Advertise Here

Monday, April 1, 2013

Waumini wakaguliwa kabla ya kuingia ibadani.

KATIKA hali isiyo ya kawaida Kanisa Katoliki la Mtakatifu Joseph, Jimbo Kuu la Dar es Salaam, juzi liliimarisha ulinzi kwa kila aliyeiingia kukaguliwa na walinzi kwa kutumia machine maalumu ya utambuzi wa vitu vya hatari.

Ukaguzi huo ulifanyika kwenye lango la geti kuu kabla ya kuingia ndani ya kanisa hilo kwa ibada ya mkesha wa sikukuu ya Pasaka ukihusisha Waumini, Watawa, Mapadri, Askofu na watumishi wengine wa kanisa kabla ya kuanza kwa ibada. 

Walinzi wa kampuni binafsi walionekana wakiendelea na kazi hiyo kuhakikisha kila anayeingia kanisani humo haingii na silaha yoyote ambayo ni tishio kwa usalama wa kanisa na waumini wake.

Hatua hiyo imekuja kukiwa tayari kumetokea matukio ya kuchomwa moto makanisa, kuibwa mali za kanisa, na hujuma nyinginezo kwa makanisa maeneo ya Zanzibar na Dar es Salaam na kushambuliwa na kuuwawa kwa viongozi wa kanisa.

Wakizungumzia hatua hiyo, baadhi ya waumini, Neema John na Joseph Mwaipopo, walisema kwa kiasi fulani inashangaza lakini kwa kujiridhisha kwenye suala la ulinzi ni vyema likawa zoezi endelevu hasa ikizingatiwa hali tete iliyopo dhidi ya makanisa.

"Hatukuwahi kufikiri wakristo tutafikia hatua hii ya kutoaminina, tuliabudu kwa wazi bila hofu yoyote, kwa imani za dini zetu Watanzania tunapaswa kumuomba Mungu lulu ya amani tulioyonayo isitoweke," alisema Mwaipopo.

Katika mahubiri yake, Askofu Mkuu wa Jimbo hilo, Polcarp Kadinali Pengo, aliwataka waumini waliobatizwa kwa siku hiyo na wengine kusisimama kwenye imani yao kuwa mfano mzuri kwa wanajamii wengine.

Chanzo: Nipashe