Advertise Here

Saturday, August 24, 2013

Kanisa lapanga kuzika tena mwili wa kasisi uliofukuliwa nchini Kenya.

Dominic Jordan
Maafisa wa polisi wakichunguza kaburi alimozikwa Padre Dominic Jordan katika makaburi ya Mathari Consolata Mission Nyeri Agosti 20, 2013.
MATAYARISHO ya kumzika tena Kasisi Dominic Jordan ambaye mwili wake ulifukuliwa kutoka kwa kaburi lake huko Mathari,Nyeri mnamo siku ya Jumanne yanaendelea.

Makasisi wa kanisa katoliki wamemteua Kasisi Gachanja ili kuandaa  matayarisho  ya mazishi  hayo ambayo yatakuwa ya kipekee kufanyiwa Kasisi wa Kanisa katoliki hapa nchini.

Alhamisi Polisi walithibitisha kwamba mwili wa Kasisi Jordan ulikuwa na viungo vyote huku wakishuku kwamba wahalifu wanaoshukiwa kuchimba kaburi lake maarehemu walikuwa na nia ya kuiba mali.

Mwili huo hata hivyo ulikuwa umeoza  kiasi kwamba ilibidi Mwalimu  mkuu wa shule ya upili ya St.Mary’s aitwe ili kuutambua mwili wa kasisi kwa kutumia mavazi aliyovalishwa wakati wa mazishi yake.

Marehemu Kasisi Jordan alikuwa mwalimu mkuu wa shule hiyo kabla ya kifo chake. Viatu alivyovalia, shungi la nywele kichwani mwake na kola inayovalishwa makasisi wa Kanisa Katoliki ya Kirumi ndivyo vitu vilivyotumika kuutambua mwili wa marehemu.

Kasisi Jordan anasifika kwa kuwasaidia wanafunzi wengi kujiunga na chuo kikuu maarufu cha Harvard huko marekani wakati wa huduma yake.

Akiongea  na Taifa Leo kupitia kwa simu Afisa Mkuu wa Polisi mjini Nyeri  bwana Joseph Mwika alisema tofauti na ilivyodhaniwa hapo awali, ni mwili wa Kasisi Jordan ambao ulitolewa kwa Jeneza na kuwekwa kando  ya kaburi na wala hapakuwa na miili miwili ndani ya kaburi.

Bwana Mwika alisema mwili huo ulipelekwa kwenye chumba cha kuhifadhia maiti cha Hospitali ya Konsolata Mathari huku matayarisho  ya mazizi yakiendelea.

Afisa huyo aliongezea kwamba  uchunguzi bado  unaendelea  lakini itakuwa vigumu kutoa ushahidi kwa bidhaa alizotumia mshukiwa kuchimba kaburi  kwani  mshukiwa huyo alikuwa amevalia glovu kwa mikono yake ili  kuficha alama za vidole.
Glovu alizovalia mshukiwa zilipatikana kando ya kaburi pamoja na jembe na sepetu.

Wakati huo huo Naibu wa Kamishna wa Kaunti ya Nyeri amewataka wakaazi kutohusisha tukio hilo na ushirikina.

Akiongea na waandishi wa habari Naibu wa Kamishna bwana John Marete alisema tukio hilo  lilikuwa ni uhalifu wa kawaida uliotekelezwa na watu waliodhania watapata mali kwenye  kaburi  la marehemu na wala lisihusishwe na  mambo mengine.

“Kama wakristo hatuamini ushirikina, tusifikirie kuna mambo mengine kuhusu tukio hili.Hili ni jambo la haibu na lisilostahili kutendeka katika jamii iliyostaharabika,”akasema bwana Marete.

Kasisi Bartholomew Mwangi  kwa upande wake alisema visa kama hivi vinaonyesha ukosefu wa maandili  katika jamii lakini akasisitiza kwamba  kanisa linatekeleza jukumu lake la kuwafunza wanadamu maadlili mema.

- Swahili Hub -