Advertise Here

Thursday, February 21, 2013

Dar yaibuka kidedea Tamasha la Pasaka.

HATIMAYE Jiji la Dar es Salaam limeshinda katika mchakato wa kuchagua mkoa wa kwanza kati ya saba ambayo Tamasha la Pasaka mwaka huu litafanyika.

Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari jana na Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya tamasha hilo, Alex Msama, ilisema kamati yake iliendesha kura za maoni kwa mashabiki wao, wa eneo lipi tamasha hilo lifanyike.


“Tulifanya kura za maoni kwa njia ya simu za mkononi, pia tulikuwa na vipindi maalumu kwenye baadhi ya redio kwa mashabiki kutoa maoni yao.


“Mikoa ya Dar es Salaam, Mbeya, Dodoma na Mwanza ilikuwa ikichuana vikali katika kupata mahali ambapo tamasha litafanyika, maana tulikuwa bado hatujatangaza.


“Lakini leo tumechagua Dar es Salaam, ambapo zaidi ya mashabiki 15,000 walichagua tamasha lifanyike Dar es Salaam, mashabiki 13,000 walitaka lifanyike Mbeya, mashabiki 7,000 walitaka Mwanza na mashabiki 3,000 walitaka Dodoma,” alisema Msama.

Alieleza kuwa hivi sasa wanatazama mkoa upi lifanyike Jumatatu ya Pasaka na siku zingine zitakazofuata.


“Siku yenyewe ya Pasaka tushapata kwamba ni Dar es Salaam, sasa tunajipanga kwa siku zingine, maana mwaka huu tunataka mikoa saba tufanye tamasha letu,” alisema Msama na kuongeza kuwa kwa Dar es Salaam litakuwa Machi 31.


Pia alisema bado wanaendelea na mazungumzo na wasanii mbalimbali kwa ajili ya kushiriki tamasha la mwaka huu.

- Elizabeth John -