Advertise Here

Saturday, February 16, 2013

Dr. Nchimbi kuwasaka wale wote walioanzisha vurugu Mkoani Geita.

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dr. emmanuel Nchimbi
Serikali imemteua Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Jeshi la Polisi (SACP), Hezron Kigondo, kuongoza uchunguzi kubaini watu waliohusika na vurugu zilizosababisha mauaji ya Mchungaji wa Kanisa la Pentecoste Assemblies of God Tanzania (PAGT), Mathayo Kachila, ili kuwafikisha mbele ya vyombo vya sheria.
 
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Emmanuel Nchimbi, alisema hayo alipotembelea mkoani geita na kukutana na kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa huo na viongozi wa dini za Kiislamu na Kikristo Siku chache zilizopita. Alisema serikali inalaani vurugu hizo, ambazo alisema iwapo zitafumbiwa macho zinaweza kulipasua Taifa vipande vipande.
 
Waziri Nchimbi alisema anashangazwa na matukio hayo kutokea hivi sasa kwa kuwa hapo awali, haukuwapo kwa Watanzania utamaduni na chuki na vurugu.
 
Kutokana na hali hiyo, alisema huenda matukio hayo yakawa ni mbinu za watu wachache zinazolenga kuibua vurugu kwa kutumia kivuli cha dini kuliangamiza taifa, kitendo ambacho alisema serikali haiwezi kukikubali.
 
Awali, akizungumza na waandishi wa habari, Waziri Nchimbi alisema itawasaka kwa hali na mali watu wote waliohusika na vurugu hizo na kwamba, tayari watuhumiwa wawili wameshakamatwa.
 
Akiwa mkoani hapo, Waziri Nchimbi alikutana na kamati ya ulinzi na usalama iliyo chini ya Mkuu wa Mkoa huo, Mh. Said Magalula.
 
Baadaye, alikutana na wawakilishi wa viongozi wa dini ya Kikristo, wakiwamo Mapadri na Maaskofu kabla ya kukutana na viongozi wa dini ya Kiislamu, wakiwamo Masheikh kwenye ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita.
 
Waziri Nchimbi alikutana na viongozi hao kwa lengo la kusikiliza maoni na mapendekezo yao juu ya kupatikana ufumbuzi wa kudumu wa mgogoro uliosababisha vurugu Mkoani humo.