Advertise Here

Wednesday, January 8, 2014

Kanisa la Moravian Mkoani Mbeya latoa Msaada kwa watoto yatima.

Kanisa la Moravian Tanzania Jimbo la Kusini Magharibi Ushirika wa Chunya Mjini, limetumia zaidi ya Sh6 milioni kwa ajili ya ununuzi wa vifaa vya shule kwa watoto 100 yatima na wanaoishi katika mazingira hatarishi.
 
Akikabidhi msaada huo jana mbele ya Mkuu wa Wilaya ya Chunya, Deodatus Kinawiro, Mchungaji wa Kanisa hilo Anyandwile Kajage alisema kuwa fedha hizo zilitumika kwa ajili ya ununuzi wa sare za shule, madaftari, viatu na chakula.

Kajage alisema kuwa lengo la kutoa msaada huo ni sehemu ya hamasa kwa watoto walio katika makundi hayo ili kuwajengea mazingira mazuri ya kuishi kwa amani na faraja.

Awali, Mkuu wa Wilaya ya Chunya Deodatus Kinawiro alipongeza jitihada za wadau na waumini katika kutoa misaada na kuitaka jamii kujitolea kwani kutoa ni moyo na siyo utajiri.

Alisema amefarijika kwa kiasi kikubwa kwa mwamko wa madhehebu ya dini kwa kutambua uhitaji wao kwa kukabiliana na janga la ongezeko la watoto wa mitaani na kuzitaka asasi nyingine za kiraia kuiga mfano huo.

Naye Mtoto Salome Zumbe alilishukuru kanisa hilo kwa kutoa msaada huo na kwamba utakuwa ni chachu na kichocheo cha wao kufanya vizuri katika mitihani yao na kuzingatia masomo ili kuweza kuendelea katika elimu ya ngazi za juu.

- Mwananchi -