Advertise Here

Thursday, October 11, 2012

Kanisa la Moravian lamsimamisha kazi mwenyekiti wake.

KANISA la Moravian Tanzania, Jimbo la Misheni Mashariki limemsimamisha kazi mchungaji wake, Clement Fumbo baada ya kubainika kwenda kinyume na taratibu za kanisa hilo.

Fumbo alikuwa ni Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu Jimbo la Mashariki na Zanzibar.

Akizungumza Dar es Salaam juzi, Katibu Mkuu wa jimbo hilo, Mchungaji Adolf Mwakanyamale alisema wamefikia hatua ya kumsimamisha kazi Mchungaji Fumbo, kwa sababu alikuwa anakiuka  taratibu za kanisa.

Pia, anadaiwa alikuwa akiidhinisha hundi tupu bila ya  kuwapo kwa wajumbe wala kufahamishwa.

Mchungaji Mwakanyamale alisema kanisa hilo limefikia uamuzi huo baada ya kikao cha dharura kilichofanyika Oktoba 6,mwaka huu Ushirika wa Moravian, mkoani Morogoro.

Alisema sababu nyingine iliyochangia mwenyekiti huyo kusimamishwa kazi, ni kukosekana kwa ushirikano mzuri katika utekelezaji majukumu ya kanisa kati yake na wajumbe wengine wa kamati ya utendaji.

Pamoja na kukosekana kwa ushirikiano mzuri katika utekelezaji wa majukumu ya kanisa, anadaiwa amekuwa akipinga baadhi ya uamuzi unaotolewa na kuubadili atakavyo na kudharau maazimio halali yaliyotolewa kwenye mkutano mkuu.

Pia, Mchungaji Mwakanyamale  alisema Mchungaji Fumbo alishindwa  kusimamia  vyema Katiba ya kanisa na kanuni zake katika mwenendo wa fedha na mali za kanisa.

“Mchungaji Fumbo amesimamishwa kazi yake ya mwenyekiti baada ya kanisa kubaini kuwa, matumizi mabaya ya mali za kanisa  mfano kuchukua vyerehani vya kanisa vilivyokuwa Ukonga na kuvipeleka mahali pasipojulikana ikiwamo kusaini hundi tupu bila kuwapo wajumbe wa kanisa au halmashauri kuu,” alisema Mchungaji Mwakanyamale na kuongeza:

“Kanisa pia liligundua kuwa  mwenyekiti huyu alikuwa na dharau kwa viongozi wenzake wa kamati tendaji na anawadhalilisha kwa watumishi na wachungaji wengine, pamoja na kwenda kinyume na matakwa ya kanuni na katiba ya kanisa.” 

Anadaiwa kuvunja agizo la Sinodi la kuendelea na ujenzi wa Makao Makuu ya Kanisa la Chamazi na kuanza mchakato wa ujenzi wa makao makuu kuwa Tabata.

Gazeti la Mwananchi