Advertise Here

Saturday, April 13, 2013

Namna ya Kuongeza Imani unapokuwa kwenye Jaribu.

2 
Mpenzi msomaji Shalom,

Biblia katika kitabu cha Mathayo 17:18 inasema‘..Ni kwa sababu ya upungufu wa imani yenu. Kwa maana amini nawaambia, Mkiwa na imani kiasi cha punje ya haradali mtauambia mlima huu, Ondoka hapa uende kule; nao utaondoka; wala halitakuwako neno lisilowezekana kwenu. Hii ni habari ya yule kijana aliyekuwa na pepo bubu na kiziwi, mzazi wake akamleta kwa wanafunzi wa Yesu wamwombee. Biblia inatueleza kwamba wanafunzi walijaribu kumtoa yule pepo wasiweze, wakati huo Yesu alikuwa amepanda Mlimani kwenda kuomba.
 
Yesu aliporudi alielezwa kilichotokea, akawakemea wanafunzi wake na kisha akamuombea yule kijana akapona. Baadaye wanafunzi wa Yesu wakamuuliza, kwa nini sisi hatukuweza kumtoa yule pepo. Ndipo Yesu akawajibu akasema ‘Ni kwa sababu ya upungufu wa imani yenu… Neno upungufu lina ya isiyo – tosheleza, yaani imani yao ilikuwa ina upungufu na kwa hiyo wasingeweza kumtoa yule pepo. Jambo ninalotaka tuliangalie ni kwamba kwa kuwa tatizo lilikuwa ni upungufu wa imani yao, ina maana walitakiwa kuongeza imani yao wakati wanaendelea kukemea. Sasa swali muhimu ni je wangeongezaje imani yao wakati wako kwenye jaribu/vitani?

Naam licha ya swali hili kuna maswali mengine ambayo ni muhimu kuyatafakari ili tuweze kuwa na ufahamu mzuri wa imani. Je upungufu huu wa imani kwa wanafunzi walikuwa nao kabla hawajaanza kukemea yule pepo au ulikuja wakati wanaendelea kuomba. Naam Yesu anatuonyesha kwamba kosa la hawa wandugu wenzetu lilikuwa upungufu wa imani yao?

Ni kwa namna gani walikuwa na upungufu wa imani?
Biblia katika Waebrania 11:1 inaeleza kwamba ‘imani ni kuwa na uhakika wa mambo yatarajiwayo ni bayana ya mambo yasiyoonekana’. Kwa hiyo endapo Yesu alisema ni kwa sababu ya upungufu wa imani yao ina maana ndani yao walipungukiwa uhakika wa kile walichokitarajia, ambacho ni kufunguliwa/kuponywa kwa kijana mwenye pepo. Naam upungufu wao wa imani ulitokana na  mashaka juu ya uhakika wa yule kijana kufunguliwa.

Nini kilipelekea wao kuingiza hofu/mashaka?
  • Kukosekana kwa dalili za kijana kufunguliwa – Ni imani yangu kwamba wanafunzi walipoanza kukemea walikuwa na uhakika kwamba Yule kijana atafunguliwa. Naam kadri walivyoendelea kuomba na kuona kwamba hakuna mabadiliko ya aina yoyote kwa mgonjwa yule ndipo hofu/mashaka yakawaingia mioyoni mwao. 
  • Maneno ya kusikia – Ikumbukwe kwamba chanzo cha imani yoyote ni kusikia (Warumi 10:17)?  Kumbuka wakati wanendelea kuomba kulikuwa kuna kundi kubwa la watu ambao walikuwa wanamsubiri Yesu pamoja nao. Hivyo huenda wakati wanafunzi wanaaendelea kuomba walisikia watu wakisema, wanafunzi wa Yohana wenyewe walishindwa kumuombea, wao wataweza, wamejaribu watumishi wa kila aina wameshindwa, huyu hawezekani anasubiri kifo, naam haya yote yakapunguza uhakika ndani yao kwamba kwa jina la Yesu yule kijana anaweza kupona.
  • Maneno yao wenyewe – Biblia haituelezi namna/approach waliyoitumia kuomba/kukemea. Huenda walianza kuomba mmoja mmoja/ au waliomba wachache na mwishowe ndipo wakaomba kama kundi. Kwenye kundi lolote kuna mengi, huenda walipokemea kwa muda kadhaa na bila kijana kuonyesha dalili za kupona baadhi ya wanafunzi wakaingiwa na hofu na wakawaambukiza na wengine na hivyo kushindwa kumtoa pepo. Hebu jaribu kufikiri mtu kama Yuda Iskariote alikuwa anafanya nini wakati wenzake wanakemea?

Nini cha kufanya?
Hofu/mashaka ni silaha kubwa sana ambayo Shetani huitumia kuwafanya watu washindwe kupata majibu ya maombi/miujiza yao kutoka kwa Mungu. Shetani anafahamu kwamba imeandikwa ‘Mwenye haki wangu ataishi kwa imani, naye akisstasita roho yangu haina furaha naye’ (Wabrania 10:38). Hivyo ili kuharibu/kuondoa imani ya mtu kwa Mungu, silaha anayotumia ni kuingiza mashaka moyoni mwake dhidi ya ahadi za Mungu/neno la Mungu kwenye maisha yake. Yesu aliwaambia hivi wanafunzi wake ‘… amini nawaambia yeyote atakayeuambia mlima huu ng’oka ukatupwe baharini, wala asione shaka moyoni mwake, ila aamini kwamba hayo asemayo yametukia, yatakuwa yake’ (Marko 11:22).  

Mpenzi msomaji kamwe usimruhusu Shetani kwa kutumia silaha hii ya mashaka azuie baraka zako na wale wanaokuhusu maishani mwako. Haijalishi jaribu limesimama mbele yako kwa kiwango gani usiondoe imani yako juu ya kile ambacho Yesu amekisema kwenye neno lake juu yako. Naam Mungu wetu si mtu hata aseme uongo, ahadi zake ni amina na kweli.   Naam katikati ya jaribu/changamoto wewe ongeza imani yako kwa kupambana na roho ya mashaka/hofu, naam tumia Biblia ili ikuongoze kukupa mistari ambayo itakuongezea uhakika wa kufanikiwa katika lile ulifanyalo.

Zaidi kuwa makini na maneno ya kusikia kwa habari ya imani yako. Wanafunzi wa Yesu walipaswa kutokujali maneno ya kusikia kutoka kwa watu, au kwa wenzao walioingia mashaka, naam walipswa kudumu kuamini kwamba kijana atapona naam ingekuwa hivyo. Je si unakumbuka habari za Petro alivyoambiwa na Yesu atembee juu ya maji. Awali alianza vema na akatembea hatua kadhaa juu ya maji.    Biblia inasema dhoruba ilipompiga akaona shaka na kuanza kuzama. Kwa nini alizama? si kwa sababu Yesu hakuwepo, bali ni kwa sababu aliona shaka.

Naam kitu kilichopungua kwenye imani ya wanafunzi, ni uhakika kwamba yule kijana atapona. Na kilichopelekea upungufu wao wa imani, si   kutokumwamini/kumjua Yesu, bali ni kuruhusu hofu ichukue nafasi ya imani/uhakika waliokuwa nao kwamba yule mgonjwa atapona. Naam kwa mara nyingine tena ‘usirihusu hofu iharibu muujiza/future yako’.

Neema ya Bwana wetu Yesu Kristo iwe nawe daima.

Mwl. Patrick Samson Sanga
+255 755 816 800