Advertise Here

Thursday, February 21, 2013

Kanisa la TAG Songea latishiwa kuchomwa Moto.

 KANISA la Tanzania Asemblies of God (TAG) mtaa wa Msufini Songea mjini mkoani Ruvuma limetishiwa kuchomwa moto kutokana na maandishi yaliyoandikwa kwenye ukuta wa jengo la kanisa hilo yanayosomeka ‘CHOMA’.

Mchungaji wa Kanisa hilo, Alimosa Mwasangapole alisema ameshitushwa na maandishi hayo kutokana na mfulululizo wa matukio mbalimbali hasa kuchomwa moto makanisa na kuuawa kwa baadhi ya watumishi wa Mungu nchini.

Mwasangapole alisema baada ya kuona maneno hayo alikwenda kutoa taarifa polisi ambao wamemuahidi kulifuatilia suala hilo.

Naye Oliver Richard kutoka Iringa anaripoti kuwa Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Iringa, Dk. Owdenberg Mdegela amezungumzia uhalifu unaoendelea nchini dhidi ya matukio yanayoambatana na mauaji ya viongozi wa dini na uharibifu wa nyumba za ibada.

Dk. Mdegela alisema kwamba uhalifu huo upo nyuma ya vikundi kadhaa vilivyopatiwa mafunzo maalumu nje ya nchi kwa ajili ya utekelezaji wa mpango huo ambao umelenga kuwaangamiza maaskofu na mapadre.

Alisema amewaandikia waraka wanachama wote wa Jumuiya ya Makanisa ya Kikristo Tanzania (CCT) kuanza mara moja mfungo wa saa 24 kuanzia jana.

Hatua hiyo kwa ajili ya kuwasaidia makachero kutoka ndani na nje ya nchi kuwabaini wanaotekeleza mkakati huo dhalimu.

”Vikundi hivyo vinataka kuichafua serikali, kuuvunja Muungano na kuifanya Zanzibar kuwa nchi ya dini.

Serikali ichukue au isichukue hatua sisi tunakwenda madhabahuni na ndiyo maana nimeitisha maombi kwa makanisa yote ambayo ni wanachama wa CCT.

“Ingawa matamko haya hayawezi kumaliza tatizo, tutasugua goti kudhihirisha nguvu ya maombi,” alisema na kuongeza:

”Naagiza kuwe na ulinzi kuanzia geti la mbele la nyuma na kwenye kengele ili wakitokea watu hao, walinzi wapige kengele na kupambana nao”.

- Mtanzania -