Advertise Here

Tuesday, January 7, 2014

Safu ya James Kalekwa: Ongeza Maana/Thamani kwenye maisha yako kwa kuwa na malengo na kuyaelekea. - Part 1

James Kalekwa
Mithali 29:18, “Pasipo maono, watu huacha kujizuia…” 
Habakuki 2-3, “BWANA akanijibu, akasema, Iandike njozi ukaifanye iwe wazi sana katika vibao, ili kila aisomaye apate kuisoma kama maji. Maana njozi hii bado ni kwa wakati ulioamriwa, inafanya haraka ili kuufikilia mwisho wake, wala haitasema uongo; ijapokawia, ingoje; Kwakuwa haina budi kuja, haitakawia.”

Salamu za mwanzo wa Mwaka
 Ndugu msomaji na mfuatiliaji wa mafundisho yetu kwa njia ya mitandao, pokea salamu za heri ya mwaka mpya kwa jina la Yesu Kristo kutoka kwangu na mke wangu kipenzi, Frida. Tumekuwa na shauku sana kukushirikisha mafundisho haya na tumeomba sana kwaajili yako. Kiu iliyojaza mioyo yetu ni kuona unatembea na kuliishi kusudi la Mungu kwenye maisha yako binafsi, familia, jamii na kisha uweze kuepika (influence) taifa letu kwa ujumla.

Pia, tunaomba upatapo muda tafadhali omba kwaajili yetu tunapotekeleza wito tulioitiwa wa kuwakamilisha watakatifu kwa njia ya mafundisho. Mwaka huu tunataraji kuona wigo ukifunguka zaidi na mikoa na wilaya nyingi hapa kwetu
tutawafikia kwa mafundisho ya neno la Mungu. Kumbuka kuomba kiwemo chakula cha kutosha ghalani!

Sasa, nikukaribishe uungane nasi kwenye mfululizo huu mpya juu ya kuongeza thamani ya maisha yako kwa kuwa na malengo na kuyaelekea.

Lengo kuu la somo:
Kumuwezesha mtu binafsi kuwa na ufanisi na mwelekeo katika maisha ya siku kwa siku.

Malengo mahususi ya somo:
        i.            Kuelekeza kwa upana juu ya usuri (essence) wa maisha yenye malengo.
     ii.            Kujifunza kutoka kwenye maisha ya waliotutangulia juu ya malengo na kumahalisha (contextualize) mafunzo hayo.
   iii.            Kujenga stadi na mbinu za kuweka, kutekeleza na kutathmini malengo kwa mtu binafsi na vikundi.
   iv.            Kumuandaa mtu binafsi kwaajili ya kuwa chachu ya mabadiliko kwenye taifa.

Ni Muhimu sana ukatunza kumbukumbu ya malengo hayo ili uyapime na ujipime kulingana nayo wakati wote wa mfululizo huu.
Ndugu, imekuwa ni desturi miongoni mwa watu wengi sasa kila ifikapo mwanzo na/au mwisho wa mwaka au msimu fulani kuwasikia wakisema, wakielekeza na wakikumbushana juu ya kuwa na malengo kwenye maisha. Mijadala ya namna hiyo si maarufu sana katikati ya mwaka na wengi hawajisumbui kuyaelekea wala kutathmini hayo malengo – hilo ni tatizo kubwa. Nasi kwa neema ya Mungu, tumeiona ni vyema tuanze mwaka huu kwa kukukumbusha na kukuelekeza juu ya hilo, si kama desturi, kwa kuwa ni shauku yetu kuona unakuwa na kustawi… Karibu ujifunze, si kama desturi.

Hebu jiulize pamoja na mimi juu ya mambo haya:
Kisa mkasa (Scenario) #1. Msafiri asiyejua aendako:

Nimewahi kuzungumza mahali pengi na kwenye kitabu changu cha “Wokovu ni uhakika wa maisha ya Sasa na ya Baadaye.”  Juu ya mfano huu… Hebu jaribu kufikiri ukiwa katika stendi kubwa ya mabasi yaendayo katika mikoa mbalimbali (mfano stendi ya Ubungo- Dar Es Salaam, Nyegezi/Buzuruga- Mwanza, Msamvu- Morogoro n.k) Anatokea mtu mmoja ambaye kwa mwonekano wake ni msafiri… amebeba mabegi na mizigo kadhaa, mkononi ameshikilia chupa ya maji ya kunywa… akakujia kisha akakuuliza, “Ndugu, naomba unionyeshe basi kwani ninataka kusafiri.”

Je, utamuonyesha basi gani? Au utamuonyesha basi la kwenda wapi?...
Kwa kadiri nijuavyo mimi ni kwamba mtu mwenye akili timamu na nia njema, kama wewe ndugu msomaji wangu, utahitaji kupata maelezo kamilifu… utataka kujua kule anakoelekea yaani mwisho wa safari yake ili umwonyeshe basi linaloelekea mwisho huo.

Sasa iwapo ukimuuliza swali hilo kisha akakujibu kwamba “ndugu, sijui kule ninakokwenda.”  Je, utamuonyesha basi liendalo wapi? Au utamwonyesha basi gani? Huwa ninaamini na kushawishika kabisa ya kwamba wewe hutakuwa na kosa utakapomwonyesha basi lolote ili aende kokote kwasababu hajui kule aendako! Kwahiyo kokote atakapopelekwa ni sawa.

Somo litaendelea Jumatatu Ijayo.....

 Mafundisho haya yameandaliwa na James Kalekwa
Mwanataaluma, Mwandishi wa vitabu na Mwalimu wa Neno la Mungu
+255 714 762 669
+255 754 917 764