Advertise Here

Tuesday, October 16, 2012

Kanisa lingine lachomwa Moto Mkoani Kigoma.

Mchungaji Emmanuel Simon(Aliyeshika Kenchi) akiwa kwenye Kanisa lake lililoteketea kwa Moto. (Picha; Fungo Omary)
 KANISA la Pentekoste(MMPT) lililopo Buronge katika Manispaa ya Kigoma/Ujiji limeteketea kwa Moto baada ya kuchomwa moto na Watu wasiofahamika usiku wa Kuamkia Jana. Mali za Kanisa hilo kama Mabenchi 14, Ubao wa Kufundishia, Mikeka 3 na Mlango 1 viliteketea kwa moto. Jumla ya mali zilizoteketea kwa moto ni Sh.Milioni 1,337,000.
 
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kigoma alisema "Kiini cha tukio hili bado hakijafahamika, na hakuna madhara kwa binadamu. Upelelezi wa tukio hili unaendelea ili kuwabaini wahalifu hao kwa hatua za kisheria."
 
Kwa upande wake Mchungaji wa Kanisa hilo la Pentecoste(MMPT) Bw. Emmanuel Simon(49) alisema kuwa,"Mimi nilipata taarifa kuwa Kanisa langu linateketea kwa moto, na hivyo niliamua kwenda kituo cha Polisi kutoa taarifa, na tulipofika eneo la tukio tukakuta Kanisa lote limeteketea kwa moto".
 
Mchungaji Emmanuel alisema tukio hilo lilitokea juzi majira ya saa 4 usiku katika eneo la Buronge Manispaa ya Kigoma/Ujiji, na kwamba hajui watu waliochoma kanisa hilo, wala hakuna mtu anayeshikiliwa na polisi kuhusiana na tukio hilo.

Mchungaji huyo aliiomba Serikali iangalie sana matatizo ya uchomaji wa Makanisa ambayo sasa yanaenea nchi nzima. Pia amelitaka Jeshi la polisi Mkoani hapo kufanya doria kwenye Makanisa wakati wa usiku ili kukomesha vitendo vya uchomaji wa Makanisa.
 
Alisema kanisa ni taasisi ya jamii hivyo anaomba Serikali ichangie gharama za ujenzi wa jengo hilo ili wananchi wanaoabudu katika kanisa hilo wapate sehemu ya kuabudia.