Advertise Here

Monday, August 26, 2013

Mchungaji Kanisa la FPCT acharazwa bakora.

MCHUNGAJI wa makanisa ya Pentekoste yaliyoko katika kijiji cha Buatika katika wilaya ya Butiama, mkoani Mara, amejeruhiwa na kushonwa nyuzi 12 kichwani baada ya kucharazwa viboko na wazee wa kimila wa Kizanaki akituhumiwa kuhamasisha watu kupinga tambiko kwa mizimu.

Mchungaji huyo Yohana Jimwaga wa Kanisa la Free Pentecost Church of Tanzania-FPCT, alifikwa na zahama hiyo juzi majira ya saa 10.00 baada ya kuvamiwa na kundi la wazee hao wakati akiwa njiani kutoka kisimani kuchota maji kwa baiskeli.

Akizungumza na Tanzania Daima kwa njia ya simu jana, Yohana alisema akiwa hajui kinachoendelea ghafla wazee hao wa kimila waliokuwa wamevalia ngozi za wanyama na shanga shingoni, walimvamia na kuanza kumpiga wakidai anaenda kinyume na mila zao.

Kwa mujibu wa Yohana siku mbili zilizopita wazee hao wa kimila waliutangazia umma wa kijiji hicho kuwa hairuhusiwi kufanya kazi zozote za kiuchumi wala kijamii ikiwa ni pamoja na kusomba maji, kuchanja kuni, kupika, kuchinja nyama na kuuza maduka.

Alisema sababu za wazee hao kutangaza hilo ilikuwa kuwataka wakazi hao wajitakase tayari kwa kutambika kwa mizimu ili mvua inyeshe katika maeneo hayo sambamba na kuishawishi iwarejeshee dhahabu katika mgodi wa Buhemba ulioharibiwa na wawekezaji.

Alisema baada ya tangazo hilo la wazee, waumini wa madhehebu mbalimbali ya kidini kwa upande wao hawakulitilia maanani kwa vile haiendani na imani yao hali iliyowafanya waendelee na shughuli zao kama kawaida.

Mchungaji Yohana alisema baada ya wazee hao kuona kwamba wamepingwa na waumini wa dini, waliendesha operesheni maalumu ya kuwasaka viongozi wa dini ikiwa ni pamoja na kuzikamata mali zao ikiwemo mifugo kama faini huku wengine wakiambulia vipigo.

Kamanda wa polisi mkoani Mara Kamishna Msaidizi, Ferdinand Mtui, alipoulizwa kwa njia ya simu alikiri kutokea kwa tukio hilo na kwamba watu 11 wanashikiliwa na polisi kwa mahojiano zaidi huku uchunguzi ukiendelea.

- Habari Leo -