Advertise Here

Monday, January 27, 2014

Safu ya James Kalekwa: Ongeza Maana/Thamani kwenye maisha yako kwa kuwa na malengo na kuyaelekea. - Part 4

James Kalekwa
R  -(Realistic). Lengo zuri lazima liwe na uhalisia, ambao huja kutona  na kuangalia hali halisi ya pale ulipo, majukumu na nafasi yako. Mfano mzuri ni huo hapo juu kwenye sifa ya kufikika. Unapoweka malengo juu ya jambo fulani haimaanishi kwamba umeacha kufanya mambo mengine.

Unapoweka malengo ya kihuduma haimaanishi kuwa umeacha kuwa baba au mama (kama Mungu amekupa watoto) kwahiyo usijitoe kwenye wajibu mwingine uliopewa na Mungu, haimaanishi kwamba utastaafu kuwa mme au mke (ikiwa umeoa kama mimi au umeolewa), haimaanishi kwamba wewe si mtoto wa wazazi wako (ikiwa bado wa hai) kwahiyo unawajibu huo.

Lakini jambo jingine la msingi kufahamu, ni je, utapata muda wa kutathmini kazi yako au unaenda kienyeji kienyeji tu, Je, utapata muda wa kufuatilia mavuno hayo na kuyaombea au kuyalea (hakuna umuhimu wa kuzaa kama huwezi kulea), Je kuna mafundisho ya kutosha kwa watu hao? Lazima uzingatie kanuni ya kuwa mkweli juu ya nafsi yako?

Watoto wengine wa Mungu wamekwama sehemu si kwasababu hawana Yesu. Yesu wanae, Roho Mtakatifu yupo pamoja nao na wanaenda mbinguni lakini wamekwama sehemu kwasababu hawana maarifa juu ya jambo hilo. Mtumishi mmoja wa Mungu aliandika, "Upako unaletwa na maombi lakini maarifa ya neno huja kwa kusoma.

Maombi kamwe hayawezi kufuta ujinga na kukupa maarifa. Neno la Mungu limeweka bayana kuwa watu wanaangamizwa kwa kukosa maarifa Hosea 4:6. Ina maana upako siyo tiketi ya kukuzuia kuangamizwa kama huna maarifa ya neno la Mungu."



T  -(Time bound). Kitu cha kuzingatia katika kuweka malengo ni swala la muda, yaani tamati ya malengo husika. Hii itasakusaidia sana kupima mafanikio na kuweza kufanya tathmini juu ya maendeleo wakati wote wa utekelezaji wa malengo husika. Hebu fikiria nini kilimfanya Bwana Yesu aseme “…hali nimeimaliza kazi ile uliyonipa niifanye.", kwasababu malengo yake yalikuwa yamefungwa katika muda wa kuyakamilisha, alikuwa anaujua mwisho tangu mwanzo, kama ni msafiri basi alikuwa anajua stendi au kituo cha mwisho cha safari yake.

Hebu jiulize nini kinaweza kutokea kama malengo yako hayatakuwa na muda wa kuyaona yakitimilika, ”time of their realization.”?. Ngoja nikupe mfano wa kawaida sana ndipo utaelewa nini ninamaanisha, hebu fikiri pamoja na mimi itakuwaje kama mwanafunzi wa darasa la tano akibakia darasa hilo siku zote, bila kuhitimu wala kwenda darasa jingine, siku zote ni darasa la tano?

Ingefika wakati mwanafunzi huyu angechoka na masomo kwasababu hayana mwisho, lakini pia mzazi wake pia angechoka kulipia gharama za kitu kisicho na ukomo au utimilifu. Maana yangu hapa ni kwamba kinachomfanya mwanafunzi wa darasa la tano asome kwa bidii ni kwasababu kuna darasa la sita mbele na la saba yaani kuna kipindi cha kuhitimu hatua husika ya masomo la sivyo asingesoma kwa bidii.

Hebu fikiri nini kitatokea kama inatokea wanawake wanakuwa wajawazito siku zote, bila mwisho!!! Najua wengine wasingetamani kuwa na hali hiyo, kwasababu hakuna kuhitimu hali hiyo, yaani kujifungua.


Mfano wa lengo ambalo ni SMART: Kuihubiri injili kwa watu 1000 nchini Tanzania katika wilaya 4 kwa mwaka mmoja.


Je, lengo hilo ni hususani (Specific)? Ndiyo kwasababu limetaja idadi ya watu,idadi ya wilaya na nchi.

Je, lengo hilo Linapimika (Measurable)? Ndiyo kwasababu ya idadi, eneo la kijiografia (mahali) yaani mwisho wa siku unaweza kukaa chini na kuangalia kama wilaya 4 zimefikiwa na kwa kiasi gani, vilevile kuona kama watu 100 wamefikiwa.


Je, lengo hilo linafikika (Attainable)? Ndiyo, kwa Jiografia ya Tanzania inawezekana kuzifikia wilaya hizo kwa muda huo. Pia unaweza kupata muda wa kujiandaa, kifedha, kimaombi, ujumbe kwani mwalimu mzuri ni mwanafunzi wa kudumu, kwahiyo lazima ujifunze ili ukafundishe.


Je,lengo hilo linauhalisia  (Realistic)? Ndiyo, kwasababu muda unaruhusu kufanya mambo mengine kama maandalizi ya uwanja/ukumbi wa mikutano, mahali pa kufikia, watu wa kushirikiana nao (si unajua huwezi kushirikiana na watu wote na kwa upande mwingine huwezi kushirikiana na kila mtu?) n.k yaani kwa lugha ya kiingereza wanaita "logistics", pia unaweza kuwa na muda wa kutimiza wajibu wako mwingine kama baba/mama (mzazi), kama mme/mke, kama mtoto na vitu vya msingi kama hivyo lakini pia kuna jambo la muhimu ambalo watu wengi hulipuuzia,lakini ni la muhimu sana.

MAPUMZIKO! Mungu baada ya kutenda kazi siku sita alipumzika! Umuhimu wa kupumzika ni kwamba unaporudi tena kwenye utekelezaji, unakuja na nguvu mpya "fresh". Mungu akusaidie kuyaelewa haya na kuyatendea kazi na maisha yako hayatakuwa kama yalivyo, na hayo ndiyo maombi yangu kwa Mungu kwaajili yako msomaji wangu.

Somo litaendelea Jumatatu Ijayo.....

 Mafundisho haya yameandaliwa na James Kalekwa
Mwanataaluma, Mwandishi wa vitabu na Mwalimu wa Neno la Mungu
+255 714 762 669
+255 754 917 764