|
Mwinjilisti Simon Mkanza |
Shaloom Mpendwa!
Upo umuhimu wa kujua neno la Mungu katika maisha ya Mkristo halisi. Biblia inatuambia Yesu Kristo ndiye Neno la Mungu. Kwa maneno mengine Yesu ndiye Neno ambalo Mkristo anapaswa kuwa nalo (Yohana 1:1).
Kwa kusema hivyo kuna umuhimu wa kumjua Yesu na kumshika, kwa maana
yeye ndiye Neno la Mungu. Katika Biblia mtume Petro anasema mbele za
Yesu kwamba, twende kwa nani na wewe ndio mwenye maneno ya uzima? Petro
alijua upo umuhimu wa kumjua Yesu kama Neno maana ndani ya Neno kuna
uzima
Biblia inasema neno la Kristo likae kwa wingi ndani yetu (Wakolosai 3:16).
Kwa nini basi neno la Kristo likae kwa wingi ndani yetu? Ni kwa
sababu lina mambo yafuatayo ambayo ni muhimu katika maisha yetu ya
Ukristo. Mambo hayo ni…
A) Neno la Mungu li Hai
B) Neno la Mungu lina nguvu (Mwanzo 1:6).
C) Neno la Mungu lina ukali kuliko upanga
D) Neno la Mungu linachoma hata kuzigawanya nafsi, roho viungo na mafuta yaliyomo ndani yake
E) Neno la Mungu li jepesi kuyatambua mawazo na makusudi ya moyo.
Kwa Nini Neno la Mungu li Hai?
Neno la Mungu li hai kwa sababu Mungu mwenyewe analithibitisha kwamba li hai maana
a) Linafanya mabadiliko (Isaya 55:10-11).
b) Linatupa kushinda dhambi (Zaburi 119:11).
c) Neno la Mungu li hai kwa sababu linatupa mafanikio katik mwili.
Petro anasema ”kwa neno lako tunatupa nyavu zetu.“ Hapa tunaona kuwa
Neno la Mungu pekee yake ndilo linaloweza kuleta majibu katika maisha
yetu (Luka 5:3-6).
Uhai wa Neno la Mungu kwa mtu ndio unaoleta kushinda dhambi. Nao wakamshinda kwa neno la ushuhuda wao (Ufunuo 12:11).
Daudi aligundua au kwa maneno mengine alifahamu umuhimu wa neno la
Mungu katika maisha, kama vile mtume Paulo anavyosema na Wakolosai kwa
habari ya neno la Kristo kwamba likae kwa wingi ndani ya mioyo yetu.
Neno la Mungu lina nguvu na ndio maana tunamshinda shetani kwa neno la Mungu. Yesu kama kielelezo yeye mwenyewe ni neno ndani ya neno anamshinda shetani (Luka 4:1-12).
Katika mistari hiyo tunaona Yesu anamwambia shetani ”imeandikwa“
Shetani nae anageuza usemi nae anamwambia Yesu ”imeandikwa kwamba
atakuagizia malaika usije ukajikwaa mguu wako.“ Kwa kuwaYesu neno la
Mungu limo ndani yake hamwambii tena shetani imeandikwa ila anamwambia
imenenwa.
Kwa maneno mengine tukiwa na neno la Yesu ndani yetu hatuwezi
kuyumbishwa. Kwanini? Kwa sababu tumeshaona jinsi ambavyo shetani
anajaribu kutumia neno la Mungu kwa kusema ”imeandikwa.“ Na ni kweli
imeandikwa ananukuu kutoka kitabu cha Zaburi 91 :1-12.
Hata kama shetani
ananukuu maandiko haina sababu yamimi kushindwa na shetani maana Yesu
tayari alikwisha mshinda. Yesu kumshinda shetani ina nipelekea mimi
kusoma neno la Mungu kwa bidii sana. Kwa mfano, ni kweli kabisa
imeandikwa mtakula vitu vya kufisha havitawadhuru lakini je, ninywe sumu
sitakufa kwa sababu imeandikwa? Hapana, ukinywa hakika utakufa. Shetani
hutumia mandiko kuwafunga wasiojua neno la KristoYesu.
Katika Biblia tunasoma pia kwamba ”imeandikwa“ Wanandoa MKE na MUME
wasinyimane. Kwa kutojua neno vijana wa kiume na wa kike wamedanganywa.
Si hao tu hata walioko kwenye ndoa wametegwa kwa andiko hilo. Neno
linasema katika Mithali 6:32 ”Aziniye na
mwanamke hana akili kabisa“ na Mwanamke vivyo hivyo akizini na mwanaume
hana akili kabisa. Watu wamepata hasara ya mambo mengi kwa kutojua neno
la Mungu. Ili tuweze kumshinda shetani ni lazima neno la Yesu liwe
ndani yetu ndiposa tutamshinda shetani. Ayubu kwa neno la Mungu
alishinda. (Ayubu 19:25-27, Waefeso 6:17).
Nataka nikwambie neno la Mungu ni msaada katika maisha yetu maana hutupa majibu ya maisha yetu. Katika Luka 5:3-6
tunasoma jinsi Petro na wenzake walivyopata samaki wengi kwa kutii neno
la Kristo. Kumbuka pia juu ya yule akida, alimwambia Yesu ”...sema neno
tu na mtumwa wangu atapona“ (Luka 7:2-10). Yesu akisema neno lazima mabadiliko yatokee.
Neno la Mungu lina ukali kuliko upanga.
Kwa nini neno la Mungu lina ukali kuliko upanga? Upanga unaweza
kukukata na usipone. Lakini neno linakata na kuponya. Kwa neno hili
wafalme wanatubu. Yona alitumia neno la Mungu likawa kali watu wakatubu.
(Yona 3:1-10; Matendo ya Mitume 8:18-24).
Neno la Mungu linachoma hata kuzigawa nafsi na roho na viungo na mafuta yaliyomo ndani yake (Matendo 7:51-54, Yohana 4:16 -18, 27-29). Mwanamke akaambiwa mambo yake; Neno likachambua kila tabia.
Neno la Mungu li jepesi kutambua mawazo na makusudi ya moyo.
Yesu kama Neno la Mungu anajua mambo ambayo watu wanawaza ndani ya mioyo yao (Luka 5:17-24, 6:6-8 ; Mathayo 16:1-4). Yapo
makusudi ya moyo ambayo ni ya siri sana kwa mwanadamu lakini nataka
nikuambie neno la Mungu ni jepesi kutambua makusudi ya moyo.
Mtume Petro aliyependa kujua neno la Mungu, naye pia Mungu alimjalia neema ya kuyajua makusudi ya moyo wa mwanadamu (Matendo 5:1-11). Elisha aliyajua makusudi ya moyo wa mfalme ya kuwatenda Israeli kwa siri ila Mungu alimpa neema ya kuyajua mawazo ya mfalme (2 Wafalme 6:8-12).
Hili ni jambo la msingi katika maisha ya Mkristo yaani kulijua neno
la Mungu. Neno la Mungu tukiwa nalo na likitenda kazi ndani yetu lazima
tufanikiwe (Yoshua 1:8)
Je unahitaji kuwa na imani katika neno la Mungu? Basi, ni neno la
Mungu peke yake ambalo laweza kuumba imani, maana pasipo neno la Mungu
hakuna imani (Waebrania 11:3 ; Warumi10:17). Ili uwe mwanafunzi wa Yesu ni lazima ulijue neno la Mungu na kulishika.(Yohana 8:31 ; Luka 2:19).
Kama neno halimo ndani yetu tunayoyafanya yanakuwa hayana Mungu, hata
twaweza kusalitiana. Mtu anayelitamani neno la Yesu huling’ang’ania na
kulitenda maana kwake ni nguvu. (1Wakorintho 1:18). Si kwamba Neno la Mungu ni nguvu tu: bali huleta faida (Mathayo 13:23). Watu wengi tunapotea kwa kutokujua uwezo (nguvu) iliyomo katika neno la Mungu (Mathayo 22:29).
Yesu anasema, mtu anayelitenda neno la Mungu na kulishika huyo
amepanda mbegu ambayo itazaa sana, maana ndani ya moyo wake imo mbegu
ambayo ni neno la Mungu la uponyaji na mafanikio, msamaha, utu wema na
mengi yanayofanana na hayo.
Yapaswa maisha yetu yawe yenye neno (mbegu) la Mungu ili tuweze kuzaa mambo mazuri.
Wokovu wetu unaimarika kwenye neno la Mungu. Hilo neno la Mungu tunalipata wapi? Isaya 34:16. Upo umuhimu wa kuyachunguza maandiko ili kujua Mungu anasema nini (Matendo 17.10-11). Je, tangu ulipowekwa msingi wa wokovu, neno limo ndani? (Hagai 2:18-19). Kila kitu kinaweza kupita lakini sio neno la Mungu (Isaya 40:8, Mathayo 24:35).
Ili neno litende kazi katika kinywa chako unapolitamka na kuamini ni
lazima iwepo nguvu ya Roho Mtakatifu. Bila hii nguvu hamna kitakacho
endelea. Utasema umeamini lakini hakutakuwa na matokeo. Mungu mwenyewe
alipotamka neno liliambatana na nguvu ya Roho Mtakatifu (Mwanzo1:2-3).
Imeandikwa na Mwinjilisti Simon Mkanza
0784 475622, 0786 477021