuhakikisha kuwa kasisi huyo ataachiliwa.

Akizungumza mjini Monaco, aliwasihi raia wa Ufansa kutohatarisha maisha yao.

Mapema mwaka huu, jamaa saba wa familia moja , wanne kati yao watoto, walitekwa nyara na wapiganaji wa kiisilamu na kuzuiliwa kwa miezi miwili.

- BBC Swahili -

Dhehebu Jipya linalomwamini Yohana Mbatizaji kuliko Yesu laibuka huko Kenya.

Dhehebu jipya limeibuka huko Nchini Kenya lijulikanalo kama "Gospel of God" huku likiwa linamwamini Yohana Mbatizaji ambaye alikufa na Kufufuka, na si Yesu, kinyume na Wakristo wengine Ulimwenguni.

Kwa Mujibu wa Imani yao, Yohana Mbatizaji alikufa na kufufuka Nchini Zimbabwe mnamo Octoba 1914. Waumini hawa kwao ni Marufuku kutoa fungu la kumi, na kwa kawaida Ibada zao hufanyia Nje ya Nyumba za Waumini huku Wanawake wakisalia Mbali na Wanaume.

Tazama Video hii ujionee mambo yalivyo
- Swahili Hub -

Friday, November 15, 2013

Sonnie Badu asherehekea Birthday yake na Watoto yatima huko Ghana.

Sonnie Badu orphans
Sonnie Badu akiwa na watoto yatima
Mwimbaji wa Kimataifa wa Nyimbo za injili aliyegusa Maisha ya watu mbalimbali kwa nyimbo zake, Sonnie Badu Jumamosi iliyopita yaani Novemba 9, alisherehekea siku yake ya kuzaliwa na Watoto yatima katika Vituo vinne tofauti huko Ghana.

Alitembelea Vituo vya Remar Ghana Christian Rehabilitation Center in Dansoman, Teshie Orphanage, New Life Orphanage International kilichopo Nungua na Lighthouse Christian Children’s Home kilichopo Aburi.

Katika vituo vyote alivyotembelea, watoto waliandaliwa kwa ajili ya kumlaki Sonnie kwa Nyimbo maarufu kama "Baaba" na "Let it rain".

Katika kila eneo alilotembelea, alikula pamoja na watoto hao keki yake ya birthday pamoja na kuchangisha kiasi cha pesa kwa ajili ya kuwasaidia watoto hao.

Sonnie aliwasili Ghana wiki iliyopita kwa ajili ya Maandalizi ya Tamasha atakalolifanya Nchini Ghana Novemba 30, Mwaka huu.