Advertise Here

Monday, September 30, 2013

Safu ya James Kalekwa: Umejenga Juu ya Mwamba au Mchanga? - Part II

James Kalekwa
Somo linaendelea....

Kusoma sehemu ya Kwanza, Bofya Hapa

Mwamba 1: Tawala nafsi yako kwa kuongoza milango yako ya fahamu.

Mithali 4:23
"Linda sana moyo wako kuliko yote uyalindayo; Maana ndiko zitokako chemchemi za uzima."

Ili uweze kusaidika juu ya habari ya nafsi ni muhimu sana kutambua na kukumbuka siku zote mwanadamu ni nani, wewe ni nani au ni kiumbe wa namna gani.  Wewe ni roho yenye nafsi inayoishi ndani ya mwili. Rejea kitabu cha Mwanzo 2:7, " BWANA Mungu akamfanya mtu kwa mavumbi ya ardhi, akampulizia puani pumzi ya uhai; mtu akawa nafsi hai." Ambapo  utaona mwanadamu ni muunganiko wa mavumbi ya ardhi, pumzi ya uhai na nafsi hai… Kwa msingi huo basi mavumbi ndiyo mwili, pumzi ya uhai ni roho na nafsi hai ni nafsi!

Ukienda ndani ya neno la Mungu utakuta lile eneo la nafsi linazungumziwa kwa lugha au tafsiri tofauti tofauti kwa maana ileile. Kuna nyakati Biblia inatumia neno “moyo”, “nafsi”, “ufahamu”, “roho” kuelezea eneo moja tu la mwanadamu nalo ni nafsi. Kwasababu hiyo nakuomba ufungue macho yako kuyatazama maandiko kwa maana pana zaidi. Hebu tazama mstari huo kwa tafsiri za kiingereza: “Guard your heart above all else for it determines the course of your life." (NLT)

"Linda moyo wako zaidi ya vitu vyote kwasababu moyo wako ndiyo huamua mwenendo/mtiririko wa maisha yako."

"keep your heart with all diligence, for out of it springs out the issues of life." (KJV)

"Linda moyo wako kwa umakini mkubwa sana ,kwasababu moyo wako hububujisha mambo yahusianayo na maisha."

Kimsingi tafsiri zote zinatuelekeza kwenye uelewa kwamba maisha ya mwanadamu huamuliwa na moyo wake, mwenendo/mtiririko wa maisha hujengwa ndani ya moyo, chemchemi/chanzo cha maisha ya mwanadamu ni moyo! Natamani uone kwa ukubwa ambao mwandishi wa Mithali anaukusudia uuone… Ya kwamba chochote kinachotokea kwenye maisha yako, kimetokea moyoni mwako. Yaani kama moyo wako ni kiwanda na maisha yako ni bidhaa itokayo ndani ya kiwanda hicho na kwa uelewa huo basi, ni dhahiri ya kwamba kama hupendi bidhaa fulani usikurupuke kuiangamiza bidhaa hiyo kwasababu utakuwa umetatua tatizo kwa muda (immediate solution), bali unapaswa kudhibiti uzalishaji unaofanywa kiwandani. Au kama hupendi mazao yaliyomo gharani mwako, tafadhali usiyachome mazao hayo kwasababu utakuwa unatatua kwa muda, bali chukua hatua ya kudhibiti shughuli za shamba… Mungu akusaidie sana uelewe hapa!

Kwakuwa moyo ni sehemu muhimu kiasi hiki, basi tunapaswa kujua bayana na kwa uhakika tunaposema moyo tunamaanisha nini hasa ili tusijikute tunazungumza mambo tusiyoyajua “vague”… 

Ukishauelewa moyo basi umepata mtaji wa ushindi! Kila mara ninapozungumza na vijana wenzangu huwa napenda kuwapa tahadhari ya kwamba moyo wa mwanadamu, huu unaozungumwa hapa si ule wa kwenye masomo ya sayansi hasa somo la Baiolojia…. 

Ninachofundisha hapa ni zaidi ya ule moyo wenye kazi ya kusambaza damu mwilini, kwasababu moyo usambazao damu umeumbwa kwa damu na nyama, yaani huo ni sehemu ya mwili na kwa uelewa nilioujenga kwako ni kwamba mwili ni mavumbi ya ardhi. Si kazi ngumu sana kung’amua kwamba moyo usambazao damu mwilini nao ni nyama (ni mwili) kwasababu baada ya roho kutoka, mtu kufariki, mavumbi (mwili) hurudi mavumbini… na moyo huo wa kwenye somo la Baiolojia huwa sehemu ya virudivyo mavumbini.

Kwahiyo kwa kutazama kuwa mwanadamu ni roho yenye nafsi inayoishi ndani ya mwili….uwe na uhakika Biblia inaposema "moyo"  katika andiko hili haimaanishi moyo wa nyama na haimaanishi roho bali inamaanisha nafsi. Kwahiyo unapojifunza katika eneo hili naomba ubebe mtazamo wa nafsi ili uelewe vizuri zaidi.

Neno la Mungu linatanabaisha kuwa  moyo/nafsi ndiyo huamua mwenendo wa maisha yetu na hububujisha mambo yahusianayo na maisha yetu kwa tafsiri nyepesi ni kwamba jinsi ulivyo ndivyo ulivyoamua kuwa; na uamuzi huo umefanyika ndani ya nafsi yako Mithali 23:7a,"Maana aonavyo nafsini mwake ndivyo alivyo." Hakuna mtu anapaswa kulaumiwa bali ndivyo ulivyoamua.Basi kama nafsi ni sehemu ya muhimu kiasi hicho, tunawajibu mkubwa sana kulinda sana nafsi zetu.

Hebu tuitazamae nafsi kwa mfano wa hazina…. Naomba uyaelekeze mawazo yako kwenye maisha ya kawaida kabisa, maisha ya kila siku. Ninaamini kwamba umeshawahi kusikia ama wewe au mtu anayekuhusu ni mtumiaji wa huduma za kifedha kwa njia ya simu ya mkononi. Kwa hapa Tanzania kuna huduma ya M-Pesa, Z Pesa, Airtel Money na Tigo Pesa…

Kwa mfano huo basi, hebu mfikirie mtu ambaye hufunga safari kwenda kutoa pesa (kwa mtoa huduma) wakati anajua fika ya kwamba hana akiba/salio kwenye akaunti yake. Huyo ni sawa na mkulima ambaye wakati wa msimu wa mavuno unapofika yeye hufunga safari kwenda shambani ili akaanze shughuli ya kuvuna wakati anafahamu wazi ya kwamba hakuna siku ambayo aliwahi kuweka mbengu ndani ya shamba hilo… Inawezekanaje kuvuna wakati hujapanda? Kwa lugha ya kiingereza wanasema “you can not give what you do not have.”.

Ni ukosefu wa akili timamu ndiyo utamwongoza mtu kwenda kutoa pesa kwenye akaunti ambayo haina pesa (na muhusika hajawahi kuongeza pesa); ni upumbavu kwenda kuvuna kwenye shamba ambalo hujawahi kupanda mbegu yoyote.

Nimetumia mifano hiyo kukuleta kwenye dhana moja ya Muhimu sana ya kwamba kabla ya kutoa pesa kwenye akaunti unapaswa kuweka pesa; kabla ya kuvuna unapaswa kupanda mbegu. Kama basi inaonekana ni hekima kwa mkulima na mtumiaji wa huduma za pesa kwenye simu ya mkononi… ni hekima zaidi kwa mtumiaji wa moyo, mtumiaji wa nafsi ambaye ni wewe. Kabla hujavuna au hujatoa chochote kutoka kwenye nafsi yako, ni wajibu wako kuweka kitu.

Somo litaendelea Jumatatu Ijayo....

Mafundisho haya yameandaliwa na James Kalekwa
Mwanataaluma, Mwandishi wa vitabu, na Mwalimu wa Neno la Mungu
+255 714 762 669
+255 754 917 764
jameskalekwa@gmail.com

Sunday, September 29, 2013

Ibada ya Kusifu na Kuabudu katika Kanisa la New Vine Christian Centre.

Kanisa la New Vine Christian Centre lililopo Nyegezi, Mwanza linakukaribisha katika Ibada Maalum ya Kusifu na Kuabudu Itakayofanyika Kanisani hapo Siku ya Jumapili ya October 6, 2013 Kuanzia Saa 8:00 Mchana.

Tshirts za Event hii zinapatika kwa Rangi Mbalimbali na Size Mbalimbali. Kama unahitaji Tshirt, Piga Simu Namba: 0712 113305 na 0754 030789.

- Wote Mnakaribishwa -

Wednesday, September 25, 2013

Mwl. Christopher Mwakasege: Zijue Karama Za Roho Mtakatifu – II.

Mwl. Christopher Mwakasege

SEHEMU YA NNE Karama ya neno la Maarifa
I Wakorintho 12:4,8; ”Basi pana tofauti za karama bali Roho ni yeye yule. Maana mtu mmoja kwa Roho apewa neno la hekima, na mwingine neno la maarifa, apendavyo Roho yeye yule”.
 

Kama tulivyo jifunza huko nyuma kazi ya karama ni kulijenga kanisa.
Kazi ya karama ya neno la maarifa.

 Kukupa habari ya mambo yaliyopo na/au yaliyopita ili kukurahisishia kufanya maamuzi na kutambua hila zilizojificha ili kukwamisha utumishi wako.

Wakati mwingine karama hii itakupa kujua maswali waliyonayo watu kabla hawajauliza au kujua mahitaji waliyonayo kabla hawajakwambia.
 

Njia nne ambazo karama ya neno la maarifa inafanya kazi:
i. kwa kutumia mawazo
ii. kwa kutumia ndoto
iii. kwa kutumia maono, maono yamegawanyika katika sehemu zifatazo:

 maono ya ndani

 maono ya wazi

 maono yanayotokea wakati akili zako hazina matunda.(suspended)
iv.  kwa kutumia njia ya kuweka mwilini mwako maumivu au hali aliyo nayo mtu mwenye kuhitaji.

Karama zinafanya kazi kwa kutegemeana/kushirikiana.
Mfano. Unaweza kupewa swali na jibu. Kulijua swali ni neno la maarifa na kujua jibu la swali hilo ni neno la hekima.

i. Njia ya kutumia MAWAZO / WAZO
Hii ndio njia kuu ambayo inatumika mara nyingi zaidi. Marko 2:6-8 inasema ”……. Mara (ghafla) Yesu akafahamu rohoni mwake kwamba wanafikiri hivyo nafsini mwao…..”. Maana yake ghafla wazo tofauti, na lile alilokuwa akiwaza saa hiyo lililetwa na Roho Mtakatifu ndani yake.


Ukisoma Luka 3:15-16; inasema ”……….Yohana alijibu akawaambia wote,…………”. Yaani alijibu swali ambalo lililetwa ndani yake na Roho Mtakatifu; sio kwamba aliulizwa na mtu yeyote yule.

Luka 20:18-26; inasema ”……….wakamvizia-vizia, wakatuma wapelelezi waliojifanya kuwa watu wa haki, ili wamnase katika maneno yake, wapate kumtia katika enzi na mamlaka ya liwali. Wakamwuliza wakisema,………………. Lakini yeye alitambua hila yao akawaambia ……………. Wakastaajabia majibu yake, wakanyamaa”.

Mambo ya kukuwezesha kufanya kazi na njia hii ya mawazo:
a. Jizoeze kukabidhi roho yako, nafsi yako na mwili wako kila siku upya mbele za Mungu.
b. Omba maombi ya vitu vifuatavyo:

 Usikivu (sensitivity)

 Utulivu

 Kufundishwa na Mungu namna ya kutembea katika hiyo karama.
Hii inasaidia kwa mfano, Mungu akisema jenga safina wakati sio msimu wa mvua. Yaani kutii sauti ya Mungu bila kuangalia dalili za nje.

SEHEMU YA TANO
Karama ya neno la hekima
I Wakorintho 12:4,8; inasema ” Basi pana tofauti za karama bali Roho ni yeye yule. Maana mtu mmoja kwa Roho apewa neno la hekima…….”.

I Wakorintho 14:12 ” ……takeni sana mzidi kuwa nazo ili kulijenga kanisa”.

Karama ya neno la maarifa na neno la hekima zinafanya kazi kwa karibu sana.

Kazi ya karama ya neno la hekima na inavyofanya kazi:
1. kukupa jibu la swali unaloulizwa lakini hasa swali lenye hila, mtego, ushindani au mashtaka ndani yake.

Luka 21:12-15 inasema ”lakini, kabla hayo yote hayajatokea watawakamata na kuwaudhi; watawapeleka mbele ya masinagogi…….. basi kusudieni mioyoni mwenu, kutofikiri-fikiri kwanza, mtakavyojibu, kwa sababu mimi nitawapa kinywa na hekima ambayo watesi wenu wote hawataweza kushindana nayo wala kuipinga”.

Luka 20:19-26; ”…lakini yeye alitambua hila yao …..”
Marko 3:1-6; inasema ”……….akamwambia yule mtu mwenye mkono uliopooza simama katikati ……….nyosha mkono wako. Naye akaunyosha mkono wake ukawa mzima tena”.
Hapa tunaona neno la maarifa (kutambua hila ya wale waliotaka kumkamata) ilianza kufanya kazi, neno la hekima pia likafanya kazi baadaye pale Yesu alipomwambia yule mwenye kupooza ”simama katikati” na tunasoma akaanza kuzungumza na wale watu.

2. inakupa uwezo wa kutatua tatizo lililoko mbele yako.
Mathayo sura ya 1 na ya 2: Habari ya Yusufu na Mariamu. Katika sura hizi karama ya neno la maarifa na la hekima ilifanya kazi kwa kutumia ndoto. Si ndoto zote zinatoka kwa Mungu lakini kama ukiwa na neno la Mungu utatambua ndoto ya Mungu na isiyo ya Mungu.

3. kukupa uhuru wa kushirikiana na watu usiowajua kwa kazi ya Mungu.

Matendo ya mitume 10:1-20; Habari za Petro na Kornelio. Habari hii inaeleza jinsi Petro alivyoona maono wakati amezimia roho (akili zake zilikuwa hazina matunda).

Maono ya aina nyingine, kama tulivyokwishaona hapo nyuma ni ya wazi, ambapo akili zako zinaona na zinaelewa na bado unaweza kuona katika ulimwengu wa roho.

Aina nyingine ni maono ya ndani kwa mfano: unapoomba halafu ghafla ndani yako inakuja picha.

Sasa karama ya neno la maarifa na la hekima itakusaidia kukuwezesha kushirikiana na watu usiowajua.

4. inakurahisishia kuamua kwa haki katika nafasi ya uongozi Mungu aliyokupa au mahali unapohitajika kutoa maamuzi
I Wafalme 3:4-28; habari za mfalme Sulemani, jinsi alivyoomba hekima kwa Mungu na akapewa. Vilevile tunaona jinsi ambavyo aliweza kutoa uamuzi wa haki juu ya kesi ya wanawake wawili waliokuwa wakigombea mtoto. Uamuzi wa haki unahitaji msaada wa Mungu.

SEHEMU YA SITA
Karama ya unabii
I Wakorintho 12:4,10 ”Basi pana tofauti za karama bali Roho ni yeye yule. na mwingine matendo ya miujiza; na mwingine unabii, na mwingine kupambanua roho; mwingine aina za lugha; na mwingine tafsiri za lugha.
 

I Wakorintho 14:12; inasema ”…….takeni kwamba mzidi sana kuwa nazo ili kulijenga kanisa”.
 

Mambo ya msingi kuhusu huduma ya Nabii na karama ya unabii:-
1. kuna tofauti kati ya huduma ya nabii na karama ya unabii.
Efeso 4:11 ”Naye alitoa wengine kuwa Mitume; na wengine kuwa manabii….”. Hapa anazungumza habari ya nabii (ofisi) ya nabii. Huduma ni ofisi na karama ni vitendea kazi katika ofisi.
Kazi za nabii (kama huduma)

kufundisha mafundisho ya msingi / ya kuweka msingi wa kiroho ndani yako. Efeso 2:19-20 inasema, ”Basi tangu sasa ninyi si wageni wala wapitaji, ……..mmejengwa juu ya msingi wa mitume na manabii, naye Kristo Yesu mwenyewe ni jiwe kuu la pembeni”. Hii haimaanishi kwamba kila nabii amepewa kufundisha.

 Nabii pia anaweza kupewa kufanya kazi ya kubomoa na kuharibu kazi za shetani na kupanda pando la Mungu ndani ya mioyo ya watu, kama kuna mahali panahitajika kufanya hivyo. Tunaweza kusoma haya katika kitabu cha Yeremia 1:4,5,10; inasema ” …..kabla sijakuumba katika tumbo nalikujua, na kabla hujatoka tumboni, nalikutakasa; nimekuweka kuwa nabii wa mataifa …………. Ili kung’oa na kubomoa na kuharibu na kuangamiza; ili kujenga na kupanda”.

Kazi nyingine ni kuonya. Tunaweza kuona haya katika kitabu cha Ezekieli 2:3-5; ”akaniambia mwanadamu, nakutuma kwa wana wa Israel, kwa mataifa wanaoasi, walioniasi mimi wao na baba zao wamekosa juu yangu…..”

Kazi nyingine ni mwonaji. I Samweli 9:9 ”(Hapo zamani katika Israel, mtu alipokwenda kuuliza neno kwa Mungu, husema hivi, Haya! Twende kwa mwonaji; maana mtu aitwaye sasa Nabii hapo zamani aliitwa mwonaji)”.

 Kutabiri (kusema mambo yajayo). Yeremia 23:21; inasema ”mimi sikuwatuma manabii hao, lakini walikwenda mbio; sikusema nao, lakini walitabiri.

Kazi ya karama ya unabii. (kama kitendea kazi):
Ni kujenga, kufariji, kutia moyo na kujirunza, pia huthibitisha kile ambacho Mungu amekwisha kusema na wewe. Katika kitabu cha I Wakorintho 14:3,4,24,25,31; tunasoma ”Bali yeye ahutubuye, asema na watu maneno ya kuwajenga, na kuwafariji, na kuwatia moyo. Yeye anenaye kwa lugha hujijenga nafsi yake; bali ahutubuye hulijenga kanisa. Lakini wote wakihutubu, kisha akaingia mtu asiyeamini, au mjinga, abainishwa na wote, ahukumiwa na wote; siri za moyo wake huwa wazi, na hivyo atamwabudu Mungu, akianguka kifudi-fudi, na kukiri ya kuwa Mungu yu kati yenu bila shaka. Kwa maana ninyi nyote mwaweza kuhutubu mmoja mmoja, ili wote wapate kujifunza, na wote wafarijiwe”.
2. manabii wapo hata leo ila nafasi zao ni tofauti na za wale wa agano la kale.

Efeso 4:11,14; ”naye alitoa wengine kuwa mitume na wengine kuwa manabii; na wengine kuwa wainjilisti na wengine kuwa wachungaji na waalimu; kwa kusudi la kuwakamisisha watakatifu; hata kazi ya huduma itendeke hata mwili wa Kristo ujengwe; hata na sisi sote tutakapoufikia umoja wa Imani na kumfahamu sana mwana wa Mungu, hata kuwa mtu mkamilifu…………. Ili tusiwe tena watoto wachanga, tukitupwa huku na huku na kuchukuliwa na kila upepo wa elimu, kwa hila ya watu, kwa ujanja tukizifuata njia za udanganyifu”.
Pia katika kitabu cha Matendo ya Mitume 13:1; tunasoma ”……. Palikuwako manabii na waalimu …..”. hii inaonyesha kuwa manabii wapo hata leo.

Tofauti iko hivi: kwamba manabii hapo zamani (katika agano la kale) walikuwa viongozi wakiongoza watu, yaani walipewa kuongoza watu, lakini katika agano jipya huduma ya nabii ipo ndani ya Kanisa na nabii hakupewa kuongoza kanisa- kila mmoja wakati huu amepewa Roho Mtakatifu ambaye anamwongoza. Hivyo nabii anayesema kwa mausia ya Mungu ni yule anayesema sawasawa na neno la Mungu.
Kanisa linajengwa juu ya misingi miwili ambayo ni:
a. Yesu Kristo


b. Mafundisho ya mitume na manabii ambao wanafundisha mafundisho ya msingi ambayo yanamfanya mtu awe mkristo. (foundation series). Ukisoma kitabu cha Waebrania 6:1; inasema ”kwa sababu hiyo, tukiacha kuyanena mafundishao ya kwanza ya Kristo; tukaze mwendo ili tuufikilie utimilifu; tusiweke msingi tena wa kuzitubia kazi zisizo na uhai, na wa kuwa na Imani kwa Mungu na wa mafundisho ya mabatizo, na kuwekea mikono, na kufufuliwa wafu na hukumu ya milele”.

Manabii wa sasa wanatofauti na akina Paulo na akina Petro ambapo hao wa zamani walipewa mafundisho ya msingi na hawa wa sasa wanapewa wito (hekima au special revelation) wanaposoma Biblia wanafungua siri za mafundisho ya msingi, ambayo akina Paulo walifundisha, na kutufunulia sisi.

- Mwisho -

Tuesday, September 24, 2013

Safu ya James Kalekwa: Umejenga Juu ya Mwamba au Mchanga?



James Kalekwa

Utangulizi wa somo:

Mathayo 7:24-27
“Basi kila asikiaye hayo maneno yangu, na kuyafanya, atafananishwa na mtu mwenye akili, aliyejenga nyumba yake juu ya mwamba; mvua ikanyesha, mafuriko yakaja, pepo zikavuma, zikaipiga nyumba ile, isianguke; kwa maana misingi yake imewekwa juu ya mwamba. Na kila asikiaye hayo maneno yangu asiyafanye, atafananishwa na mtu mpumbavu, aliyejenga nyumba yake juu ya mchanga; mvua ikanyesha, afuriko yakaja, pepo zikavuma, zikaipiga nyumba ile, ikaanguka; nalo anguko lake likawa kubwa.”

Kwa muda mrefu nimekuwa nikizunguka sehemu mbalimbali, makanisani na mikusanyiko, nikifundisha na kuwezesha semina, makongamano ndani ya nchi ya Tanzania. Moja ya msisitizo wangu ni kwamba wokovu si dini, wokovu si tamaduni au mapokeo (tradition).

Hii ni baada ya uchunguzi wangu wa kina na mapito kwenye maisha yangu binafsi ambapo niligundua ya kwamba kuna uelewa tofauti sana miongoni mwa watu juu ya wokovu (hata miongoni mwa watu waliookoka). Uelewa wako juu ya jambo fulani, ndiyo huamua kiwango cha maisha yako juu ya jambo hilo… Kama una uelewa mdogo, uelewa potofu, uelewa finyu… Ndivyo kiwango cha maisha yako kitakavyokuwa… “Your attitude determines your altitude.”

Kama unataka kutambua uelewa wa mtu binafsi kuhusu wokovu, tazama maisha yake ndani ya wokovu au sikiliza msimamo wake kuhusiana na wokovu… Ukikuta ni maisha ya dini, mapokeo/tamaduni… Basi tambua huo ndiyo uelewa wake. Kama asemavyo mfalme Sulemani “Maana aonavyo mtu nafsini mwake, ndivyo alivyo.”

Pia, kuna watu ambao bado hawajaokoka na hawataki kuokoka kwasababu bado hawajapewa taarifa sahihi kuhusu wokovu. Hii inamaanisha ya kwamba uelewa wao juu ya wokovu, umeyaathiri maisha yao. Laiti kama angetokea mtu wa kuwasikilizisha habari njema, basi uelewa wao ungebadilika na kisha wangeuelekea wokovu – Mungu atusaidie tuwasikilizishe wengine taarifa sahihi kuhusu wokovu.

Naamini unaelewa kuna taasisi au makusanyiko ya watu ambao wanajitahidi kujimilikisha wokovu kuwa ni mali yao binafsi yaani kama wewe si mshiriki au mmoja wa wanachama wao basi ni dhahiri kwamba wewe hujaokoka – hujapata wokovu! Wao huamini hakuna mtu mwingine aliyeokoka isipokuwa aliye ndani ya taasisi au makusanyiko yao…  Pia upande wa pili vivyo hivyo kuna wale ambao wamekuwa na juhudi nyingi sana kuukataa wokovu… kwa wao wokovu si dini yao, wokovu si utamaduni wao...

Kwa mtazamo wao, kuokoka ni kujifuta ushirika katika taasisi au makusanyiko yao. Pande zote hizi mbili, wanaoumiliki na wanaoukataa wokovu, wote wapo katika tatizo moja: tatizo la uelewa juu ya wokovu!

Ni heshima kubwa sana mbele za Mungu na mbele zako kwamba ninakukaribisha kujifunza ili kuulekeza uelewa wako juu wokovu. Karibu na uwajulishe na wengine juu ya mafundisho haya! Karibu na Mungu wa amani, Yesu Krsito aliye asili ya wokovu, akufungue macho yako ya ndani upate kuelewa mafundisho haya. 

Tujenge uelewa wa pamoja
 Naomba nikurejeshe kwenye andiko nililoanza nalo hapo awali:

Mathayo 7:24-27
“Basi kila asikiaye hayo maneno yangu, na kuyafanya, atafananishwa na mtu mwenye akili, aliyejenga nyumba yake juu ya mwamba; mvua ikanyesha, mafuriko yakaja, pepo zikavuma, zikaipiga nyumba ile, isianguke; kwa maana misingi yake imewekwa juu ya mwamba. Na kila asikiaye hayo maneno yangu asiyafanye, atafananishwa na mtu mpumbavu, aliyejenga nyumba yake juu ya mchanga; mvua ikanyesha, afuriko yakaja, pepo zikavuma, zikaipiga nyumba ile, ikaanguka; nalo anguko lake likawa kubwa.”

Ili kuweza kutembea pamoja katika mfululizo wa mafundisho haya, ni vyema tukajenga uelewa wa pamoja juu ya andiko hilo amabalo ndilo msingi wa mafundisho haya. Bwana Yesu Kristo anazungumza juu ya wajenzi wa aina mbili, mjenzi mwenye busara na mjenzi mpumbavu. Ukitazama kwa umakini kwenye maandiko hayo utagundua ya kwamba maisha ya wajenzi hawa waiwili twaweza kuyafupisha hivi:



Mambo waliyofanana
Mambo waliyotofautiana

Mwenye akili
Mtu mpumbavu
1.        Wote walifanya shughuli ya ujenzi wa nyumba
*      Alijenga nyumba juu ya Imwamba
*I      Alijenga nyumba kwenye mchanga
2.       Wote walipata misukosuko inayofanana kwenye nyumba zao.
*      Nyumba yake haikuanguka
*      Nyumba yake ilianguka
 
Kilichoamua tofauti ya hawa ndugu ni kitu kimoja tu, nacho ni mahali walipochagua kujenga nyumba zao- mmoja alijenga kwenye mwamba na mwingine alijenga kwenye mchanga. Biblia imekaa kimya juu ya viwango vya ubora vya nyumba hizi, lakini imetueleza kwamba japo zilipitia misukosuko inayofanana lakini nyumba moja ilianguka na nyingike ilidumu (haikuanguka)…

Kwanini nyumba moja ianguke na nyingine isianguke wakati zote ni nyumba na zimepitia hali zinazofanana? Jibu ni rahisi sana, tofauti imeamuliwa na mahali nyumba zilipojengwa: kwenye mwamba na kwenye mchanga.

Naomba usisahau kwamba Bwana Yesu alitumia wajenzi kama mfano tu kuelezea dhana tofauti kabisa… Lengo lake lilikuwa ni ili kwamba watu waweze kujenga taswira (mental picture) ya anachokizungumza. Pia, ni hekima kama tukiirejea dhana ya Bwana Yesu huku tukiwa na taswira ya ndugu wajenzi ndani ya mawazo yetu.

Yesu anasema “mtu asikiaye maneno yangu, na kuyafanya, atafananishwa…” kisha anasema, “Na kila asikiaye hayo maneno yangu asiyafanye, atafananishwa…” Kwahiyo basi, dhana iliyo ndani ya moyo wa Bwana Yesu ni: kusikia maneno na kuyachukulia hatua (kuyatenda au kutoyatenda). 

Nitamanicho kiumbe ndani ya moyo wako na maisha yako ni kwamba ni wajibu wako kusikia neno na kulitenda kwasababu ni kwa njia hiyo tu ndiyo utafanana na mtu aliyejenga juu ya mwamba.

Kwakuwa sasa tumejenga uelewa wa pamoja, naomba uniruhusu nikuchukue kwenye mambo ya msingi (ambayo ni mwamba) yatakayokusaidia kuukulia wokovu… Kumbuka tunajenga wokovu wetu kwenye neno la Mungu na si mitazamo ya kidini, mapokeo au mifumo ya kimazoea. Ninaamini Mungu ana jambo kwaajili yako unapoendelea kufuatilia maswala haya ya msingi!

Somo litaendelea Jumatatu Ijayo....

Mafundisho haya yameandaliwa na James Kalekwa
Mwanataaluma, Mwandishi wa vitabu, na Mwalimu wa Neno la Mungu
+255 714 762 669
+255 754 917 764
jameskalekwa@gmail.com